UHABA wa walimu wa masomo ya sayansi nchini umesababisha mwalimu mmoja wa sayansi katika Shule ya Sekondari Mbagala jijini Dar es Salaam kulazimika kufundisha watoto 666 wa kidato cha kwanza, FikraPevu inaripoti.
Hali hiyo inaelezwa kuchangiwa na mpango wa elimu bure, ambapo kumekuwepo na ongezeko kubwa la uandikishaji wanafunzi, hususan mwaka huu 2017, kuliko idadi ya walimu waliopo.
Mwalimu Bugwema, ambaye ni mkuu wa taaluma shuleni hapo, amesema kwamba, masomo yote manne ya sayansi – Hisabati, Fizikia, Kemia na Baolojia – yana mwalimu mmoja mmoja ambaye analazimika kufundisha watoto wote 666 wa kidato cha kwanza – wavulana 243 na wasichana 423 – waliopo katika mikondo 13.
“Tuna hali mbaya sana kwa masomo ya sayansi kwa kidato cha kwanza mwaka huu, kwa sababu mwalimu mmoja ana takriban vipindi 66 kwa wiki badala ya vipindi 30, jambo ambalo ni mzigo mkubwa,” alisema Mwalimu Bugwema katika kikao cha wazazi kilichofanyika leo hii.
Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Silvia Sebastian, amesema wana changamoto kubwa ya uhaba wa walimu huku idadi ya wanafunzi ikiwa kubwa.
Amesema kwamba, wamepeleka maombi muda mrefu kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kuomba kuongezewa walimu, hususan wa masomo ya sayansi, lakini bado maombi hayo hayajapatiwa ufumbuzi.
“Kesho mimi na mjumbe mmoja wa Bodi ya Shule tunatarajia kwenda kuomba miadi ya kuonana na Mkurugenzi ili kumweleza mzigo mzito tulionao pamoja na maombi yetu ya kupatiwa walimu wa sayansi, hali ni ngumu sana wazazi na ndiyo maana tumewaita ili tujaribu kuangalia ni namna gani kwa pamoja tunaweza kutatua changamoto hii katika kuwajengea msingi imara watoto wetu,” alisema Mwalimu Sebastian.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1982 na walimu 68 tu, huku wengi wao wakiwa ni wa masomo ya sanaa na biashara.
Kulingana na idadi hiyo, ina maana kwamba wastani wa jumla wa mwalimu kwa wanafunzi ni 1:23, lakini katika uhalisia wake mgawanyo unawaelemea zaidi walimu wa sayansi hata kwa vidato vingine kwa kuwa wako wachache. Walimu wa kidato cha kwanza jumla yako wako 14, ukiwa ni uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 48.
FikraPevu ilihudhiria mkutano huo ambapo mbele ya wazazi 384, Mwalimu Bugwema amesema kwamba, uhaba wa walimu ni changamoto kubwa inayosababisha kushuka kitaaluma kwa wanafunzi na kwamba hata matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka 2016 hayaridhishi.
“”Mwaka 2016 wanafunzi wa kidato cha pili waliofanya mitihani walikuwa 473, lakini waliopata daraja la kwanza walikuwa 21 tu huku wengine 94 wakifeli kwa kupata daraja 0,” alisema.
Aliongeza kwamba, waliopata daraja la pili walikuwa 34, daraja la tatu 55 na daraja la nne walikuwa 249, matokeo ambayo yanakatisha tamaa ingawa alisisitiza kwamba ukosefu wa walimu wa kutosha, hasa wa sayansi, ni changamoto kubwa.
Hali hiyo imewalazimu wazazi waliohudhuria kikao hicho kuamua kwa nia moja kuangalia uwezekano hata wa kuwaajiri walimu 6 wa muda wa masomo ya sayansi kwa kidato cha kwanza ili wafundishe watoto wao kwa gharama zao wenyewe.
Maazimio hayo ya wazazi, ambayo yalifanyika baada ya kuwaomba walimu waondoke kwa kuwa hayawahusu, ni pamoja na kutafuta mwalimu mmoja wa Fizikia, mwalimu mmoja wa Kemia na walimu wawili wawili kwa masomo ya Baolojia na Hisabati.
“Jamani serikali imesema elimu ni bure, lakini kwa changamoto hii wanayokabiliana watoto wetu lazima tutafute namna hata ya kuchangishana tutafute walimu wa sayansi wawafundishe wanetu kwa sababu mpaka sasa serikali bado haijaajiri watumishi, wakiwemo wa sekta hii ya elimu,” walisema wazazi hao katika makubaliano hayo.
Aidha, wamekubaliana pia kugharamia mitihani ya kujipima ya watoto hao walau mara moja kwa mwezi ili kujua uwezo wao na maendeleo.
Kwa kauli moja walimchagua Deodatus Magomba kuongoza Kamati ya Watu Watano itakayosimamia na kuratibu zoezi la kukusanya michango kwa wazazi.
Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo ni Mussa Shaaban (Katibu), Ally Said Magani, Salma Mtei na Sarah Mwanginde.
Kamati hiyo inalazimika kuandika muhtasari na kupeleka maombi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ili kuridhia wao kama wazazi watafute walimu wa muda kwa gharama zao kufundisha watoto wao hadi hapo serikali itakapoajiri walimu wa kudumu.
Hata hivyo, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Sebastian amezitaja changamoto nyingine zinazoikabili shule yake kuwa ni ukosefu wa uzio ambao unasababisha watoto kuzurura ovyo hata nyakati za masomo, jambo ambalo amesema atalikumbusha pindi atakapokutana na Mkurugenzi wa Manispaa.
Kuhusu changamoto ya vyumba vya madarasa, Mwalimu Sebastian amesema wana uhaba mkubwa ingawa kwa sasa jengo jipya litakalokuwa na vyumba vinne linajengwa.
“Idadi ya wanafunzi ni kubwa mno, tumeamua kuwagawa kwa makundi, ambapo kidato cha kwanza na cha tatu wanaingia mchana kwa sababu vyumba havitoshi… kukamilika kwa jengo hilo kutapunguza adha hiyo, lakini bado vyumba zaidi vinahitajika,” alisema.
Awali, Mwalimu Abihudi, ambaye anashughulikia nidhamu, aliwataka wazazi washirikiane kuhusu suala la nidhamu na utoro, ambao unachangia kushuka kwa maendeleo ya kitaaluma shuleni hapo.
“Japo kuna sababu nyingine kama utoro na watoto wenyewe kutokuwa tayari kujifunza, lakini endapo uzio utajengwa utasaidia kuzuia watoto wasitoroke maana ni vigumu kwa hali ya sasa kuwachunga watoto zaidi ya 1,000,” alisema.
Akaongeza: “Suala la nidhamu linaanzia nyumbani kwa sehemu kubwa, mimi mwalimu kazi yangu kumfundisha tu mtoto na kumlea kitaaluma na kimaadili, lakini wazazi ndio wenye sehemu kubwa ya kujenga nidhamu ya watoto wao. Wahimizeni waachane na makundi na kama mtawalea katika imani ya kidini itasaidia sana kuliko baadhi yenu kutuletea wanenu eti ‘wamewashinda’. Sasa kama ninyi wazazi watoto wenu wamewashinda, mimi mwalimu nitamfanyaje?”