Siku chache zilizopita Marekani imekuwa ikitangaza hatua kadhaa za kulinda soko lake kwa kubadilisha utaratibu uliofuatwa na serikali zilizopita na kuamua kutoza ushuru kwa baadhi ya bidhaa zinazoingia Marekani.
Kwa mujibu wa matokeo ya “ukaguzi wa kipengele cha 301 cha sheria ya biashara ya Marekani”, Marekani imesema itaongeza ushuru wa forodha kwa baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka China.
Rais Donald Trump alisema thamani ya ushuru wa forodha kwa bidhaa hizo inaweza kufikia dola za Marekani 60 Bilioni. Tayari ameielekeza ofisi ya idara ya biashara ya Marekani iandae mpango kazi kuhusu ongezeko la ushuru wa forodha dhidi ya bidhaa za China. Pia ameiagiza ofisi hiyo iishitaki China kwa Shirika la Biashara Duniani (WTO), kuhusu mambo mbalimbali ambayo Marekani inaona ni ukiukaji wa sheria za biashara za kimataifa.
China haikukaa kimya na ilisema kama Marekani ikitekeleza maamuzi hayo, basi itajibu. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Bibi Hua Chunying ameikumbusha Marekani kuwa hii ni karne ya 21, zama ya kuendesha biashara kibabe zimepita.
Naye Naibu waziri wa mambo ya nje wa China, Zheng Zeguan alisema nchi yake haitaki vita ya biashara, lakini kama ikitokea basi Marekani ijue kuwa China haitaogopa.
Wataalamu wa uchumi kutoka nchi mbalimbali duniani wamekuwa wakichambua hali hii, ambayo wanaona kuwa inaweza kuzusha vita ya biashara baina ya mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa ya kiuchumi duniani na kuathiri nchi nyingine.
Akiongea na idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, Mhadhiri wa Idara ya uchumi na fedha ya Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dr. Genuine Martin amesema sera ya kujilinda kibiashara inayofuatwa na Marekani chini ya uongozi wa Rais Donald Trump, inaweza kuwa ni sera inayofurahisha baadhi ya watu kwa sasa, lakini haisaidii maendeleo ya muda mrefu ya uchumi wa nchi hiyo na pia inaweka vizuizi vikubwa kwa maendeleo ya biashara ya kimataifa.
Dr. Martin amesema, "Trump anaona kuwa Marekani kuongeza ushuru kwa kiasi kikubwa dhidi ya bidhaa za China kutaleta hasara kwa China pekee na kufanya bidhaa zitakazoagizwa kutoka China nchini humo zipungue na bei zake ziongezeke. Lakini Marekani inatakiwa kutambua kuwa bidhaa nyingi za China zina ushindani zaidi katika soko la kimataifa kuliko bidhaa za Marekani”.
Inawezekana kuwa biashara kati ya Marekani na China, au hata nchi nyingine duniani haina uwiano, lakini changamoto kubwa inayopunguza nguvu ya ushindani ya Marekani ni gharama kubwa za uzalishaji na kuifanya iachwe nyuma. Changamoto hiyo inaitaka Marekani kurekebisha muundo wake wa uzalishaji na kuboresha bidhaa zake ziwe na nguvu ya ushindani, na sio kuweka vizuizi.
Dr. Martin amesema, “kama Marekani itaendelea kutofuata kanuni za Shirika la Biashara Duniani, ukubwa wa biashara duniani huenda utapungua na nchi nyingine zitaweza kuchukua hatua kupinga bidhaa za Marekani kuingia kwenye masoko yao ya ndani, hii haitasaidia maendeleo ya uchumi wa Marekani, wala haisaidii ushindani mzuri wa soko la kimataifa na mustakabali wa biashara ya kimataifa, uwekezaji wa pande nyingi na uchumi wa dunia utadhoofika."