KILA mtu anasema kwamba ukeketaji ni mbaya na hakuna mtu anayeuliza kiundani kwanini ukeketaji. Makala haya ya SHOMARI BINDA yanatafuta majibu ya kweli kutoka kwa wenyeji wanaofanya tohara hiyo.
WANAUME katika maeneo haya ya ukeketaji wanatambua uhusiano wa tohara ya kike na juhudi za kumfanya mwanamke kubaki kuwa chombo cha kufyatua watoto pekee.
Ziko mila zinazoamini kuwa mwanamke asipokeketwa hulemewa na shauku ya ngono wakati wote, hivyo kushindwa kuitunza ndoa, sambamba na kuzembea katika masuala ya kiuchumi!
Utafiti wa JamboTanzania, umebaini hilo baada ya kuwahoji baadhi ya wazee wa kimila katika makabila ya Wakurya, Wangoreme, Wazanaki, Wanata, Wakiroba na Wasimbiti yaliyopo ndani ya mkoa wa Mara, ambako shughuli hiyo imekuwa ikifanyika mara kwa mara hasa nyakati za likizo za wanafunzi.
Uchunguzi huo unaonesha kwamba ukeketaji limekuwa ni tendo muhimu miongoni mwa jamii hizo kutokana na ukweli kuwa mwanamke kwa mujibu wa wazee wa kimila, ndiye nguzo muhimu ya familia.
Katika mazungumzo na wazee hao walitoa sababu kadhaa ikiwamo wajibu wa kuzaa watoto na kutegemewa katika shughuli zote za kiuchumi ndani ya familia, kama vile kutunza familia pamoja na mumewe, kutunza mifugo, kulima mashamba na kufanya biashara mbalimbali za kukuza pato la familia yake.
Hivyo basi ili kumfanya atulie nyumbani na kuweka mawazo yake yote katika majukumu hayo na mengineyo ya kifamilia, ni lazima afanyiwe tohara (ukeketaji) kwa kumuondoa baadhi ya viungo, ambavyo kwa mila na desturi ya jamii hiyo, wanaamini humfanya mwanamke asitulie nyumbani!
Sababu ya pili ya mwanamke kufanyiwa tohara kutokana na maelezo ya wazee hao ni kutokana na imani kuwa, humfanya asitamani tendo la ndoa, hivyo kwake yeye tendo hilo kamwe lisiwe kwa ajili ya kukidhi tamaa za kingono (na mtu yoyote yule) bali liwe kwa ajili ya uzazi tu, maalum kwa yeye na mumewe. Kama anavyosema mzee wa kimila, Mwekwabhi.
“Sikiliza tata (baba); tangu zamani wanaume wa kabila la Kikurya na makabila mengine madogo ya jamii hiyo wanaokeketa wanawake, wamekuwa wavivu na wakiwategemea sana wake zao kiuchumi, ndiyo maana wamekuwa wakiwakeketa ili kuwafanya wasizurure huku na huko, bali wakae nyumbani wakitunza familia, mifugo na mashamba” anasema Nyamuhanga Mwekwabhi wa kijiji cha Buhemba.
“Unajua baba hii mila imekuwa ikimfanya mwanamke kuwa kama chombo cha kuzaa watoto, kuwatunza na kubeba majukumu yote ya familia,..” anasema mama Wegesa Matiko, mkazi wa kijiji cha Nyankanga wilayani Butiama.
Bibi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mama Nyankani, Ngariba mstaafu na mkazi wa wilayani Serengeti, mkoa wa Mara anakiri kuwepo ukweli katika utafiti huu wa ‘Jinsi mila na desturi potofu zinavyochangia ukeketaji’ ingawa anadai kwa sasa hali hiyo imeanza kupungua kutokana na imani za dini, elimu na ukali wa sheria za nchi.
“Ni kweli zamani ilikuwa hivyo kama walivyokueleza wenzangu, hayo ndiyo yalikuwa baadhi ya malengo ya kuwakeketa wanawake, lakini siku hizi mambo yamebadilika, watu wameelimika, wanajua madhara ya kufanya hivyo na hata mambo ya dini na ukali wa sheria umesaidia kupunguza hali hiyo” anasema.
Mganga wa Halimashauri ya Wilaya ya Tarime Charles Samson ameelezea madhara makubwa ambayo wanayapata wale wanaofanyiwa ukeketaji na wengine kupelekea vifo kutokana na kung’ang’ania mila hiyo.
Anasema licha ya kuwasababishia maumivu makali wakati wa tendo la ukeketaji wamekuwa wakitokwa na damu nyingi na wengine tendo limekuwa likiwaharibu maumbile na kupelekea hatari wakati wa kujifungaua.
Baadhi ya wahanga wa ukeketaji wakiwemo wasichana wadogo na akina mama ambao wamezungumza na mwandishi wa Makala hii wameelezea kuonekana watu wa ajabu kwenye jamii kutokana na kufanyiwa ukeketaji na hata kuchekwa kila wanapopita mitaani.
Mmoja wa wasichana ambaye alikimbia kuogopa kufanyiwa ukeketaji na kwenda kuomba msaada wa hifadhi kwenye kituo cha kuhifadhi wasichana cha Masanga kilichopo wilayani Tarime alidai kilichomfanya kukimbia ni pale aliposimuliwa na dada yake aliyefanyiwa ukeketaji na kutokwa na damu nyingi na kupoteza fahamu.
“Hao waliosema wanaondoa utamu ili mwanamke abaki nyumbani ni waongo mimi ninao ushahidi wa kutosha kwa wasichana waliofanyiwa ukeketaji na hivi leo hapa Tarime ndio”Malaya”na wanafanya biashara za kujiuza mjini,”anaeleza mtaalamu wa saikolojia Kulwa Japhet kutoka Taasisi ya ABC Youth ya Tarime.
Licha ya kuwepo jitihada kadha wa kadha za kudhibiti vitendo vya ukeketaji kwa wanawake, bado inasemekana wapo wanaoendelea kisiri kutekeleza mila hiyo potofu, huku wakitumia mbinu mbalimbali za kuhakikisha kuwa mwanamke hajishughulishi kabisa na masuala ya ngono ya starehe, zaidi ya uzazi pekee!.
Mbinu hizo mpya ni pamoja na kutokukata kwa kuondoa kabisa vinembe (clitoris), bali kwa mujibu wa manju mmoja mstaafu, wamekuwa sasa wakividunga kwa vitu vyenye ncha kali kama sindano, ili kuvifanya visinyae kabisa kwa kuvia damu na kuwa baridi, hivyo kushindwa kabisa kuhisi chochote ingawa vinakuwepo sehemu zake.
Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Tarime Mwambala Mwambala ameelezea baadhi ya jamii kuendeleza mila za ukeketaji unaoleta athari licha ya kutolewa elimu juu ya kuachana na ukeketaji huo.
Anasema elimu zimekuwa zikitolewa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazopingana na mila potofu ya ukeketaji kwa kuiendea jamii na kuelezea athari zake na kudai jambo hilo litafanikiwa kwa jamii kubadilika na kuamua kuachana nayo.
Mwambala anasema utamaduni wa kumfanyia Mwanamke ukeketaji ili awe kitega uchumi kwa madai ya kumpunguzia hamu ya kufanya mapenzi haupo na kudai kila mmoja anapaswa kuwa muwajibikaji kwa nafasi yake na kuachana na mila potofu.
“Siku hizi bwana, kama kuna mwanamme anayeota kumtegemea mke wake katika masuala ya kiuchumi kwa kigezo cha ukeketaji, basi ategemee kufukuzwa na familia yake aende anakojua, elimu na dini imevunja kabisa hizo mila potofu” anasema Mwambala Afisa Utamaduni Wilaya ya Tarime.
Lakini pamoja na ukweli huo wote, inasemekana pia zipo tafiti nyingine zinazoonesha kwamba, kati ya mabinti kumi ni mmoja tu anayelazimishwa kufanyiwa tohara, huku tisa wakienda kwa hiari yao kwa sababu kama vile mkumbo rika, kujengewa moyo wa ujasiri na fahari kutoka kwa wazazi wao, ama kutishwa kupatwa na madhara kama wasipofanya hivyo, au kutengwa katika masuala muhimu ya kifamilia n.k.
Ili kuifanya jamii iondokane na mila hii potofu, jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali na mashirika binafsi ya kijamii, kwa kufanya semina na makongamano ya kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za ukeketaji na jinsi ya kukomesha mila zinazochangia uwepo wa hali hiyo.
Ni wajibu sasa kwa Viongozi wa dini kuzungumzia athari za ukeketaji kwa njia za mafundisho ya dini, huku pia serikali ikishauriwa kuangalia uwezekano wa kuweka kwenye mitaala yake ya elimu, somo juu ya athari za ukeketaji hasa kwenye mikoa iliyoathiriwa na mila hizo.
Hilo linaweza kusaidia kupunguza kama siyo kumaliza kabisa mila hiyo potofu ya ukeketaji wa wanawake, ingawa pia iko haja ya kuwatafutia Ngariba wote shughuli mbadala ya kuwaingizia kipato, ikiwa ni pamoja na kuwatumia Ngariba hao hao, pamoja na Wazee wa Kimila kutoa elimu ya madhara juu ya ukeketaji.