AMESIMAMA mbele ya majengo yake na anaonesha hali ya kuridhika na maendeleo anayofanya katika ujenzi wa hoteli ya kisasa kijijini kwake.
Hoteli hiyo itaongeza kipato chake maradufu. Huu si mradi wake wa kwanza, bali ni wa tatu kwa Mwalimu Salvaus Nindi (40). Yeye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkenda iliyopo kijiji cha Mkenda Wilaya ya Songea Vijijini, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Akiwa pembezoni mwa nchi, Mwalimu Nindi amebadili sura na mwonekano wa mwalimu anayeishi katika mazingira magumu na kuwa wa kupigiwa mfano. Mwalimu Nindi ni mmoja wa walimu wachache, waliofanikiwa japo wametupwa pembezoni bila msaada, wakihudumia watu ambao nao wana matatizo yao ya kiuchumi na kijamii.
Nindi alizaliwa Namatuhi, Songea Vijijini, miaka 40 iliyopita na kufanikiwa kumaliza shule ya msingi mwaka 1987 huko Namatuhi. Baadaye alisoma Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea, na mwaka 1993 alihitimu elimu ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Matogoro
mjini Songea.
“Nilipohitimu elimu yangu ya ualimu, nilipata ajira na kupangiwa kazi Likusanguse. Kijiji hiki sasa hivi kimeingizwa katika Wilaya mpya ya Namtumbo, sikusita kwa sababu nilijua nitaweza, nilikwenda kuanza kazi” anasema.
Nindi anaelezea kuwa alianza maisha kwenye mazingira magumu na katika kipindi cha miaka 3 ya mwanzo, alikaa peke yake na kuamua kutumia fedha zake za mshahara alizopata kupata mapori katika kijiji hicho na kuyageuza mashamba.
Huko ndiko alikoanzia shughuli ambazo zimemfanya kuwa tajiri wa kutosha kwa misingi ya kuweza kujiendesha na kuwa mtu wa mfano kijijini. Ilimchukua miaka mitatu kuweka hali sawa, na kuwa na mtaji, kwani alitumia jembe la mkono kupigania maisha huku akijua kwamba jembe hilo lina kawaida ya kuchosha watu na kukosekana kwa tija.
Akiwa anayajua yote hayo, alidhamiria kuleta utofauti. Akiwa anatumia maarifa ya ualimu,
mwalimu huyo alifanikiwa kuvuna gunia 120 katika eka 6 alizokuwa akizilima. Pamoja na kujishughulisha na kilimo, hakuacha kazi yake ya kufundisha, kwani aliifanya wakati wa muda wake wa ziada na mapumziko.
Kama Wahenga wasemavyo ‘Mchumia juani hulia kivulini’, Mwalimu huyo mwaka 1999 alipata mtaji kutokana na kilimo na akaweza kufungua duka, hali iliyomfanya kuongeza kipato zaidi. Waswahili husema ‘Ng’ombe wa maskini hazai’.
Ukweli wa msemo huo ulijidhihirisha kwa Mwalimu huyo mwaka 2002, ambapo alitakiwa kuondoka katika kijiji Lukusanguse, ambako alikuwa ameanza kuuaga umasikini. Alitakiwa kwenda kufanyakazi katika kijiji kingine.
“Hakika niliyumba, mtaji ulitetereka, lakini nilikaza buti nilipohamia kijijini hapa Mkenda, sikusita kutafuta pori tena na kuanza na kilimo ili kupata mtaji wa kufanyia biashara”.
Pamoja na kutetereka kwake, mkewe ambaye alimuoa miaka mitatu baada ya kuanza kazi, alimpa moyo ajaribu tena maisha ya kulima, kama njia ya kuongeza kipato chake.
Mwalimu Nindi alisema kupitia ushawishi wa mke wake, alitafuta mapori ya kulima katika kijiji cha Mkenda na kweli aliyapata. Mapori hayo kwa mara nyingine tena, ‘yalimtoa’.
Baada ya kuuza mazao yake, aliongeza mtaji na kufanikiwa kubadili biashara kutoka ya duka, alilohama nalo kutoka Likusanguse na kuingia katika biashara ya nyumba ya kulala wageni, ambayo hadi sasa ndio anaendelea nayo.
Kwa mujibu wa Nindi, gesti yake yenye vyumba 10 na kila chumba akiuza Sh 5,000 kwa siku, sasa ameanza kazi ya kutengeneza nyumba ya wageni, yenye hadhi ya kitalii kwa kutumia matofali ya kuchoma.
Kinachomuingizia fedha kwa sasa, si tu nyumba hiyo ya kulala wageni, bali pia baa ambayo anauza vivywaji mbalimbali. Wageni wake wengi ni kutoka nchi jirani ya Msumbiji.
Hakuna mafanikio yasiyokuwa na kikwazo, Mwalimu huyu anasema anakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwamo za kutokuwepo na miundombinu mizuri katika maeneo hayo na huduma za mawasiliano simu, kwani kwa sasa wanatumia mitandao ya Msumbiji, kutokana na kampuni za Tanzania, kushindwa kufikisha huduma hiyo kijijini hapo.
“Mimi nilitaka kusema moja tu ndugu mwandishi. Kuna kazi kwelikweli kuwa mwalimu, tena pembezoni. Lakini mimi sikukata tamaa, niliamua kupambana na katika hilo Mungu amenikubalia” alisema Nindi, akizungumzia maisha ya mwalimu wa kijijini.
Alisema Mwalimu Nindi kuwa alibahatika kupata upenyo wa kuongeza kipato chake na kukomaa, lakini si rahisi hivyo unapokuwa huna huduma yoyote pamoja na kupata mshahara katika muda mzuri.
Anaomba Serikali kusaidia kuhakikisha walimu wanakuwa na uwezo wa kumudu maisha ili waweze kuwafunza vyema vijana, kwani wanaposhindwa kujimudu hali huwa si barabara.
Kuna mambo mengi ya kujivunia kwa mwalimu huyo na yenye mfano kwa walimu wenzake wengi.
Lakini pia kijijini hapo, amekuwa kama kiongozi katika jamii inayomzunguka. Ni mtu wa watu, anapendwa na wapitanjia na hata wanaoishi hapo.
habari nzuri sana,hii mwalimu huyu awe mfano kwa walimu wengine wanaodai mishahara kila kukicha, kumbe maarifa zaidi ndiyo yanayohitajika katika kuzalisha na kumudu maisha. Big up mwalimu, nashukuru Latifa kwa makala hii nzuri ya kijamii na ya tofauti na makala ambazo niwahi kuzisoma kila la heri.
pongezi nampa mwalimu kwa juhudi zake za kupambana na umaskini.ombi langu kwake asizame zaidi kwenye biashara na kusahau kuwafundisha watoto wetu.mwajiri naye asimwamishe tena kwani mwalimu huyu ameshamudu kupambana na mazingira magumu ya kijijini ambayo walimu wenzake wanayakimbia.
hongera sana mwalimu. naamini kupitia makala hii. hakuna tena mwalimu ambaye atakataa kwenda kituo cha kazi atakachopangiwa kwani mafanikio huja mahali popote na muda wowote kikubwa tu nikuonesha juhudi na kumuomba Mungu.
PONGEZI KWA MWANDISHI,KWA KUTAFUTA NA KUTOA HABARI HII MUHIMU ILIKUTOA MSUKUMO CHANYA KWA WALIMU NA WATUMISHI WA SERIKALI WANOKATAA KUFANYA KAZI VIJJINI.GOD BLESS YOU.
hongera sana mwalimu.nimejifunza kutoka kwako,jamani watu wote wangefuata mfano wa huyu mwalimu hakungekuwa na shida yoyote.kwa hivyo mimi niko nyuma kufuata mfano wako.ahsante.
Hongera sana mwandishi pamoja na mwalimu. Nakuomba sana mwalimu elimu hii uwapatie na vijana wanaokimbilia mijini wakitegemea huko mambo mswano kumbe kitanzi!!
Apongezwe sana huyo mwalimu kwa jitiada zake za kimaendeleo na ni moja ya funzo kwa vijana wengi kwamba tusikate tamaa kimaisha tufanye jitiada ili tuweze kuendelea kimaisha kamw alivo unesha huyo mwalimu..!!
kilimo kweli kinalipa!mabadiliko ya hali ya hewa yatatupa upenyo wa kufikia malengo?kama sio ndoto za kujipa moyo?binafsi nakiwaziwa,mungu atubariki,atupe sawa na tuombavyo,namuomba hali njema ya hewa kufikia malengo!