Rufiji: Vichanga hupimwa uzito kwa kukadiria tu!

Stella Mwaikusa

“Tangu nilipofika hapa ni mwaka mmoja sasa, niliukuta mzani huu wa kupimia vichanga ukiwa umeharibika hivyo ninachofanya ni kukadiria uzito wa mtoto anayezaliwa au kutompima kabisa” anaeleza Dokta Dollo Victor.

Dokta Dollo ambaye anafanya kazi katika zahanati ya Ndundunyikanza iliyopo kata ya Kipugira wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, anasema tangu alipofika katika kituo hicho mwaka 2011 amekuwa akikadiria  uzito wa watoto wachanga baada ya kuzaliwa  kutokana na kukosekana kwa mzani wa kupimia.

ndundunyikanza

PICHA: Zahanati ya Ndundunyikanza

Dollo anasema hali hiyo imekuwa ngumu kwake kama mtaalam kwani kujua uzito wa mtoto anapozaliwa kuna maana kubwa kwa afya ya mama na mtoto.

Dollo anasema mtoto anapozaliwa na kupimwa uzito inamsaidia daktari kujua mahitaji ya mtoto husika, anatoa mfano kwamba ikiwa mtoto mchanga atapimwa na kukutwa ana uzito wa chini ya kg mbili na nusu,  basi itaeleweka wazi kwamba mtoto ana matatizo ya kiafya mfano ugonjwa wa utapiamlo.

Anafafanua kwamba mtoto anapozaliwa anaweza kuwa na uzito wa kawaida ambao ni kuanzia kg mbili na nusu hadi kg tatu na nusu, na akiwa na uzito chini ya kg hizo basi anakuwa amezaliwa chini ya uzito wa kawaida pia akizaliwa na kg zaidi ya tatu na nusu anakuwa ana uzito uliozidi.

“Kwa kawaida mama aliyebeba mimba kwa miezi tisa anatakiwa kuwa na mtoto kuanzia kg mbili  na gram 500 mpaka kg tatu na nusu lakini ikiwa chini ya hapo basi daktari anapata mashaka juu ya afya ya mtoto au mama” anaeleza

Baada ya kumpima mtoto mchanga na kugundua kwamba ana uzito mdogo basi hupimwa na kujua ana matatizo gani mengine, kwani  uzito mdogo ni viashiria  kwamba huenda mama ana matatizo ya kiafya au mtoto mwenyewe.

Anasema inapotokea mtoto amezaliwa chini ya uzito wa kawaida daktari analazimika kumpima mama na mtoto kujua kama mama ana kinga ndogo au mtoto amezaliwa na matatizo ya kiafya.

Anasema baada ya kugundua tatizo kama liko kwa mama au kwa mtoto ndipo wanaanzisha matibabu na kutoa ushauri wa vyakula kwa mama ili kuimarisha afya yake na mtoto.

Dk Dollo anasema wakati mwingine mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na uzito wa zaidi ya kg tatu na nusu, na inapotokea hivyo daktari hulazimika kumpima mtoto na mama kwani hali hii pia inaashiria kwamba huenda mama ana matatizo ya kiafya japo si mara zote.

“Mtoto anapozaliwa na uzito mkubwa kuliko kawaida wakati mwingine inatokana na matatizo ya kiafya ya mama ikiwemo ugonjwa wa kisukari.” Anafafanua

Anasema kujua hayo yote ni lazima kuwepo na mzani wa kupimia watoto wachanga ambao ndio chanzo cha kujihakikishia usalama wa afya ya mama na mtoto.

mzani

PICHA: Mzani wa kupimia vichanga ambao umeharibika na hautumiki kwa sasa

Kutokana na kukosekana kwa mzani huo katika zahanati ya Ndundunyikanza inakuwa vigumu kujua hali ya kiafya ya mama na mtoto.

Tatizo la kukosekana kwa mzani linaikumba pia zahanati ya Mtanza ambayo inapatikana  katika kata hiyohiyo ya Kipugira,  hakuna mzani wa kupimia watoto wachanga baada ya kuzaliwa hivyo mzani wa kupimia watu wazima ndio hutumika kumpimia mtoto mchanga.

Muuguzi msaidizi wa zahanati hiyo Fatma Mpakwaku anasema mzani wa kupimia vichanga uliharibika miezi sita iliyopita hivyo amekuwa akitumia mzani  wa kupimia watu wazima ili kupata uzito wa mtoto aliyezaliwa.

Kinachofanyika ni mama au ndugu yeyote wa mama aliyejifungua kumbeba mtoto aliyezaliwa na kupima, baadaye mama au ndugu huyo hupimwa akiwa peke yake na baadae kuangalia kilo ngapi ziliongezeka alipokuwa amembeba mtoto.

Mpakwaku anasema kukosekana kwa mzani wa kupimia watoto wachanga baada ya kuzaliwa  kunampa kazi ya ziada kwani kazi iliyotakiwa kufanyika kwa muda wa dakika mbili anaifanya kwa robo saa.

Anasema mzani wa kupimia vichanga ni mhimu kwani pamoja na kutumia njia ya mtoto kubebwa na mtu mzima na kupimwa hapati uzito sahihi ambao ungepatikana kwenye mzani uliotengenezwa maalum kwa kazi hiyo.

Mzani huo wa kupimia vichanga (Scale infant clinic metric 15.5 kg*5g) huuzwa kwa sh 220,000 kwa bei ya  bohari ya dawa ya Taifa (MSD) ya mwaka 2010/2011 hii ni kwa mjibu wa Dk Victor Dollo.  

Tatizo lingine linaloikumba  zahanati ya Ndundunyikanza  ni kukosa umeme  tangu mwaka 2008 hali inayowalazimu akina mama wajawazito wa Ndundunyikanza  kubeba mafuta ya taa wanapokwenda kujifungua.

Dk Dollo Victor anasema hutumia chemli wakati wa shughuli nzima ya kumhudumia mama wakati wa kujifungua.

Anasema si akina mama wote wanaokuja na mafuta ya taa kutokana na haraka za kuwahi zahanati pale mama anapojisikia uchungu lakini mara nyingine ni kukosekana kwa bidhaa hiyo katika maeneo wanayotoka.

“Nina tochi yangu ninayotumia pale chemli inapokuwa haina mafuta, kama unavyojua huwezi kufanya kazi ile bila mwanga”anaeleza.

Dr-Dollo-Victor

PICHA: Dk Dollo Victor akionyesha taa ya chemli inayotumika kumulika wakati mama anapojifungua

Dk Dollo ambaye ni mhudumu pekee katika zahanati hiyo anasema analazimika kumuomba mtu yeyote atakayekuwepo hapo zahanati ili amsaidie kumulika, hali inayomfanya mtu mwingine kushuhudia zoezi zima la kuzalisha wakati yeye si mtaalam wala hakupaswa kuwa mahali hapo.

Mkuu wa wilaya  ya Rufiji Nurdin Hassan Babu anakiri  kukosekana kwa umeme katika baadhi ya zahanati ikiwemo zahanati ya Ndundunyikanza.

Babu anasema hawajaweza kufikisha umeme wa jua katika kila zahanati, anasema ni suala wanalolifanyia kazi kuhakikisha kila zahanati inapata umeme.

Mbunge wa Jimbo la Rufiji ambaye pia ni Naibu waziri wa afya na ustawi wa jamii, Dk Seif Rashid anakiri kuwepo kwa kile alichokiita “changamoto nyingi kwa akinamama wajawazito katika jimbo lake.”

Dk Seif anasisitiza kwamba ni wajibu wa wanavijiji kufahamu thamani ya vifaa vilivyopo, anasema katika zahanati ya Ndundunyikanza kulikuwa na umeme wa jua lakini mashine  ikaibiwa kwa sababu hapakuwa na ulinzi wa kutosha.

Wakati wauguzi na madaktari wakikosa vifaa mhimu katika zahanati, dira ya sera ya afya ya mwaka 2007, ni kuwa na jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo binafsi na ya nchi.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *