Na Phinias Bashaya, Bukoba
CHUO cha usafirishaji cha taifa(NIT)kinadaiwa kuchangia mgogoro unaofukuta baina ya vyuo vya ufundi mjini Bukoba vinavyowania kuwatoza madereva ada ili vitoe mafunzo ya kubadilisha leseni.
Mwisho wa uhai wa leseni za daraja la tatu ni Juni 30 mwaka huu (2011) na madereva wa magari ya abiria hawatapatiwa leseni mpya bila kupitia mafunzo ya wiki moja kwenye vyuo vilivyoidhinishwa.
Kutokana na utaratibu huo wiki mbili zilizopita madreva mkoani Kagera walikutana na viongozi wa zoezi hilo ngazi ya taifa kujulishwa taratibu za ada na kuwa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kimeidhinishwa na NIT kutoa mafunzo hayo.
Meneja wa TRA mkoa wa Kagera Leonard Shija alieleza taratibu za mfumo mpya wa leseni na mwakilishi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa Venesto Rwekamwa akisisitiza VETA ndicho chenye wataalamu waliofuzu kwa kazi hiyo.
Hata hivyo wakati madreva wakilalamikia ada ya shilingi 163,000/=. Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani mkoani hapa Winston Kabantega ambaye pia anamiliki moja ya chuo cha ufundi ametoa maelezo mengine yaliyowachanganya madereva.
Kwa mujibu wa Kabantega katika mkutano ulioandaliwa na chama cha madereva, alidai ataleta wataalamu kutoka NIT na tayari wametoa sharti la kuorodhesha idadi ya wale wanaotaka kupewa mafunzo na kuwapa matumaini ya kupunguziwa ada.
Akizungumzia mkanganyiko huo mwenyekiti wa chama cha madreva mkoani Kagera Victor Sherejei alisema chuo kimoja hakiwezi kutoa mafunzo hayo na kuwa watawashauri madereva kutafuta chuo chenye unafuu wa gharama.
Pia alithibitisha kuwa tayari madreva 300 wamejaza fomu kuhudhuria mafunzo hayo ambapo inadaiwa kuwepo kwa mvutano wa masirahi ya kugombea ada itakayotolewa na madereva na kuwa NIT iko katikati ya mgogoro huo.
Naye mkuu wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi (VETA) John Gassomi alisema tayari wana wataalamu kwa ajili ya kazi hiyo na kuwa wataweka utaratibu utakaowawezesha madereva kuhudhuria mafunzo bila usumbufu.
Pia Mwenyekiti wa kamati ya uhamasishaji wa mafunzo ngazi ya taifa ambaye pia ni katibu wa umoja wa madereva na makondakta (utingo) wa mabasi ya abiria Dar es Salaam (UWAMADAR) Shukuru Mlawi alisema chuo cha VETA ndicho chenye idhini ya kutoa mafunzo hayo.