Licha ya pato la ndani la bara la Africa kwa sehemu kubwa kuchangiwa na uchumi usio rasmi, serikali na mashirika ya kimataifa yakiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) wanapingana na uchumi huo na kuhimiza mifumo rasmi ya sekta ya ukusanyaji mapato.
Uchumi usio rasmi kwa Afrika ni biashara kubwa ambayo haiwezi kuzuilika. Shirika la Kazi Duniani (ILO) linakadiria kuwa sekta hiyo inachangia asilimia 41 ya pato la ndani la Afrika, ambapo hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine. Afrika Kusini huchangia chini ya asilimia 30 na 60% kwa Nigeria, Zimbabwe na Tanzania.
Pia inatoa ajira nyingi kwa vijana. Inawakilisha robo tatu ya ajira zote nje ya kilimo, na asilimia 72 ya ajira zote za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Inaelezwa kuwa 93% ya ajira zote zilizotengenezwa miaka ya 1990 zilikuwa ni za sekta isiyo rasmi.
Shirika la Kazi Duniani linaelezea uchumi usio rasmi ni shughuli zote za kiuchumi ambazo zina wafanyakazi na vitengo lakini haziendeshwi kwa mfumo rasmi.
Kutokana uchumi huo kukuwa kwa kasi na kuonyesha matumaini kwa vijana wengi, serikali na mashirika ya kimataifa imekuwa ikibuni njia rahisi za kuboresha sekta hiyo ili kujipatia kodi na takwimu muhimu za kiuchumi.
Hata hivyo, juhudi hizo zimekuwa zikiibua malalamiko na migongano baina ya serikali na wafanyabiashara wadogo ambao huuza bidhaa kwenye mikusanyiko ya watu na barabarani.
Sekta hiyo pia inachochewa zaidi na kutokuwepo kwa miundombinu muhimu na sekta ya mashirika ya biashara. Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaeleza kuwa sekta isiyo rasmi itaendelea kukuwa kila Siku ikizingatiwa kuwa inaajiri watu wengi wakiwemo wasomi wa vyuo vikuu ambao wamekosa ajira kwenye sekta rasmi.
Hii sio habari njema kwa serikali za Afrika ambazo zinashinikizwa na mashirika ya fedha duniani kuboresha sekta hiyo kuwa rasmi ili kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato.
Changamoto nyingine ni matumizi ya teknolojia ya kisasa ambayo kulingana na watafiti wa Shule Kuu ya Uchumi ya Uingereza (new white paper) wanaeleza teknolojia inaweza kuboresha au kuididimiza sekta hiyo kulingana na kada ya watu wanaokusudiwa.
Utafiti huo unabainisha ili sekta isiyo rasmi ikue ni muhimu elimu ya teknolojia ipejezwe katika shughuli za wajasiriamali kuimarisha sekta nyingine za kilimo, usafiri, pesa ya mtandao na ajira.
Hata hivyo, watafiti hao wanaeleza kuwa ikiwa mfumo huo wa digitali ukiruhusiwa unaweza kuharibu mfumo wa sekta isiyo rasmi kwa kuwatoa wafanyabiashara wadogo kwenye maeneo yao. Pia inaweza kupunguza idadi ya wafanyakazi kwasababu kazi nyingine zitaratibiwa na mfumo wa kompyuta.
Wanaenda mbali na kuongeza kuwa ikiwa teknolojia hiyo ina lengo la kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za miamala na ajira uwezekano wa wafanyabiashara wengi kuachwa nyuma ni mkubwa.
Wanashauri msisitizo uegemea zaidi kuwajengea ujuzi na maadili, hifadhi za kijamii na mafao yao umma kwa watu maskini ambao ndio wahusika wa sekta isiyo rasmi.
Pia kuzingatia maslai mapana ya wananchi na upatikanaji wa soko la uhakika linalochochewa uvumbuzi wa digitali.