Soko Kuu la Bukoba Mjini kubomolewa

Phinias Bashaya

WAFANYABIASHARA wa soko kuu mjini Bukoba wamepewa muda wa miezi mitano kufanya maandalizi ya kuhama ikiwa kama kengele ya mwisho kabla ya soko halijabomolewa na kujengwa upya.

Kwa zaidi ya kipindi cha nusu karne soko hilo limeendelea kuwa kama lilivyo,  likishindwa kuhimili utoaji wa huduma zenye sifa ya kiwango cha wananchi wanaoishi ndani ya Manispaa kama ilivyo katika miji mingine.

soko-bukoba

Manispaa ya Bukoba imetoa ofa ya miezi mitano tangu Julai hadi Novemba na katika kipindi hicho wafanyabiashara hawatatozwa ushuru wala kodi yoyote ili wakusanye nguvu ya kuhama na kupisha ujenzi wa soko jipya.

Tangu kutangazwa kwa mpango huo, wafanyabiashara walionekana kutofautiana na hata malumbano yao kuwafumbua macho walioko nje ya soko baada ya kufichua siri nzito iliyofichika miaka mingi.

Kwamba ndani ya soko hilo kuna mfumo sugu wa ‘Nyarubanja’ambao uliwezesha kundi dogo kumiliki maeneo mengi ya biashara ambayo huyakodisha kwa gharama kubwa huku wakipeleka malipo kiduchu Manispaa.

Hivyo ujenzi wa soko jipya ilikuwa ni zaidi ya habari  mbaya kwa kundi hilo kwani ulikuwa unavunja mfumo wa Nyarubanja na badala yake kuwepo kwa utaratibu mpya ambao utakuwa wazi zaidi tofauti na sasa.

Mfumo huo unadaiwa kuasisiwa na Madiwani ambapo baadhi yao baada ya kuwa madarakani kwa muda mrefu walitumia nafasi hiyo kuhodhi maeneo mengi kwa kuwashawishi viongozi wa Manispaa.

Kwa muda mrefu utaratibu wa kupangisha maeneo ya biashara katika soko kuu la Bukoba ulitawaliwa na utata kutokana na maeneo mengi kumilkiwa na kundi dogo ambalo nalo hupangisha maeneo hayo kwa watu wengine.

sokoni-bukoba

Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara hao wameanza kuhamisha  shughuli zao na kutafuta maeneo mengine katika mitaa mbalimbali ikiwa ni dalili ya kukubali kuwa uboamoaji wa soko sasa haukwepeki.

Miezi miwili iliyopita maduka mapya yameibuka kwa kasi katika mitaa ya Uswahilini, Nyakanyasi, Kashai na kwenye vichochoro vya mji wa Bukoba na wengi wanatajwa kuwa wafanyabiashara wanaohama kutoka sokoni.

Hali hiyo pia imechangia kupanda kwa bei ya kukodisha vyumba vya biashara, ambapo katika mtaa wa Kashenye kodi imepanda na kuwa kati ya shilingi elfu thelathini na arobaini kwa mwezi tofauti na ilivyo kuwa kabla ya kuwepo kwa taarifa za kuvunja soko.

Kauli ya Kagasheki

Balozi Khamis Kagasheki ambaye ni Mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini anasema ujenzi wa soko jipya haukwepeki na soko linalotumiwa na wafanyabiashara kwa sasa halikuwahi kubadilika tangu akiwa kijana mdogo.

Anasema haikubaliki wafanyabiashara kuendelea kufanyia shughuli zao katika soko kuu kuu ambalo halina miundombinu bora inayokwenda sambamba na wananchi wanaohitaji huduma za soko hilo kutoka ndani na nje ya mji.

Pia anashangazwa na baadhi ya wafanyabiashara wanapinga ujenzi wa soko jipya kwamba hiyo ni miongoni mwa ahadi zake kubwa alizozitoa wakati akiomba kura kwa wananchi katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Wakati naomba kura nilihaidi ujenzi wa soko jipya, nakumbuka wananchi walishangilia na kupiga makofi, hili lililopo limechoka na limekuwepo tangu nikiwa kijana lazima tukubali mabadiliko ujenzi wa soko jipya haukwepeki”anasema Balozi Kagasheki

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Zipolla Pangani anasema mbio za kusaka maendeleo ya mji wa Bukoba lazima ziende sambamba na kubadili taswira ya mji kupitia utekelezaji wa miradi mbaimbali likiwemo soko kongwe la mji huo.

Anasema mji huo unatakiwa kushindana na miji mingine katika nyanja mbalimbali hasa kuboresha na kuwa na maeneo yanayovutia tunapoelekea shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki alilosema kasi yake ni mkubwa.

Anasema ni lazima wananchi wakubali mabadiliko chanya yanayoendana na mikakati inayotekelezeka na kuwa hakuna sababu ya kushindwa kujenga soko jipya wakati uwezo wa kufanya hivyo upo.

Mkuu huyo wa Wilaya anasisitiza kuwa ni bora kuwa na mtazamo wa kusonga mbele na hapa anaomba Rais Jakaya Kikwete asimhamishe katika mji huu kabla ya soko jipya halijajengwa na kukamilika.

Aidha, anaongeza kwa kusema kuwa Bukoba ni mji pekee unaopakana na nchi nyingi za Jumuiya ya Afika Mashariki na hautakiwi kuendelea kuwa hivi ulivyo kama wananchi wake wanataka kuingia katika ushindani wa biashara kimataifa.

Ujenzi miezi 18

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Hamis Kaputa anasema baada ya soko kubomolewa wafanyabiashara hawatakaa nje ya soko kwa muda mrefu kwani ujenzi utachukua kipindi cha miezi kumi na nane tu.

Anasema miongoni mwa masharti atakayopewa mkandarasi baada ya tenda kutangazwa ni pamoja na uhakika wa kumaliza kazi hiyo kwa muda uliotajwa ili wafanyabiashara waweze kuendelea na shughuli zao kwa kuafuata utaratibu mpya utakaowekwa.

Kuhusu haki za wafanyabishara waliopo, Kaputa anasema wameanza kuhakiki majina ya wale waliopo na kuwa hao ndio watapewa kipaumbele cha kupangishwa baada ya ujenzi kukamilika na kuwa hakuna mfanyabishara yeyote aliyeko sokoni atakayepoteza haki yake.

Hata hivyo anasema wamelazimika kufanya uhakiki wa majina bila kujali kama mfanyabiashara ana mkataba ili hata wale waliopangishwa na watu wengine waweze kupewa maeneo yao ya biashara baada ya ujenzi kukamilika.

“Wote wana haki sawa na kila aliyeko sokoni atarudi, tunahakiki hata yule aliyepangishwa na mwingine ili naye baadaye awe mpangaji bila kulazimika kupitia mgongo wa mtu mwingine” anabainisha Kaputa

Mshangao wa Meya wa Manispaa hiyo Dokta Anatory Aman ni jinsi zoezi la uhakiki lilivyoibua kundi dogo la ‘Nyarubanja’ ambapo mmoja wa wapangaji mbaye pia anapangisha  ana maeneo zaidi ya kumi ya kufanyia biashara.

Anasema utaratibu mpya utakaotumika baada  ya ujenzi kukamilika utatoa nafasi kwa wafanyabiashara wengi kuwa na mikataba yao na kumiliki maeneo tofauti na sasa ambapo wananyonywa na wanaowapangisha.

Pamoja na kutokuwa tayari kuyari kutaja gharama halisi za mradi huo kwani hata utaratibu wa tenda haujatangazwa alisema soko jipya litakuwa na uwezo mkubwa  na kufanya kila aina ya biashara kuwa na nafasi yake.

Anasema miongoni mwa maandalizi yaliyofanyika ni kuhainisha maeneo mbadala watakapohamia wafanyabiashara kwa muda na tayari Manispaa imeandaa michoro kwa ajili ya kuboresha maeneo hayo.

Maeneo hayo ni pamoja na kuboresha masoko ya Nyakanyasi na Kashai, kiwanja cha Bukoba Sekondari kilichopo Mafumbo ambapo baadhi ya wafanyabiashara wengine watahamia  uwanja wa jengo la CCM kwa muda.

Anasema soko jipya litakuwa na maeneo ya uwekezaji na hivyo kuvutia wafanyabiashara wa aina mbalimbali kupitia shughuli ambazo zitaongeza pato la wananchi baada ya kuongezeka maeneo ya kufanyia biashara.

Dokta Aman anasema ni sera kandamizi na kuwaletea wananchi umasikini kufunga soko kila siku za Jumapili na sikukuu, ambazo baadhi ya wafanyabiashara haziwahusu na wangependa kuendelea na shughuli zao kwani wanaohitaji huduma hata siku hizo wapo.

Ni mwezi mmoja sasa tangu aondoe utaratibu huo uliodumu kwa miongo kadhaa katika soko hilo ambapo wafanyabiashara wanaonekana kufanya shughuli zao pamoja na upungufu wa wateja huku huduma nyingine zikiwa zimefungwa.

Hofo ya wafanyabiashara

Tangu Manispaa kutangaza dhamira ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko jipya wafanyabiashara wengi walikubwa na hofu ya kutofahamu hatima yao kabla na baada ya ujenzi wa soko jipya kukamilika.

Pamoja na tofauti ndogo iliyopo miongoni mwao, idadi kubwa ya wafanyabiashara wanakubaliana na mpango wa ujenzi wa soko jipya kwani wamehaidiwa kupewa kipaumbele cha kupanga maeneo ya biashara  baada ya ujenzi kukamilika.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Habibu Mayoro anasema Manispaa inawashirikisha katika hatua mabli mbali ikiwemo zoezi la kuhakiki majina ya wafanyabiashara walioko sokoni na hawaoni sababu ya kupingana na mipango ya ujenzi wa soko jipya.

Hata hivyo hofu ya Geraldina John ambaye ni mfanyabiashara wa ndizi katika soko hilo anasema huenda wakapoteza wateja wa bidhaa hiyo kutokana na umbali wa maeneo watayotakiwa kuhamia.

Kwa upande wake Zainabu Marijani mpangaji katika banda namba tisa eneo la mitumba anasema yuko tayari kuhama ingawa anatoha tahadhari kwa Manispaa juu ya ukweli wa ahadi yake ya kuwapa kipaumbele cha kurudi kama wapangaji wapya.

Naye Rashid Ismail ambaye ni mfanyabishara wa nyama bucha namba tisa na kumi anataka kabla ya maeneo yao kuvunjwa lazima wakubaliane kwanza nani analipa fidia kwani wamefanya ukarabati mkubwa wa maeneo yao kwa gharama kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Anasema kimsingi kwa ukarabati uliofanyika bado wanaidai Manispaa gharama walizotumia kuboresha maeneo yao ya biashara na ni bora wakaelezwa kwanza hatima ya jambo hilo kabla ya ubomoaji kufanyika.

Naye Audax Mathias mtengeneza mihuri na fundi cherehani katika soko hilo anataka zoezi la kuhakiki majina ya wafanyabiashara walioko sokoni lifanyike kwa umakini ili kuepuka uandikaji wa majina hewa au wasiokuwa wafanyabiashara katika soko hilo.

Vyovyote iwavyo Bukoba inahitaji viongozi watakaodhubutu kuanzisha na kusimamia safari ya mabadiliko na kukabili changamoto mbele ya safari ambayo ni lazima yaanze sasa ikiwemo ujenzi wa soko jipya .

Phinias Bashaya-Mwandishi wa FikraPevu – Kagera

3 Comments
  • halmashauri itoe muongozo namna gani wafanya biashara wa soko hilo watarejeshwa katika soko hilo baada ya ujenzi wake kukamilika vinginevyo itakuwa ngumu sana kwa wao kurudi sokoni hapo baada ya ujenzi kukamilika.

  • Ndugu Mwambungu,hoja yako ni ya msingi sana,pale Bukoba kuwa ombwe kubwa la kiuongozi Wafanyabiashara wanyonge,watarudi soko kuu kwenda kuemea tu si kupata meza na kuendelea na maisha yao ya kufanya biashara kama walivyozoea.Namaanisha hawatakuwa na uwezo wa kulipia gharama mpya za kukodi vibanda.

  • napenda na vyo ona mabadiliko ya nakua sana mikoani serikali na jamii kwa ujumula tusikate tama tukazane tupinge atua na bukoba yetu ni nzuli na iwe mfano kwa wengine.

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *