Kudorora kwa bandari ya Kigoma kumalizwa na reli ya kati

Emmanuel Matinde

Bandari ya Kigoma, ni moja ya bandari mbili kubwa ambazo zinamilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Nyingine ni bandari ya Kasanga pamoja na bandari nyingine ndogo ndogo 19.

Bandari ya Kigoma ilijengwa kati ya mwaka 1922 na 1927 na serikali ya Ubelgiji, na kuanza kufanya kazi mwaka 1927. Ina uwezo wa kuhudumia tani 680,000 za shehena mchanganyiko kwa mwaka kupitia magati matatu, Gati la mizigo(Cargo Terminal),Gati la Abiria(Passangers Terminal) na Gati la Mafuta(Oil Jetty Terminal).

Gati la mizigo lina urefu wa mita 301 na kina cha maji cha mita 4, lina uwezo wa kuhudumia tani 500,000 kwa mwaka. Gati la abiria lina urefu wa mita 100 na kina cha maji cha mita 3, likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria 300,000 na shehena mchanganyiko tani 150,000 kwa mwaka.

Gati la mafuta lina urefu wa mita 202.7 na upana wa mita 6, likiwa na uwezo wa kuhudumia tani 30,000 za shehena ya mafuta kwa mwaka.

Bandari ya Kigoma ilijengwa mahsusi kama lango la kupitishia bidhaa mbali mbali kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi kituo cha mwisho cha reli ya kati kilichojengwa karne ya 20 kwa ajili ya kusafirisha bidhaa za kilimo kutoka nchi za ndani ya bara la Afrika kuja mwambao wa Afrika Mashariki hususan katika nchi ambazo hazina bahari.

Bandari hii pia ni muhimu sana kwa uchumi na ustawi wa mkoa wa Kigoma na ndiyo inategemewa na wananchi wa mkoa wa Kigoma na mikoa jirani, katika utoaji wa huduma ya usafirishaji wa bidhaa zinazopitia reli ya kati kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tena kwa gharama nafuu.

Kulingana na mkuu wa bandari ya Kigoma Patrick Namahuta lengo la kujengwa bandari lilifikiwa kwani meli za kutoka nchi za Congo DRC na Burundi, kwa muda mrefu zimekuwa zikitumia bandari hiyo kusafirisha mizigo inayotoka ndani na nje ya nchi kwenda katika nchi hizo.

Hata hivyo wakati lengo la bandari hiyo likiwa ni kuendelea kutoa huduma hizo kwa miaka mingi zaidi, changamoto mbali mbali zinakabili bandari ya Kigoma ikiwemo kushuka kwa kiwango cha utendaji.

Mfano Mwaka 2007/2008 Bandari ilihudumia tani za mizigo 79,031, mwaka 2008/09, tani 116, 750, mwaka 2009/10, tani 65,797, mwaka 2010/11, tani 38,525, mwaka 2011/12, tani 56,176 na mpaka Disemba mwaka jana , tani 21,000.

Kati ya mwaka 2007 mpaka 2013, gati la abiria lilihudumia jumla ya abiria 156,082, wakati gati la mafuta lilihudumia shehena ya majimaji tani 72,295 katika kipindi cha mwaka 2008 mpaka 2013.

Mwaka 2006 na kurudi nyuma bandari ya kigoma ilikuwa inapokea behewa kati ya 20-40 ya mizigo kwa siku na behewa moja linachukua tani 40 lakini kufikia mwezi Septemba mwaka juzi wakati naibu waziri wa uchukuzi Charles Tizeba anatembelea bandari ya Kigoma, kulikuwa na wastani wa behewa moja tu kwa siku na wakati mwingine ilishuka mpaka 0.9.katika mwaka.

Sababu kubwa ya kushuka kwa kiwango cha utendaji wa bandari ya Kigoma inatajwa kuwa ni uchakavu wa miundombinu ya reli ya kati, kwa kuwa shehena nyingi inayohudumiwa na bandari hiyo inategemea ufanisi wa usafiri wa njia ya reli ya kati ya Dar es Salaam na Kigoma.

Kutokana na uchakavu wa reli ya kati bandari ya Kigoma imekuwa ikipokea wastani wa mabehewa kati ya matatu na matano kwa juma katika siku za hivi karibuni na hivyo kukatisha tamaa wafanyabiashara ambao wanaamua kusafirisha mizigo yao kwa njia ya barabara kupitia korido ya katiinayoanzia bandari ya Dar es Salaam.

Uchakavu wa miundombinu ya reli umesababisha wasafirishaji kupoteza imani kwa usafiri wa treni kusafirisha mizigo yao kutokana na kutokuwa wa uhakika kwani mizigo imekuwa ikichelewa kufika bandarini wakati mwingine miezi mitatu au zaidi.

Korido ya Kati inaanzia Bandari ya Dar es Salaam na kupitia reli ya kati hadi upande wa mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Burundi kupitia Kigoma kwenye Ziwa Tanganyika hadi Rwanda kupitia Bandari ya Nchi Kavu ya Isaka na hadi Uganda kupitia Mwanza kwenye Ziwa Victoria.

 Korido inatoa umbali wa karibu zaidi kati ya Bandari ya Dar es Salaam na nchi za bara zisizo na bahari zifuatazo: Dar es Salaam-Kigoma-Bujumbura kwa barabara/reli na ziwa kilomita 1,436; Dar es Salaam-Kigoma-Kalemie kwa barabara/reli na ziwa, kilomita 1,374; Dar es Salaam-Isaka-Kigali kwa reli na barabara, kilomita 1,463 na Dar es Salaam-Mwanza-Portbell kwa reli na ziwa, kilomita 1,581.

Njia ya barabara kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro-Dodoma-Manyoni-Singida-Nzega-Kahama-Rusumo na Kobero au Dar es Salaam-Kigoma-Bujumbura kwa barabara ndio imekuwa njia kuu ya kusafirisha mizigo kwenda katika nchi za, Rwanda na Burundi.

Uchunguzi uliofanywa namwandishi wa makala haya, umebaini kuwa tangu mwezi Januari mpaka Novemba mwaka jana hakuna mzigo wowote unaokwenda nchi ya Burundi uliopita katika bandari ya Kigoma kwa sababu wasafirishaji wa mizigo kwenda nchini humo hutumia usafiri wa barabara.

Ubovu wa miundombinu ya reli ya kati haujaathiri tu wafanyabishara wasafirishaji mizigo pia umeathiri maelfu ya wananchi wa mkoa wa Kigoma na maeneo mengine ambako reli ya kati inapita hasa wenye kipato cha chini ambao usafiri wa treni umekuwa ndio tegemeo lao kubwa kwani ndio usafiri nafuu zaidi ukilinganisha na usafiri mwingine.

Sekta ya kilimo na uvuvi pia zimeathirika na hivyo wananchi wengi pia kuathirika kiuchumi.

Dkt. Audas Bilame mkuu wa kitivo cha Sayansi na jamii na mawasiliano katika chuo kikuu cha mtakatifu Augustino anasema kutokufanya vizuri kwa reli ya kati kumeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo.

Anasema mchango wa sekta ya kilimo kwenye pato la taifa katika miaka ya 80 wakati ambapo reli ilikuwa imara ulikuwa asilimia 50% lakini hivi sasa imeshuka sana mpaka kufikia asilimia 21% na kwamba uchakavu wa miundombinu ya reli umechangia hali hiyo.

“Kiuchumi serikali inaathirika kwa kukosa mapato na mwananchi mmoja mmoja ambaye reli ilikuwa ikimsaidia kusafirisha mazao mbali mbali ya kilimo na uvuvi pia anaathirika,” anasema Dkt. Bilame na kuongeza kuwa,”wakati usafiri wa reli ulipokuwa imara ilikuwa ni rahisi mkulima akishavuna mazao yake kuyasafirisha kwenda kwenye soko lakini kwa sasa ni vigumu kusafirisha hivyo watu wanalima vyakula lakini wanauza kwa bei ndogo.

Anasema zamani reli ilipokuwa ya uhakika dagaa na samaki aina ya migebuka wanaovuliwa Kigoma katika ziwa Tanganyika walikuwa wakipatikana katika masoko ya Dodoma, Tabora, Dar es Salaam na maeneo mengine wakiwa bado na ubora wao.

Sekta ya ajira nayo imeendelea kuathirika katika bandari ya Kigoma.Wengi waVijana wanaofanya kazi katika bandari hiyo hawana ajira za kudumu kwa sababu shughuli za ubebaji mizigo zimeendelea kupungua. Ajira za bandarini sasa hivi zinategemea kiwango cha mizigo inayofika bandarini.

Wasafirishaji mizigo mathalani kutoka nchi ya Jamhuri ya watu wa Congo DRC ni lazima watumie bandari ya Kigoma na ndio wadau wakubwa wa bandari, lakini pia ni waathirika wakubwa wa reli ya kati.

Bi.Mwema Bulugu ni meneja katika kampuni ya usafirishaji ya serikali ya DRC,Société Nationale des Chemins de Fer du Congo (SNCC), anasema matatizo yaliyopo kwenye miundombinu ya reli yanawaathiri kwa kiasi kikubwa.

“Sisi tunapenda reli iwe nzuri kwa sababu kazi yetu inakuwa ngumu, muda mwingi tunakaa tu ofisini hakuna mzigo,”alisema na kuonesha kusikitika.

Nae Abdallah Mohamed wa kampuni ya kusafirisha mizigo ya ABS MAMRY kutoka Jamhuri ya Kidemoklasia ya Congo DRC anasema miaka ya nyuma walikuwa wakifanya safari kumi kwa mwezi au zaidi kwa kuwa mizigo ilikuwa inafika kwa wakati kupitia reli ya kati.

“Sasa hivi mizigo mpaka ifike hapa bandarini ni miezi mitatu au wakati mwingine inakuja kidogo kidogo kwa hiyo inabidi tusubiri kwa sababu hatuwezi kuondoa meli hapa ikiwa na mzigo kidogo wakati meli moja tu ina uwezo wa kubeba tani 600, ni hasara,”alisema Abdallah na kuongeza kuwa wanalazimika kulipa dola moja kila siku kama gharama ya kuhifadhi mzigo bandarini na baada ya siku 15 gharama hiyo huongezeka zaidi.

Je nini kifanyike ili kiwango cha utendaji cha bandari ya Kigoma kiwe kinachoridhisha?

Mkurugenzi wa sera na ushawishi kutoka Shirikisho la viwanda Tanzania (CTI), Bw.Husein Kamote anasema Serikali itaheshimika sana na kuaminika kwa wananchi na wadau wengine pale ambapo itatekeleza yale ambayo inayapanga kwa vitendo badala ya kuahidi tu kwa maneno.

Anaongeza kuwa duniani kote reli na bandari ndio kiungo kikuu katika kukua kwa uchumi kwa kasi kubwa kwa kuwa mizigo mingi mizito hubebwa na reli na bandari na hivyo ameshauri serikali kuharakisha kuboresha reli ya kati kama kweli ina dhamira ya kuinua uchumi wan chi..

Hata hivyo anapendekeza kuwa wakati umefika kwa sekta binafsi ambazo zina uwezo wa kuchangia kuboresha miundombinu ya reli ya kati kama vile kununua vichwa vya treni na mabehewa ziruhusiwe kufanya hivyo akitolea mfano kampuni ya Bakhessa ambayo imenunua mabehewa yake kwa ajili ya kusafirishia bidhaa zake.

“Nafikiri sasa badala ya kufikiria kwamba serikali peke yake inaweza kununua hivyo vichwa vya treni au mabehewa sekta binafsi ziruhusiwe kununua ili walete changamoto katika usafiri wa reli ya kati na kuongeza ufanisi kwenye bandari ya Kigoma.

Kwa upande wa serikali, kumekuwepo na mipango na ahadi mbali mbali za kuboresha reli ya kati ikiwa ni pamoja na kubinafsisha Shirika la reli TRL lakini ubinafsishaji huo haukuleta matokeo tarajiwa.

Mfano ni mpango wa biashara wa kampuni ya reli Tanzania (TRL).

Ikumbukwe kuwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ilianzishwa mwaka 2007 kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Na.12 ya mwaka 2002 kama Kampuni binafsi inayomilkiwa na serikali ya Tanzania (49%) na RITES ya India (51%).

Kabla ya kuanzishwa TRL Reli ya kati ilikuwa ikiendeshwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) lililokuwa linamilikiwa na Serikali kuanzia 1977. Kuanzishwa kwa TRL ilikuwa matokeo ya sera ya Serikali ya kuongeza kasi ya maendeleo ya uchumi kwa kubinafsisha uendeshaji ukiwemo Makampuni yaliyokuwa yanamilikiwa na Serikali, TRC ikiwa mojawapo.

Shabaha maalumu ya kuundwa TRL ilikuwa ni kubadili kuporomoka kulikokuwa kunaendelea katika usafirishaji wa mizigo na abiria, na kushuka kwa morali ya wafanyakazi kwa kutokuwa na uhakika wa hatima yao.

Hali kadhalika kuhuishwa utendaji wa reli ya kati ili kuiwezesha Tanzania kufaidika na nafasi yake ya kijiografia ikiwa ni nchi yenye kupakana na bahari ; kwa kupata mapato zaidi yanayotokana na mizigo inayoingizwa na kusafirishwa na nchi jirani ambazo hazipakani na bahari. Uendeshaji wa TRL ulikabidhiwa rasmi kwa RITES ya India Oktoba 1, 2007.

Uongozi wa RITES baada ya kuchukua uendeshaji wa TRL ulitengeneza mpango wa biashara wa miaka 10 (2007 – 2017), huu ni mpango waliouwasilisha wakati wa zabuni mnamo mwaka 2002. Mpango huo wa 2007 pamoja na mambo mengine ulikuwa uongeze tani milioni 0.42 za wakati huo wa Oktoba 2007 hadi tani milioni 3.14 za mizigo itakapofika mwaka 2007.

Hata hivyo kinyume na matarajio hayo mizigo iliyokuwa inasafirishwa iliendelea kushuka, hali hiyo iliyosababisha uongozi wa TRL chini ya RITEs upitie upya mpango huo wa biashara mwezi Juni 2009; na hivyo basi makadirio mapya yakawa kusafirisha tani milioni 2 za mizigo ifikapo 2017, ikilinganishwa na makadirio ya awali ya kusafirisha tani milioni 3.14.

Hata hivyo kama ilivyokuwa katika utekelezaji ule wa mpango wa awali, usafirishaji wa mizigo ukaendelea kushuka toka tani 577,581 mwaka 2007 hadi kufikia tani 267,008 mnamo mwaka 2011. Hali hii ya utendaji haikukubaliwa na Serikali ya Tanzania, ambayo iliamua kununua hisa 51% za kampuni ya RITEs. Makubaliano yalifikiwa na Serikali ikachukua uendeshaji kamili wa TRL Julai 2011.

Mnamo mwezi Januari 2013 Serikali iliteua Bodi ya Wakurugenzi ikiwaagiza kufufua TRL. Bodi hiyo ikaanza juhudi ya kuandaa mikakati wa kuifufua TRL na kupata Mpango mpya wa Biashara, ambao unafahamika kwamba ‘Mpango wa kuifufua TRL.

Mpango huu unakwenda sambamba na ‘Programu ya Matokeo Makubwa Sasa’ (BRN), ambayo pamoja na mambo mengine inapanga kuhuisha mpango wa usafirishaji wa kanda ya kati ikiwa ni moja ya vipaumbele sita vyenye lengo la kufanikisha visheni ya Kitaifa 2025 ambapo lengo lake kuu ni kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati.

Kwa mujibu wa mpango wa biashara wa kuifufua TRL dira na dhima ya TRL ni kama ifuatavyo:-

“DIRA”: Ni kuwa kampuni chaguo la usafiri ulio nafuu wenye ufanisi na usalama katika Afrika Mashariki.

“DHIMA”:Kutoa huduma ya Reli yenye ufanisi, gharama nafuu ya kutumainiwa yenye uhakika na usalama.

Aidha katika hotuba yake ya kufunga mwaka Disemba 31, 2013 Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete alisema kuwa huduma katika reli ya kati itaboreshwa kwa mwaka 2014.

Alisema shirika la reli TRL litapokea injini mpya 13, mabehewa ya mizigo 274 na breki 34. Aidha alisema kuwa ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa utaanza katika nusu ya pili ya mwaka 2014.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *