Mwana wa Malkia wa Uingereza – Prince Charles of Wales – anatarajiwa kutembelea Tanzania kuanzia Jumapili akitokea Afrika ya Kusini ambako ameanza ziara ya siku nane katika bara la Afrika. Prince Charles ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa Uingereza ni mtoto wa kwanza wa Malkia Elizabeth wa Pili.
Katika ziara yake hiyo Prince Charles ameambatana na mkewe Duchess of Cornwell Camilla Parker. Ziara ya Tanzania itaanza tarehe 6 hadi tarehe 9 na ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika. Tanganyika (eneo la Tanzania Bara) ilipata uhuru wake kutoka Uingereza iliyokuwa inaitawala kwa agizo la Umoja wa Mataifa ambapo Uingereza ilitakiwa iiandae Tanganyika kuwa huru.
Mara ya mwisho kwa Prince Charles kutembelea Tanzania katika ziara rasmi ilikuwa ni 1984 na Bi. Parker hajawahi kutembelea Tanzania. Prince Charles ndiye baba yao Prince William na Prince Harry na mke wake wa kwanza Princess Diana (mama yao William na Harry) alikufa katika ajali ya gari mwaka 1997.