Ruvuma: Sasa hakuna shule yenye mwalimu mmoja wilayani Nyasa

Jamii Africa

LICHA ya kuwepo kwa uhaba wa walimu nchini Tanzania, lakini kwa sasa hakuna shule yenye mwalimu mmoja katika Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

FikraPevu imeelezwa kwamba, hali hiyo imefuatia agizo la Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Isabela Chilumba, alilolitoa Januari 30, 2017 wakati alipotembelea Shule ya Msingi Matarawe katika Kijiji cha Marungu, ambayo ilikuwa na mwalimu mmoja tu.

Mwandishi wa FikraPevu, Daniel Mbega (kushoto) akihojiana na Gaudence Msuha, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Matarawe wilayani Nyasa hivi karibuni.

“Mkuu wa Wilaya aliagiza kwamba, pamoja na serikali kutotoa ajjira mpya za walimu, lakini hataki kusikia kwamba kuna shule yenye mwalimu mmoja, hivyo akamwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anatafuta walimu kutoka katika shule zenye walimu wengi na kuwapaleka katika zile ambazo zilikuwa na uhaba mkubwa wa walimu wakati wakiendelea kusubiria ajira mpya,” kilisema chanzo kimoja kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.

Aidha, agizo la Mkuu wa Wilaya lilifutia ripoti ya FikraPevu, ambayo Alhamisi, Januari 26, 2017, iliripoti kwamba Shule ya Msingi Matarawe katika Kijiji cha Marungu, Tarafa ya Mpepo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ilikuwa imefungwa kwa wiki mbili zaidi tangu kufunguliwa kutokana na mwalimu pekee aliyekuwepo, Gaudence Msuha (48), kuwa mafunzoni mjini Songea.

Kati ya Januari 10 hadi 18, 2017, Mwalimu Msuha alikuwa akihudhuria mafunzo ya siku nane mjini Songea ya kujengewa uwezo masomo ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) yaliyotolewa kwa walimu wote wa awali kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma.

Mwalimu Charioni Mpombo, ambaye amehamishiwa katika Shule ya Msingi Matarawe kuinusuru shule hiyo isifungwe.

Taarifa zimeeleza kwamba, siku hiyo hiyo, Mkuu wa Wilaya aliitisha kikao na watendaji wa halmashauri akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Maofisa Elimu wa Msingi na Sekondari pamoja na watendaji wengine, na kuagiza mwalimu mwingine apelekwe shuleni hapo mara moja.

FikraPevu ilitembelea Shule ya Matarawe, ambapo ilielezwa kwamba, mwalimu mwingine, Charioni Mpombo kutoka Shule ya Msingi Tingi, aliwasili shuleni hapo siku moja tu baada ya taarifa ya gazeti hilo tando.

“Nililetewa mwalimu mmoja wa kiume Januari 27, 2017. Ingawa upungufu wa walimu bado upo, lakini ni afadhali kuliko kipindi kile nilipokuwa peke yangu,” alisema kwa furaha Mwalimu Msuha ambaye alikuwa akifundisha vipindi takriban kumi kwa siku.

Mwalimu Mpombo aliiambia FikraPevu kwamba, alipokea simu kutoka kwa Ofisa Elimu majira ya jioni na kupata hofu kubwa baada ya kuambiwa ni lazima waonane hapo kijijini Tingi.

“Nilipata hofu, si unajua mwendo wa sasa wa ‘kutumbuliwa’? sasa nikajiuliza, nimefanya nini tena jamani? Lakini Ofisa Elimu alipokuja akanieleza kwamba ananihamisha kituo changu cha kazi… akanitaka nikaripoti haraka na ndipo nirudi kujipanga. Sikuona shida yoyote kuja hapa,” aliiambia FikraPevu.

Katika taarifa yake ya awali, FikraPevu ilieleza kwamba, Mwalimu Msuha alikuwa anafundisha peke yake wanafunzi 195 ambao wako darasa la awali, la kwanza na la pili na kwamba kila anapopata dharura hulazimika kuifunga shule, jambo ambalo lilikuwa linawanyima watoto fursa ya kujifunza.

Matarawe ni shule iliyoanzishwa mwaka 2016 ili kuwapunguza umbali wanafunzi waliokuwa wakitembea kilometa saba kwenda katika Shule ya Marungu, ambapo imejengwa kwa nguvu za wananchi.

FikraPevu ilijionea yenyewe majengo mawili yenye vyumba vinne vya madarasa, lakini ni moja tu lenye vyumba viwili na ofisi ambalo limekamilika.

Aidha, nyumba mbili za walimu zimejengwa kwa nguvu za wananchi, ambapo mojawapo bado haijakamilika.

Jengo lenye vyumba viwili na ofisi ya walimu ambalo bado halijakamilika ingawa tayari chumba kimoja kinatumiwa na wanafunzi.

Chumba ambacho kinatumiwa na wanafunzi wa darasa la awali katika jengo ambalo bado halijakamilika.

Jengo ambalo limekamilika kwa ndani ingawa bado halijamaliziwa vyema.

Mwalimu Msuha alimshukuru Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa kumpatia mwalimu, lakini akamshukuru pia mkuu huyo wa wilaya kwa kuchangia Shs. 1.5 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la pili lenye vyumba viwili pamoja na ofisi ya walimu.

“Tunamshukuru sana mkuu wa wilaya kwa mchango wake, tunawashukuru pia JamiiForums ambao walifuatilia kwa karibu na kuripoti changamoto hii na hatimaye serikali kuchukua hatua… hata hivyo, tunaiomba halmashauri ituongeze mwalimu mwingine, wa kike, mara ajira mpya zitakapotoka,” alisema Mwalimu Msuha.

Hata hivyo, FikraPevu imebaini kwamba, licha ya kuwepo kwa matundu nane ya vyoo, lakini bado  havina ubora pamoja na kuwepo kwa ukosefu wa maji japokuwa vyanzo vya maji vipo karibu.

Mkoa wa Ruvuma unakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa umma ambao wanakadiriwa kufikia  7,747 huku sekta ya elimu ikiongoza kwa upungufu wa walimu 3,456 ikifuatiwa na sekta ya Afya ikiwa na upungufu wa watumishi 2,472.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, licha ya kujazia walimu katika shule zilizokuwa na upungufu mkubwa, lakini wilaya hiyo bado ina uhaba mkubwa wa walimu, ambapo ina walimu 737 tu katika shule 106 za msingi zenye jumla ya wanafunzi 35,381.

Kwa wastani wa haraka, inaonyesha kwamba shule moja inapaswa kuwa na walimu saba huku uwiano wa wastani ukiwa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 48, lakini uhalisia ni kwamba, shule za mjini ndizo zenye walimu wengi kuliko zile za vijijini ambako wengi wanakimbia kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu bora, huduma za jamii pamoja na uhaba wa nyumba za watumishi.

Wilaya ya Nyasa ilimegwa kutoka Wilaya ya Mbinga mwaka 2013, ambapo wakati huo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ilikuwa na walimu 2,117 tu, kati yao wanaume 1,185 na wanawake 932.

Kwa ujumla, Mkoa wa Ruvuma wenye shule za umma 732 na za binafsi 10 (kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2012), una jumla ya walimu 6,103 tu, kati yao wanaume ni 3,344 na wanawake 2,759.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Oscar Mbyuzi, hawakuweza kupatikana kutokana na kutingwa na majukumu ya nje ya ofisi hadi FikraPevu ilipoondoka wilayani humo.

Uhaba wa walimu katika shule hiyo na nchini Tanzania kwa ujumla unaonekana kuwa changamoto katika utekelezaji wa Lengo Namba Nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG) linalosisitiza elimu bora.

Lakini hivi karibuni serikali ilitangaza kwamba itatoa ajira katika sekta kadhaa, ikiwemo ya elimu na afya, ambayo nayo ina upungufu mkubwa wa watumishi.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *