Pembejeo za kilimo sasa kutolewa kwa wenye dhamana, maskini walie tu!

Jamii Africa

LICHA ya msimu wa masika kwa mwaka huu 2017 kukumbwa na hali ya ukame, lakini upatikanaji wa pembejeo za kilimo umekumbwa na changamoto kubwa inayoashiria uzalishaji duni wa mazao ya chakula na biashara.

Safari hii siyo changamoto ya ubadhirifu na ucheleweshaji wa pembejeo hizo, bali ni wakulima wenye dhamana tu ndio wanaoruhusiwa kupatiwa vocha za pembejeo.

Uchunguzi wa FikraPevu uliofanyika mkoani Dodoma umebaini kwamba, ingawa wakulima wengi mkoani humo siyo wanufaika wakubwa wa pembejeo hizo, lakini wale wanaostahili kupata safari hii wameshindwa baada ya kuwepo kwa sharti la dhamana ya kuwa na shamba lisilopungua ukubwa wa ekari moja.

Aidha, wakulima wengi ambao mara nyingi huhitaji pembejeo hizo, hususan mbegu na mbolea, na wale wanaojihusisha na kilimo cha mpunga, mahindi na vitunguu, wengi wao wakiwa katika maeneo ya mabonde ambayo yanahusisha kilimo cha umwagiliaji.

Zuberi Saidi Mlinji, Ofisa Ugani wa Kata ya Malolo, anasema kwamba, utaratibu wa ugawaji wa vocha za pembejeo umebadilika ambapo sasa si wote watakaonufaika kama ilivyokuwa zamani bali ni wale tu watakaokidhi masharti.

“Kwa mfano, katika Kijiji cha Malolo vocha zitakazokuja ni 100 tu na zitatolewa kwa wakulima ambao wanakidhi vigezo vya kuwa na shamba lisilopungua ekari moja,” anasema ofisa huyo.

Anasema serikali imefanya hivyo baada ya kugundua kwamba, baadhi ya wakulima waliokuwa wakipata vocha za pembejeo hawakuwa pia na uwezo wa kulipia hata nusu ya gharama na wengine hawakuwa kabisa na mashamba, hatua ambayo iliwafanya baadhi yao kuzigeuza mtaji kwa kuuza kwa wenye uwezo.

“Wengi walikuwa wakiziuza tena vocha hizo kwa sababu ama hawakumudu gharama, hawakuwa na mashamba na wengine waliamua tu kutotumia na kugeukia kwenye kilimo cha asili walichokizowea kwa kutumia mbegu za asili na hawakutumia mbolea kabisa,” anabainisha ofisa ugani huyo wakati akizungumza na FikraPevu kijijini Malolo.

Anasema hivi sasa wameamua kutoa pembejeo hizo kwa wakulima baada ya kujiridhisha kwamba wana uhitaji na wanayo mashamba yanayokidhi vigezo.

Aidha, anasema kwamba, kupungua kwa idadi ya vocha hizo za pembejeo ni jambo la kawaida, kwani mpango huo wa serikali ulilenga kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora pamoja na mbolea ili kukuza uzalishaji na kuongeza kipato.

Kupitia mpango huo wa ruzuku ya pembejeo ulioanza mwaka 2008, serikali ililenga kuwapunguzia mzigo wakulima kwa kubeba nusu ya gharama za pembejeo hizo wakati kiasi kingine kilipaswa kulipwa na wakulima wenyewe.

Kwa mujibu wa maelezo ya maofisa kutoka wizara ya kilimo, idadi ya vocha hizo ilikuwa ipungue kila mwaka kwa kuamini kwamba, walau katika kipindi cha miaka mitatu wakulima hao wangekuwa na uwezo wa kujinunulia wenyewe pembejeo.

“Watu wanakosea, ni kwamba, mpango huu ulipanga kuwawezesha wakulima wote walau kwa miaka mitatu, na baada ya hapo vocha zisingeweza kuja kwa idadi sawa, bali zingeendelea kupungua kwa kuwa serikali iliamini katika kipindi hicho tayari wakulima wangeweza kumudu kununua pembejeo wenyewe, jambo ambalo linaonekana kama limeshindikana,” anasema ofisa mmoja wa wizara hiyo anayeshughulikia masuala ya pembejeo, ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.

Lakini kupungua kwa vocha hizo za ruzuku, na kwa utaratibu wa sasa wa kuhakikisha wakulima wanakuwa na dhamana, kutaleta changamoto kubwa ya mpango wa serikali kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Licha ya kupungua kwa idadi hiyo, lakini mara kadhaa pembejeo zimekuwa zikichelewa kuwafikia wananchi na mpango huo umekumbwa na ufisadi mkubwa kwa watendaji pamoja na mawakala, ambapo inaelezwa kwamba, baadhi yao walishtakiwa katika mahakama za kisheria.

Kila mwaka, bajeti kuhusu pembejeo za kilimo imekuwa ikipungua na wakulima, ambao wanaamini ni haki yao kupata vocha hizo bila kujali idadi yao, wanaona kwamba serikali imewatelekeza.

FikraPevu inafahamu kwamba, katika bajeti ya kilimo ya 2015/2016, makadirio ya mahitaji ya pembejeo yalikuwa tani 485,000 za mbolea, tani 60,000 za mbegu bora, miche ya chai 1,700,000, miche ya kahawa 5,000,000, viuatilifu vya korosho tani 25,000 na viuatilifu vya pamba ekapaki 1,500,000.

Lakini hadi kufikia mwezi Aprili 2016, pembejeo ambazo zilikuwa zimepatikana zilikuwa tani 302,450 za mbolea sawa na asilimia 62.3 ya mahitaji, mbegu bora tani 36,482 sawa na asilimia 61 ya mahitaji, miche bora ya chai 1,600,000 na kahawa miche 2,106,510 na viuatilifu tani 8,011 kwa zao la korosho, na ekapaki 1,244,075 kwa zao la pamba.

Aidha, kwa mwaka 2015/2016 Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha ambapo kaya za wakulima 999,926 zilinufaika kwa kutumia tani 99,993 za mbolea, tani 10,270.86 za mbegu bora za mahindi na mpunga vyote vikiwa na thamani ya Sh. 78 bilioni.

Idadi hiyo ilipungua kwa mwaka 2016/17, serikali ilisema ingewezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji wa tani 400,000 za mbolea, tani 40,000 za mbegu bora, miche bora ya kahawa na chai pamoja na kuwezesha upatikanaji wa viuatilifu vya zao la korosho, pamba na mazao mengine.

Licha ya sekta ya kilimo kuchangia asilimia 29 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2015, lakini ukuaji wake ulipungua ulipungua kwa asilimia 2.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.4 katika mwaka 2014 kwa shughuli za kiuchumi za kilimo zinazojumuisha mazao, ufugaji, uvuvi na misitu.

Wakati ambapo mahitaji ya pembejeo yanaongezeka kila mwaka kutokana na wananchi kuhamasika kujishughulisha na kilimo, serikali imeshindwa kuongeza nguvu katika utoaji wa vocha za ruzuku hasa kwa kuzingatia kipato halisi ya mwananchi wa kawaida, hususan mkulima, ambaye hana uhakika na soko la mazao yake huku hali ya mabadiliko ya tabia nchi nayo ikimuathiri kutokana na uhaba wa mvua.

Itakumbukwa kwamba, katika mwaka wa fedha 2008/2009, makadirio ya mahitaji ya mbolea yalikuwa tani 385,000, lakini hadi mwezi Mei 2009, jumla ya tani 237,894 sawa na asilimia 61.8 ya mbolea ikijumuisha mbolea za ruzuku zilipatikana.

Katika kipindi hicho, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ilitoa ruzuku ya mbolea tani 141,050 ikilinganishwa na lengo lilowekwa la tani 130,000 ambapo jumla ya vocha 1,499,000 za mbolea na 718,000 za mbegu bora zenye thamani ya Shs. 69 bilioni 69 zilitumika.

FikraPevu inatambua kwamba, kiwango hicho cha usambazaji wa mbolea ya ruzuku kilivuka lengo kutokana na Wizara kuongezewa fedha zilizookolewa kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (EPA) Shs. 40 bilioni, ambapo jumla ya wakulima 737,000 katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, na Kigoma na wilaya za Sikonge mkoa wa Tabora na Tarime mkoa wa Mara walinufaika na mbolea ya ruzuku.

Katika mwaka huo wa 2008/2009, uzalishaji wa mazao ya chakula katika mikoa 6 ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Morogoro, na Kigoma uliongezeka kutoka tani 4,692,411 katika mwaka 2007/2008 hadi kufikia tani 5,279,278, hasa baada ya wakulima kupata ruzuku ya pmebejeo za kutosha.

Licha ya kuwepo na mafanikio katika ruzuku za pembejeo, lakini changamoto mbalimbali zimejitokeza tangu kuanza kwa utaratibu huo ikiwemo vocha kuchelewa kuwafikia wakulima kwa wakati, bei ya mbolea kuendelea kuwa juu kiasi kwamba wakulima wanashindwa kumudu gharama za uchangiaji, kutoeleweka vema kwa utaratibu wa vocha kwa wadau wengi; na usimamizi duni katika ngazi mbalimbali za utekelezaji, hususan ngazi ya wilaya na kijiji.

Wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2008/2009, aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, alilieleza Bunge kwamba, wizara yake ingepeleka vocha mapema kulingana na msimu wa kilimo wa eneo husika na kuendelea kutoa elimu zaidi ya utaratibu wa matumizi ya vocha za pembejeo za ruzuku za kilimo kwa wadau mbalimbali.

“Tutapeleka vijana 1,998 wa Cheti na Diploma kutoka Vyuo mbalimbali vya Kilimo watakaokuwa katika mafunzo kwa vitendo katika wilaya zitakazopewa ruzuku ya pembejeo kuanzia Septemba 2009 hadi Aprili, 2010. Hii itaboresha usimamizi na kutoa maelekezo ya kitaalamu kwa wakulima,” alisema.

Aidha, alisema kwamba, kuanzia msimu wa 2009/2010 mkulima alitakiwa kuchangia malipo ya tofauti ya bei ya pembejeo kabla hajapewa vocha ili kuzuia wakulima kutumia vocha kinyume na makusudio.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, katika mwaka 2009/2010, serikali ilitoa ruzuku ya tani 150,000 za mbolea ambayo iliwanufaisha wakulima milioni 1.5 ikilinganishwa na wakulima 737,000 msimu wa 2008/2009.

FikraPevu inafahamu kwamba, ongezeko hilo lilitokana na kuongezwa kwa bajeti ya ruzuku ya pembejeo baada ya kupata fedha kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Usalama wa Chakula (Accelerated Food Security Project).

Kupitia mpango huo, mikoa 20 ilinufaika na ruzuku ya mbolea ambayo ni Iringa, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Arusha, Morogoro, Kilimanjaro, Kigoma, Manyara,Tabora, Mara, Shinyanga, Kagera, Mwanza, Mtwara, Lindi, Tanga, Dodoma, Pwani na Singida.

Wakati wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2010/2011, Waziri Wassira alilieleza Bunge kwamba, wizara yake ilikuwa imetoa tani 201,050 za mbolea ya ruzuku ambayo iliwanufaisha wakulima 2,011,000, lakini pia ilitoa ruzuku ya tani 20,357.86 za mbegu bora za mahindi na mpunga na tani ikilinganishwa na tani 15,150 zilizotolewa mwaka 2009/2010.

Vilevile, Wizara ilitoa tani 15,375 za mbegu ya pamba kwa utaratibu wa vocha na ruzuku ya mbegu bora za mtama tani 356.25.

Bajeti ndogo ya kilimo inaonekana kushindwa kukidhi mahitaji ya ruzuku ya pembejeo ambayo yanadaiwa kuwa makubwa kuliko uwezo wa Serikali.

Kwa mfano, katika mwaka 2012/2013, mahitaji ya mbolea yalikuwa tani 452,202, mbegu tani 60,000 na madawa tani 328,586, lakini hadi kufikia Machi 2013, tani 240,350 za mbolea na tani  30,443.0 za mbegu bora zilifikishwa kwa wakulima.

Ni katika mwaka huo ambapo idadi ya wanufaika wa ruzuku ilianza kupungua ikilinganishwa na miaka iliyotangulia.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, serikali ilitoa ruzuku ya mbolea tani 126,118 ambapo wakulima 940,783 walinufaika.

Jumla ya tani 10,741 za mbegu bora zikiwemo tani 8,278 za mahindi; tani 1,694 za mpunga; tani 402 za mtama na tani 366 za alizeti zilisambazwa kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku.

Ni wazi kwamba, kupungua kwa pembejeo hizo kutaendelea kuathiri uzalishaji wa mazao ya kilimo, ambayo ndiyo malighafi kuu ya viwanda, hivyo kukwamisha azma ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *