UPUNGUFU WA CHAKULA NA TATIZO LA MAJI MAGANZO.

Belinda Habibu

Kijiji cha Maganzo kimo katika kata ya songwa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga,ambacho kina wakazi wapatao 11868,wanaume 7349 na wanawake 4519.
Kijiji hiki kinakaribia kupewa hadhi ya kuwa mji mdogo lakini kinakabiliwa na changamoto kibao ikiwemo ya ukosefu wa chakula,ardhi kwa watu wake haitoshi na tatizo la maji salama ya kunywa .
Ukiwa kijijini hapa kila siku karibu wakati wote utashuhudia wapanda baiskeli wakiwa wamebeba madumu ya maji wakitokea wengine kwa mwekezaji wa almasi Wiliamson Dioamond kuchota maji.
Ki mtazamo utafikiri watakuja kuyagawa bure laa hasha,dumu moja linauzwa sh.400,kama unafamilia ya watu sita na kuendelea basi hali itakuwa ngumu zaidi kwako.
Afisa kilimo kata ya Songwa Steven Kasoni alisema suala la maji limekuwa tatizo sugu na dumu moja linauzwa na wachotaji kwa sh.400, na maji hayo si safi na si salama.
Wakati kuna shida ya maji pia ukame ulioikumba wilaya ya Kishapu umeathiri pia kijiji hiki kwa hali ya chakula na kuilazimu ofisi ya kijiji kuomba chakula kutoka serikali kuu.
Mkazi wa kijiji hicho Benjamini Shimba alisema ni kweli wanakabiliwa na njaa kwa kuwa wengi hawana maeneo ya kulima baada ya kuyaachia kwa shughuli za uwekezaji wa almasi.
“Mimi najishughulisha na biashara ya kuuza maji na ninayatoa mgodini Mwadui ama kuna bwawa maeneo ya Songwa,ili familia ipate mlo wa siku”alisema Shimba.
Afisa kilimo wa kata ya Songwa ambako Maganzo inapatikana tena alisema waliomba serikalini msaada wa chakula na kupata tani 124.6 za mahindi mwezi Desemba mwaka jana 2012,kwa wahitaji 25,164 ili kukabiliana na njaa iliyoikumba sehemu hiyo.
Ameongeza waliopata walikuwa watu 2597 tu na hawakuwa na jinsi kwa kaya zingine kwani kiasi kilichoombwa na walichopata ni tofauti na kuongeza kama wangepata tani 405.7 ingetosha kuwavukisha msimu mzima wa kilimo.
Afisa huyo alisema vigezo wanavyotumia kuwapata wenye hali mbaya sana ya njaa, ni kwa kupitia mikutano ya hadhara.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Maganzo Thobias Misalaba amesema ni kweli hali ya kukosekana kwa chakula ni mbaya kwao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukame wa miaka mine mfululizo,unaosababisha mazao kukauka.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

1 Comment
  • Ni kweli kuwa uwepo wa migodi mingi kama WDL,Fantom, El-ilar-Sudi na mengine mengi hayaja msaidia mtanzania hasa anayeishi katika eneo hili la wilaya ya kishapu. Hasa tunahjiuliza kuwa Uwekezaji mkubwa na mdogo unawasaidiaje watanzania?

       Wananchi wa Maganzo, Utemini , Idukilo, Nyenze, Songwa pamoja na Ikombabuki wana hali mbaya sana. Mimi ningeishauri serikali wawalazimishe wawekezaji kuwapa wananchi huduma muhimu kama maji, afya, pamoja na elimu ili kupunguza umasikini ulio kithiri hapa wilayani kishapu.

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *