TAHADHARI: Mvua mikoa ya Pwani,  Wakulima washauriwa kulima mazao yanayokomaa kwa muda mfupi

Jamii Africa

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) nchini imewashauri wananchi wa mikoa ya kanda ya Pwani kuchukua tahadhari stahiki ya kutokana na  vipindi vya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha katika maeneo yao kwa.

Ukanda huo wa Pwani ambao utapata mvua kubwa ni mikoa ya Tanga, Dar es salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Pemba na Unguja. Mvua hiyo inatarajiwa kusambaa katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Lindi kuelekea siku ya Ijumaa ya tarehe 3 Novemba 2017.

Wananchi wa mikoa iliyotajwa wanashauriwa kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA kwasababu mvua inatarajiwa kuwa kubwa inayozidi milimita 50 kwa kiwango cha asilimia 80 kuanzia usiku wa jana Oktoba 31.

Hali hii inatokana na kuwepo na kuimarika kwa ukanda wa mvua (Inter Tropical Convergency Zone –ITCZ) katika maeneo hayo. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo kila itakapobidi.

Mvua hiyo kubwa ilinyesha wiki iliyopita katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na kuleta maafa ikiwemo uharibifu wa makazi ya watu, mazao, miundombinu ya barabara na madaraja. Hali hiyo ilisababisha adha ya usafiri kwa wananchi wanaoingia na kutoka katika mikoa hiyo.

Mvua hiyo ni sehemu ya mvua za vuli ambazo zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini. Izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na chini ya wastani.

Ukanda wa Pwani  ni miongoni mwa maeneo mengine nchini ambayo yanapata mvua mara mbili kwa mwaka ambapo utabiri wake ulitolewa Septemba mwaka huu. Mvua hizo ni sehemu ya  hujulikana kama mvua za vuli ambazo zilianza mwezi Oktoba na zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Desemba mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na TMA mwezi Septemba 2017, inaeleza kuwa  maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka  ni Ukanda wa Ziwa Viktoria wenye mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga, ambapo mvua zilianza kunyesha  mapema, kati ya wiki ya pili na tatu ya mwezi Septemba, 2017 katika maeneo ya mkoa wa Kagera  na kusambaa katika mikoa ya Geita, Mwanza, Mara, Simiyu na Shinyanga.

“Mvua za msimu wa Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2017 katika maeneo mengi ya Ziwa Viktoria, isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Mwanza ambapo mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya mwezi Disemba, 2017”, inaeleza ripoti ya TMA.

Nyanda za juu Kaskazini Mashariki yenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.  Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2017 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Manyara na Arusha.

Hata hivyo, maeneo mengi ya mkoa wa Kilimanjaro yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2017.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro). Mvua zilianza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2017. Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi   Mvua katika maeneo tajwa zinatarajia kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2017.

Ushauri kwa Wakulima na Wafugaji

Wakulima  wanaopata mvua za vuli ambazo zilianza Oktoba na kuendelea hadi Disemba 2017 hasa katika mikoa ya Manyara, Arusha, Morogoro, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Simiyu wanashauriwa kupanda mazao yanayokomaa muda mfupi kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa Kilimo waliopo katika maeneo yao.

“Hali ya unyevunyevu kwa ajili ya mazao na malisho ya mifugo na Wanyama pori inatarajiwa kuwa ya kuridhisha hususani katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba yao mapema na kupanda mazao yanayokomaa katika muda mfupi kwa kufuata ushauri wa wataalam wa kilimo”, ripoti hiyo inaeleza .

Kwa wakulima wa mikoa ya Kagera, Dar es salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro,  Visiwa vya Pemba na Unguja ambayo yanayopata mvua za wastani hadi chini ya wastani  wanashauriwa kupanda mazao yanayotumia muda mfupi kukomaa na yanayostahimili mvua chache.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa maeneo hayo yanatarajiwa kuwa na upungufu wa unyevunyevu katika ardhi kutokana na mvua za chini ya wastani.

Ili kuhakikisha wafugaji wanapata malisho ya kutosha kwa ajili ya mifugo yao wametakiwa kutumia fursa hiyo ya mvua kuvuna maji na kuhifadhi malisho ili kukidhi mahitaji katika kipindi hiki hasa katika maeneo ya Kagera, Dar es salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Visiwa vya Pemba na Unguja .

“Uzalishaji wa samaki katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani unatarajiwa kuongezeka, wakati katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani uzalishaji unatarajiwa kupungua”, inafafanua ripoti hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *