Siku moja baada ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoa ufafanuzi wa hali ya uchumi nchini, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amekamatwa na kuhojiwa na polisi kwa tuhuma za kutoa takwimu za uongo na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Zitto Kabwe ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini ameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, akituhumiwa kwa kuchapisha taarifa kinyume na kifungu namba 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao na kutoa takwimu za uongo kinyume na kifungu namba 37 (5) cha Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
Zitto anakuwa miongoni mwa viongozi wa upinzani ambao wamewahi kukamatwa kwa tuhuma za uchochezi. Mara ya mwisho kukamatwa alikuwa Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kigaila Benson ambaye alikamatwa na kuhojiwa na polisi kabla ya kuachiwa kwa dhamana.
Taarifa za kukamatwa kwa Zitto zilianza kuenea leo asubuhi, ambapo Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT -Wazalendo, Ado Shaibu alithibitisha kukamatwa kwa kiongozi huyo ambaye alipelekwa katika Kituo Cha Polisi cha Chang’ombe lakini alipata dhamana na kuruhusiwa kutoka katika kituo hicho.
Muda mfupi baada ya kupata dhamana, taarifa ya ACT Wazalendo imesema Zitto amekamatwa tena kwa amri ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuhojiwa juu ya kauli zake ambazo amekuwa akizitoa kwa nyakati tofauti ambazo zimetajwa kuwa za uongo.
Akitumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari Zitto amekuwa akitoa taarifa na takwimu za hali ya uchumi ambazo zinatofauitiana na zile za serikali.
Oktaba 29 mwaka huu akiwa katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa marudio katika kata ya Kijichi, jijini Dar es salaam, Zitto aliendelea kusisitiza kauli yake ya juu ya hali mbaya ya uchumi na kutofautiana na takwimu za serikali ambazo zinaonyesha uchumi umeimarika na mapato ya nchi yameongezeka.
Zitto Kabwe, akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuachiwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi, Dar es salaam
Fikra Pevu imepata hotuba aliyoitoa katika mkutano huo wa kampeni ambapo sehemu ya hotuba hiyo inaeleza kuwa “Hali ya uchumi wa Nchi ni mbaya sana, ni mbaya mno kinyume kabisa na takwimu zinazotolewa na kuonyesha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi kuwa kubwa kwa kiwango cha 7%. Mimi ni mchumi, pamoja na wachumi wenzangu wengi tunajua kuwa shughuli za uchumi zimedorora, na nyie wananchi ni mashahidi juu ya hali mbaya ya uchumi wa nchi, hili ni jambo la dhahiri kabisa”.
Taarifa za Mbunge huyo, ziliripotiwa kuwa ukuaji wa Pato la Taifa kwa robo ya pili ya mwaka 2017 ni asilimia 5.7 badala ya asilimia 7.8 ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali, huku akisisitiza kuwa 5.7% ilikuwa ni kwa robo ya kwanza ya Januari hadi Machi 2017.
Oktoba 30 mwaka huu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilijitokeza kufafanua utata uliojitokeza, ambapo kupitia Meneja Mkuu wa Takwimu za Pato la Taifa, Daniel Masolwa alisema takwimu zilizotolewa na Zitto juu ya ukuaji wa Pato la Taifa kwa robo ya pili ya mwaka kuanzia 2013 hadi 2017 sio sahihi.
Meneja huyo alinukuliwa akisema taarifa sahihi ni kuwa “Takwimu rasmi kwa mwaka 2013 ni (6.3), 2014 (9.8), 2015 (6.5), 2016 (8.5) na 2017 ni 7.8 wakati takwimu zisizo rasmi za Zitto Kabwe ni 2013 (7.0), 2014 (8.6), 2015 (5.7), 2016 (6.8) na mwaka 2017 ni 5.7”.
Mkanganyiko huo wa takwimu uliotolewa na Zitto Kabwe na Ofisi ya Takwimu bado umeendelea kuibua mijadala mbalimbali ya wananchi kuhusu hali ya uchumi na ukuaji wa Pato la Taifa nchini.
Mara ya mwisho Zitto kukamatwa ilikuwa Septemba 20 mwaka huu katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Kigoma, ambapo alisafirishwa hadi Dodoma kuhojiwa na Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za kudhalilisha muhimili wa Bunge.
Kutokana na tuhuma hizo, amehojiwa na kuachiwa kwa dhamana ambapo ametakiwa kuripoti tena siku ya Jumanne ya wiki ijayo katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya kupewa maelekezo.