Kulingana na Benki ya Dunia (WB) katika ripoti yake ya Mapitio ya Uchumi ya mwaka 2017, inaitaja Tanzania kutumia asilimia 80 ya maji yake yote katika shughuli za kilimo.
Matumizi hayo ni makubwa ikilinganishwa na matumizi ya dunia ambayo yanafikia 70% katika kilimo. Dhana ya kutumia maji mengi kwenye kilimo inatokana na ukweli kuwa sekta hiyo imeajiri wananchi wengi na kuwa sehemu muhimu ya kuingiza kipato.
Chanzo kikubwa cha maji yanayotumika kwenye kilimo ni mvua za msimu ambazo zinanyesha katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na jografia na hali ya hewa ya eneo husika. Kuna maeneo yanapata kipindi kimoja cha mvua za msimu na mengine vipindi viwili.
Eneo la Pwani ya Kaskazini linalojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba linapata vipindi viwili vya mvua za msimu. Kipindi cha kwanza kimepita lakini wakati huu kipindi cha pili kimeacha mwezi Machi, 2018 na kinatarajia kuendelea hadi Mei mwaka huu.
Kulingana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mvua zimeanza kunyesha tangu wiki ya kwanza ya Machi na zinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi ya mikoa iliyotajwa isipokuwa katika maeneo machache.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi alisema kuwa mvua katika eneo la Pwani ya Kaskazini ya Tanzania linapata mvua za kawaida ambapo katika baadhi ya maeneo zitakuwa nyingi kulingana na mfumo wa mabadiliko ya hali ya hewa yatakayojitokeza katika kipindi hicho.
“Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza (zilianza) wiki ya kwanza ya mwezi machi, 2018. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam, mkoa wa Pwani, visiwa vya Unguja na Pemba, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na kusini mwa mkoa wa Tanga”, alisema.
Alibainisha kuwa katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Tanga, mvua zitakuwa chache kuliko ilivyotarajiwa. “Maeneo yaliyosalia yaliyo kaskazini mwa mkoa wa Tanga yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.”, alifafanua.
Ushauri kwa wakulima
Kutokana na kuimarika kwa mvua za msimu wakulima katika eneo la Pwani la Kaskazini wanashauriwa kufanya maandalizi ya kulima mazao yanayoendana na hali ya hewa ili kuhakikisha wanapata mazao yaliyokusudiwa.
“Wakulima katika maeneo hayo wanashauriwa kuendelea na maandalizi na kufanya shughuli za kawaida za kilimo”, alisema Dkt. Agnes na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na kuwepo kwa unyevunyevu wa kutosha kwenye udongo ambao ni muhimu kwa ukuaji wa mazao.
Hata hivyo, eneo la kaskazini mwa mkoa wa Tanga linatarajiwa kuwa na vipindi vya upungufu wa unyevunyevu katika udongo hivyo wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayostahimili mvua chache na kukomaa mapema ili kuepuka kupata hasara.
Sababu za kuimarika kwa mvua
Mvua zinazonyesha katika maeneo ya Pwani zinategemea zaidi hali ya joto na upepo wa bahari ambao huvuma kuelekea bara.
Dkt. Agnes Kijazi anaeleza kuwa, “ hali ya joto la bahari la wastani inatarajiwa katika eneo la magharibi mwa bahari ya Hindi. Hata hivyo, kusini magharibi mwa bahari ya Hindi kunatarajiwa kuwa na joto la juu ya wastani katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2018”.
Aidha, hali ya kuendelea kuwa na joto la chini ya wastani katika bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola) inatarajiwa kuongeza msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo hivyo kusababisha ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo nchini.
Hata hivyo, wakulima, wanashauriwa kutafuta na kupata ushauri zaidi kutoka kwa maafisa ugani waliopo katika maeneo yao.