Pinda ashiriki maadhimisho ya miaka ya 40 ya Hospitali ya Bugando

Jamii Africa

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, ameeleza kushtushwa na ongezeko kubwa la ugonjwa wa Saratani kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, na kusema ni lazima Serikali iongeze nguvu katika kupambana na tatizo hilo, yakiwemo magonjwa ya moyo na figo.

Amesema, ugonjwa wa Saratani umeonekana kama janga linalolinyemelea taifa na ustawi wa wananchi wake, hivyo upo ulazima wa Serikali kupambana na matatizo kama hayo kwa kuongeza maradufu bajeti ya Wizara ya Afya kutoka asilimia 9 ya sasa kwa bajeti nzima ya Serikali.

Waziri Mkuu Pinda ameyasema hayo leo hii Jijini Mwanza, wakati alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 40 ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), ya jijini hapa, sherehe ambayo ilikwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

“Kwanza nawapongezeni sana hospitali ya Bugando kwa kutimiza leo miaka 40 tangu muanze kutoa huduma za matibabu. Lakini lipo tatizo kubwa la ugonjwa wa saratani kwa wananchi wetu wa Kanda ya Ziwa!. Siyo siri ugonjwa huu ni tatizo kubwa sana kwa Taifa letu.

“Kwa kutambua hili, Serikali inafanya juu chini kuhakikisha ugonjwa huu unadhibitiwa, yakiwemo magonjwa ya moyo, figo na mishipa ya fahamu. Na tutaongeza zaidi bajeti ya Wizara ya Afya kutoka asilimia 9 ya sasa ya bajeti yote ya Serikali”, alisema Waziri Mkuu ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya miaka 40 ya hospitali ya Bugando.

 

Pinda akiaga wananchi baada ya maadhimisho ya Miaka 40 ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando

Akitolea mfano wa ukubwa wa tatizo hilo la ugonjwa wa saratani, Pinda ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Katavi Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa alisema, asilimia 70 ya wagonjwa wote wanaotibiwa katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam ni wagonjwa saratani.

Akikazia hilo Waziri Mkuu alisema: “Nashukuru hospitali ya Bugando kwa kuanzisha huduma ya kutibu ugonjwa huu wa saratani. Lakini Serikali inataka huduma hii ianze kutolewa hospitali ya KCMC na ile ya Mbeya, ili kuwasaidia wananchi wetu”.

Aliupongeza pia uongozi wa hospitali ya Bugando chini ya Mkurugenzi wake, Dk. Charles Majinge kwa kuanzisha huduma nyingi za matiabu, ukiwemo upasuaji mkubwa na mdogo wa ugonjwa ya moyo, ubongo, mishipa ya fahamu, saratani pamoja na magonjwa mengine.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Bungando, Dk. Charles Majinge alimweleza Waziri Mkuu kwamba, hadi sasa jumla ya wagonjwa 120 wamefanyiwa huduma ya upasuaji mkubwa wa ugonjwa wa moyo hospitalini hapo.

“Tunapoadhimisha miaka 40 ya Bugando na miaka 50 ya Uhuru, hospitali yetu ya Bugando tumeona umuhimu wa kuwepo kwa huduma ya upasuaji wa ubongo, mishipa ya fahamu na ule upasuaji wa mifupa!.

“Huduma hizi tumezianzisha na wananchi wanapata huduma kwa kiwango cha juu sana, maana BMC inao madaktari bingwa 47 hadi kufikia 2011. BMC tumejenga pia maabara ya kisasa ambayo inafanyakazi. Na tupo kwenye mchakato wa usajili wa ubora wa Kimataifa, ili wazungu nao wawe wanakuja hapa kupima vitu vyao”, alisema Dk. Majinge.

 

(Picha na Habari na Sitta Tumma)

1 Comment
  • swala ni kwamba magonjwa na wagonjwa hayatakaa ya ishe tz zaidi ya kuongezeka,yote ni fikra zetu zipoutumwani”86%ya watz wanaumaskini waakili hasa wasomi yote sababu mtaala waelimu yetu ni mchafu na mbovu’ilitakiwa kila mtu awe daktari wa afya yake kupitia elimu anayo isoma iwe na maelezo jinsi ya kula milo ambayo ni tiba kwa magonjwa mf:DKT Ndodi anavyo fundisha ni vitu vilitakiwa kuwa ktk elimu ya msingi hadi chuo”ili wasomi wawe watu wakujivinia vyakula asilia visivyo na kemikali”siyo leo mtu anaye enda supamaketi kununu vyakulwa vya makopo na vyenye muda wa kueksipaya/vyenye makemiko anaonekana kaendelea au anahela huo ndiyo umaskini wa fikra’
    mwisho watz watakufa sana tu na wafe tu kwani ni wajinga wengi wao hasa wasomi kwani eti mtu anatafuta unenne au kitambi aonekane anapeasa alafu akija pata makisukari na mapresha analalamika’
    Htari ni kuwa 32%ya watz wanaoishi kwa tsh400kwa siku lini watapata pesa yakuwa na mazoea ya kwenda kuangalia afya yao?serikali ya KIWEWE haina maono”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *