Serikali kushirikiana na Switzerland kuwajengea uwezo watumishi wa umma

Jamii Africa

Serikali imeiomba Switzeland kuangalia uwezekano wa kutoa mafunzo kwa madaktari Bingwa na kuwajengea uwezo watumishi wa umma ili kuongeza  ufanisi kati utoaji huduma kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa wakati wa Mkutano Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Isdor Mpango na Balozi wa Switzerland hapa nchini, Florence Tinguely Mattli, ulioangazia uhusiano kati ya nchi hizo mbili na namna ya kuboresha ushirikiano.

Katika Mkutano huo Waziri Mpango amemuomba Balozi huyo kuangalia uwezekano wa kuwapa mafunzo madaktari Bingwa nchini ili kukidhi uhitaji uliopo hasa katika Jiji la Dodoma ambalo ndio makao Makuu ya Nchi na  idadi ya wakazi wake inaongezeka, na pia kufadhili mafunzo kwa Watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo katika kada mbalimbali lengo likiwa ni  kuongeza ufanisi wa kazi.

Aidha waziri Mpango aliongeza kuwa Tanzania ina mifugo mingi lakini bado haijafaidika na rasilimali hiyo. Imeiomba Switzeland kuwekeza teknolojia ya kisasa katika sekta hiyo ili kuwatengenezea ajira watanzania.

“Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika lakini ufugaji wa mifugo hiyo hauna ubora, kwa kuwa Switzerland imeendelea katika Sekta ya Mifugo fursa ipo ya uwekezaji katika eneo hilo hapa nchini” amesema Dk. Mpango.

Waziri wa Fedha na Mipango. Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango(Mb), akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Switzerland Nchini  Bi. Florence Tinguely Mattli (kushoto) kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Khatibu Kazungu Jijini Dodoma.

Amesema kuwa Serikali ya Tanzania inafanya jitihada mbalimbalimbali kukabiliana na umasikini hivyo ni vema Washirika wa Maendeleo wakatambua kuwa hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua kama kupambana na wakwepa kodi na kuboresha mikataba zina lengo la kuboresha maisha ya watanzania  kwa kuhakikisha wananufaika na rasilimali nyingi zilizopo.

Waziri Mpango amesema kuwa Switzerland inashiriki kikamilifu katika  miradi ya Matumizi bora ya misitu hususani Mkoani Morogoro, kuboresha ujuzi na kukuza ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wake Balozi wa Switzerland nchini, Florence Tinguely Mattli, amesema kuwa Uhusiano kati ya Nchi yake na Tanzania umezidi kuimarika na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania  katika sekta mbalimbali za maendeleo huku akisisitiza suala la kuzingatia uwazi na mazingira bora ya uwekezaji  kwa kuwa ni chachu kubwa ya kuvutia uwekezaji wenye tija kwa pande zote mbili.

Dk. Mpango amemhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali inatoa na itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika katika suala la uwekezaji kwa kuwa Tanzania inaongozwa  kwa utawala wa sheria unaozingatia haki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *