Mwaka 1964, Serikali iliyokuwa ikiongozwa na chama cha TANU iliamua kupiga marufuku mfumo wa vyama vingi na kuamua kuwa Tanzania itakuwa ni nchi ya chama kimoja.
Sababu za uamuzi huo zilitolewa kuwa ni pamoja na kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa; aidha vyama vingine vilikuwa ni dhaifu sana kulinganisha na TANU jambo ambalo lilikuwa linakiwezesha chama hicho kujinyakulia karibu viti vyote vya ubunge.
Moja ya faida kubwa za mfumo wa chama kimoja ni pamoja na Tanzania kuwa ni nchi yenye amani na kuweza kujenga umoja na mshikamano licha ya kuwa na makabila makubwa zaidi ya 100. Tanzania iliweza kuondoa tofauti za ukabila, udini au mahali mtu anapotoka.
Undugu na upendo uliimarika miongoni mwa Watanzania. Hili pia lilichangiwa sana na ‘siasa ya ujamaa na kujitegemea’, lugha ya Kiswahili pamoja na uongozi thabiti wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye hakufumbia macho dalili zozote za ukabili au udini.
Pamoja na faida hizo za mfumo wa chama kimoja, pia mapungufu kadhaa ya mfumo wa chama kimoja yaliweza kujitokeza. Mfumo wa chama kimoja uliwanyang’anya wananchi haki zao za uraia. Uliminya wigo wa demokrasia. Wananchi hawakuwa na uhuru kujiunga na chama wanachokitaka. Uhuru wa kuanzisha chama cha siasa, kujiunga na chama chochote kile, uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni uliminywa chini ya mfumo wa chama kimoja.
Kwa ujumla haki za binadamu na za uraia zilikiukwa. Mfumo haukutoa nafasi ya kutoa mawazo mbadala au kuikosoa serikali. Nafasi ya asasi za kiraia iliminywa na kuwa finyu sana. Vyama vya wafanyakazi na wakulima vililazimika kwa chini ya chama.
Mfumo wa chama kimoja ulivunja au uliondoa ubunifu wa watu binafsi na utamaduni wa ushindani. Ulijenga hofu na woga. Chama kilichopo madarakani kilibweteka na kuwa mbali sana na wananchi. Hiyo ni kutokana na kutokabiliwa na changamoto yoyote.
Mwalimu Nyerere alipokamilisha mradi wa kuimarisha chama katika matawi alihitimisha mradi huo kwa kuona kuwa chama kilikuwa mbali sana na wananchi na kilikuwa kimebweteka. Inasemekana, ni moja ya sababu zilizomfanya Mwalimu abadili msimamo wake na kuona kuwa chama tawala kilihitaji changamoto ili kisilale usingizi na ndipo alipotamka hadharani kuwa ‘si uhaini kujadili mfumo wa vyama vingi. Ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji’. Hapo alikuwa akitukumbusha mageuzi yaliyokuwa yakitokea kwingineko na kusema kuwa tunayo ya kujifunza.
Chama kilijaa wanachama wengi ambao waliingia kwasababu tu ya kukidhi maslahi yao binafsi. Demokrasia ndani ya chama ilizidi kupungua na hasa nafasi za viongozi zilikwenda kwa wale wale ambao walijulikana kama ‘mwenzetu, kijana wetu na ndugu yetu.’ Kwa ujumla chama kilibweteka. Ndio sababu ya Mwalimu Nyerere kusema kuwa mfumo wa vyama vingi hukifanya chama kilichopo madarakani kisibweteke.
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa katika moja ya mikutano ya kampeni mwaka 2015
Maana yake kitaendelea kufanya kazi kwa nguvu kuwatumika wananchi, kitakuwa na ubunifu ili kutatua kero za wananchi, kitahakikisha kuwa kinachagua viongozi bora na wa kupigiwa mfano, ili wasipatikane na kashfa ambazo zitawashushia heshima na kuwafanya washindwe katika chaguzi mbalimbali.
Kwa muktadha huo, Upinzani au chama kikuu cha upinzani ni jambo jema kwa kila Mtanzania na hasa mpenda maendeleo na anayeumizwa na umasikini.
Mwanzoni mwa miaka ya 1980, shinikizo kutoka katika mataifa makubwa kwa nchi za Afrika ziingie katika mfumo wa vyama vingi lilianza. Pia kulikuwa na vuguvugu kubwa ndani ya nchi la kudai mfumo wa vyama vingi. Harakati za kudai katiba mpya nazo zilishika kasi nchini.
Tanzania ilijibu hali hiyo kwa kuunda Tume ya Nyalali ambayo ilipewa jukumu la kukusanya maoni ya Watanzania kuhusiana na mfumo wa siasa ambao wanautaka. Mijadala ya Wanazuoni na wanaharakati ilipamba moto katika kujadili mfumo wa vyama vingi na madai ya kudai katiba yaliongezeka.
Mwaka 1992, kufuatia mapendekezo ya Tume ya Nyalali, tuliamua tena kurudi katika mfumo wa vyama vingi. Takwimu za Tume ya Nyalali zinasema kuwa asilimia 20 ya Watanzania walipendelea tuingie katika mfumo wa vyama vingi, na 80% walipendelea tubakia katika mfumo wa chama kimoja lakini walitaka yafanyike mabadiliko makubwa.
Hapa pia Mwalimu alitukumbusha kuwa hatuwezi kutumia sababu za mwaka 1965 kukataa mfumo wa vyama vingi mwaka 1990.
Tume ya Nyalali ilipendekeza kuwa tuingie katika mfumo wa vyama vingi licha ya wengi kutaka tubakie katika mfumo wa chama kimoja. Sababu zilizotolewa ni kuwa 20% ni idadi ya kutosha na muhimu hivyo isipuuzwe.
Hata hao 80% walitaka mabadiliko makubwa na mabadiliko hayo yasingeweza kutekelezwa nje ya mfumo wa vyama vingi. Muhimu sana ilionekana ni vyema kuwarejeshea wananchi haki zao za uraia na kisiasa. Ilionekana ni vyema kuruhusu sauti zenye mawazo tofauti, kuruhusu mgongano wa mawazo, tofauti za kisera, mikakati katika kuwatumika Watanzania. Demokrasia ya vyama vingi ilionekana kuwa ni uamuzi sahihi ili tuweze kujiletea maendeleo.
Leo hii tuna miaka 26 tukiwa ndani ya mfumo wa vyama vingi. Juhudi kubwa zimefanyika katika kujenga vyama mbadala na imara ambavyo vinaweza kuleta changamoto na kuiongoza nchi yetu. Demokrasia yetu changa ya mfumo wa vyama vingi hivi sasa, inapita katika kipindi tofauti, kipindi kigumu na chenye changamoto nyingi.
Zipo faida nyingi kuwa na chama kikuu cha upinzani madhubuti. Chama kikuu cha upinzani huisimamia serikali na kuikosoa pale ambapo inapokuwa haiwajibiki au inapofanya makosa. Hali hii huifanya serikali iliyopo madarakani kuwa makini sana katika kuwatumikia wananchi na pale makosa yanapofanyika huchukua hatua haraka kurekebisha makosa hayo na hata kuwawajibisha wale ambao wamesababisha makosa hayo.
Mifano ni mingi sana ambapo sote tumeweza kushuhudia hatua mbalimbali zikichukuliwa katika kukabiliana na vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya ofisi au uzembe.
Mfumo wa demokrasia ya vyama vingi huweza kutoa nafasi kwa chama kikuu cha upinzani kuleta mawazo mbadala, kuihoji serikali na kuisimamia ipasavyo. Serikali yoyote bora ni lazima ijibu hoja na maswali kutoka kwa wananchi. Chama mbadala huifanya kazi hii kwa niaba ya wananchi kwa kuihoji na kuibua masuala ya msingi na matatizo ili yaweze kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Chama mbadala huweza kuboresha sera na miswada na sheria kwa kushiriki katika mijadala kupitia katika kamati za bunge na bungeni kwa kuleta mawazo mbadala na ambayo chama kilichoko madarakani hakikuyaona. Hali hii huleta mijadala yenye afya.
Mathalani, tumeshuhudia Wabunge wa upinzani wakiihoji serikali na kuibua kashfa za rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi. Haya yote yaliweza kuletwa bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na hatimaye hatua kuchukuliwa.
Rais John Magufuli katika moja ya mikutano ya kampeni mwaka 2015
Wabunge kutoka vyama vya upinzani walitoa mchango mkubwa katika mijadala ya Richmond, Escrow, EPA, Mabilioni ya Uswiss, manunuzi ya rada na yale yasiyofuata sheria na kanuni. Pamoja na baadhi ya wabunge kutoka chama tawala kupaza sauti zao, lakini ni rahisi zaidi kwa wabunge wa upande mwingine kuibua kadhia mbalimbali na kuzisema kwa uhuru na bila woga.
Hali hii ni afya kwani huleta woga wa kutumia madaraka vibaya na ikiwa hivyo basi huwa ni manufaa kwa Watanzania wote bila kujali vyama vyao.
Pamoja na uzuri wa mfumo huu wa demokrasia ya vyama vingi, lakini pia ni mfumo ambao unaweza kuwa na hasara zake iwapo hautaendeshwa vizuri. Kama sababu zilizowahi kutolea huko nyuma kama tusipokuwa makini, mfumo huu unaweza kutugawa kwa misingi ya itikadi, dini, kabila na mahali mtu anapotoka.
Ni rahisi sana ndani ya mfumo huu, wajanja wachache kutafuta uhalali kwa kutumia turufu ya udini, ukabila au mahali mtu anapotoka. Hivyo, moja ya hatari za mfumo wa vyama vingi ni kuwagawa Wananchi. Ni muhimu tukumbuke tuna vyama tofauti lakini sisi bado ni Watanzania, Waafrika na sisi ni ndugu na nchi yetu ni Tanzania, hatuna mahali pengine pa kwenda. Hivyo Tanzania kwanza na vyama baadae. Tupingane kiistarabu lakini pia tupendane na tudumishe udugu wetu, mshikamano na amani.
Sambamba na hilo, demokrasia ya vyama vingi huweza kuleta chuki, visasi na uhasama baina ya wapenzi wa chama kimoja cha siasa dhidi ya kingine. Hali ambayo kwa sasa inazidi kuongezeka. Demokrasia ya vyama vingi huja na utamaduni wa uzushi, uongo na ulaghai.
Wanasiasa ili waweze kukubalika, hutumia mbinu ya kuchafuana, ulaghai, uzushi, kejeli, vitisho na kebehi. Hivi vyote havijengi kabisa na huondoa maelewano na kuzidisha chuki na mara nyingi huwachanganya wananchi.
Wanasiasa wetu wajitahidi kufanya siasa safi, wapunguze tofauti ya maneno yao na vitendo vyao, wajenge hoja na kujadili masuala ambayo yanawagusa wananchi kama vile huduma za jamii. Wawe ni wenye msimamo na wasimamie itikadi, sera na falsafa zao. Utamaduni wa kuhamahama unaipunguzia heshima fani hii ya siasa.
Kwa wale ambo wenye mtazamo HASI kuhusu vyama vya upinzani, ni vizuri wakabadili mtazamo wao na kuviangalia kwa mtazamo chanya na kuona ni namna gani wanaweza kuwa chachu ya kuvisaidia ili viweze kuwa vyama imara na viweze kutoa mchango unaotarajiwa.
Tujenge siasa za kistaarabu, tujenge hoja, tuseme kweli na tuwe wanyofu, tuzungumze na tupate muafaka, tujenge Tanzania yetu kwa pamoja. Kuua upinzani au kuwa na upinzani dhaifu ni MSIBA mkubwa kwa kila Mtanzania. Kujenga upinzani imara ni jukumu la kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na Taifa letu.
Hata hivyo, ni muhimu kwa kila Mtanzania, kujiuliza maswali yafuatayo: Kwa nini tuliamua kurejesha demokrasia ya vyama vingi? Je, tulijifunza nini ndani ya mfumo wa chama kimoja? Mfumo wa chama kimoja ulikuwa na mapungufu yapi na faida zipi? Na je, mfumo huu utaweza kukidhi mazingira ya sasa duniani? Ni zipi faida za mfumo wa demokrasia ya vyama vingi? Ndani ya miaka 26, ni yapi tumejifunza? Mambo yapi tuyadumishe na yapi tujirekebishe?
Makala hii imeandikwa na Selemani Rehani.