MENEJA wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamiii (NSSF) mkoani Mwanza, Elizabeth Ngabo, anadaiwa kupuuza agizo lililotolewa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Habari za uhakika zimeeleza kwamba , Meneja huyo bado hajachukua hatua za kisheria dhidi ya uongozi wa kamapuni ya Kilumi Security Services Ltd, kama alivyogizwa kwanjia ya barua na Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mathayo F Maselle.
Inadawa kwamba Meneja huyo anashirikiana na baadhi ya viongozi wa Kilumi Security Services Ltd jijini hapa; hatua ambayo inachangia katika uvunjaji wa sheria za ajira.
“ Inavyonekana ni kwamba Meneja wa NSSF ametutosa; kwani tangu wakati huo hatujalipwa mafao yetu na wala Meneja huyo hajachukua hatua dhidi ya aliyekuwa mwajiri wetu, Kilumi Security Services,” alidai aliyekuwa mlinzi katika kampuni hiyo, Jeremiah Nyamsongeca.
Anadai kuwa baada ya kuachishwa kazi alibaini kuwa kampuni hiyo ilikuwa haiwasilishi makato ya fedha katika mfuko wa NSSF; kitendo alichosema ni kinyume cha sheria.
Alidai pia kuwa yeye pamoja na na wenzake hawana vitambulisho licha ya kwamba waliajiriwa kwenye kampuni hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Nyamsongeca ambaye Februari mwaka huu alilalamikia uongozi wa NSSF mkoani hapa kwa kushindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya aliyekuwa mwajiri wake, aidai kuwa bado anapigwa danadana.
“ Ninao ushahidi kwamba Meneja wa NSSF alishatumiwa barua yenye kumbukumbu namba EA112/205/01 iliyosainiwa na Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, akiagizwa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya Kilumi Security Services” alidai mlalamikaji huyo.
Alidai barua hiyo (nakala tunayo) ya tarehe 14/2/2012 ilisema kuwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imechoshwa na malalamiko yasiyokoma dhidi ya kampuni ya Kilumi Security Services.
Huku akikabidhi nakala ya barua hiyo kwa mwandishi wa habari hizi, Nyamsongeca alidai kuwa uongozi wa kampuni hiyo unatamba kwamba kamwe ofisi ya NSSF mkoa haiwezi kuwafikisha mahakamani wala kuwalazimisha kulipa deni.
“ Taarifa nilizonazo ni kwamba kampuni hiyo inadaiwa zaidi ya shilingi milioni kumi,” alidai.
Alipoulizwa, Meneja wa NSSF mkoa wa Mwanza, Ngabo, alikiri kupokea barua hiyo ingawa hakuwa tayari kutoa ufafanuzi kwa madai ya kutingwa na kazi nyingi ofisini kwake.
“ Ni kweli kuna malalamiko pamoja na barua kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwamba Kilumi Security Services ambaye ni mteja wetu inadaiwa makato ya fedha. Hata hivyo, bado ninaendelea kuwasiliana nao” alikiri Meneja huyo.
Alisema ofisi yake haijachukua hatua ya kufikisha kampuni hiyo mahakamani kutokana na kuepuka usumbufu pamoja na mlolongo wa kesi mahakamani.
“ Pamoja na barua hii, Mhe Mkuu wa Mkoa anataka kuona hatua kali zinachukuliwa haraka iwezekanavyo ili pamoja na kupunguza malalamiko yasiyokuwa ya lazima lakini pia kuwatendea wananchi hawa haki na hivyo kudumisha amani na utulivu katika Jamii,” inaagiza sehemu ya
barua iliyoandikwa na Katibu wa Mkuu wa Mkoa.
Alipoulizwa kwa njia ya simu, Meneja wa kampuni hiyo , Peter David, alikiri kuwepo kwa deni hilo huku akisema suala hilo linashughulikiwa na Meneja wa NSSF mkoa wa Mwanza.
” Ni kweli malalamiko hayo yalishafikishwa katika ofisi ya Mkuu wa mkoa; hata hivyo suala hilo linaendelea kushughulikiwa na Meneja wa NSSF Mkoa” alidai.
Alidai ofisi yake inaendelea na taratibu za malipo hayo na kwamba kudai na kudaiwa ni suala la kawaida katika biashara yoyote duniani.
Imeandaliwa na Juma Ng’oko, Mwanza