ZAMA za kuwepo kwa mbolea zisizo na viwango zinaweza kuwa historia ikiwa kanuni za ununuzi wa pamoja wa mbolea zinazoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) zitatekelezwa.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, hivi sasa TFRA imeandaa kanuni za mfumo wa manunuzi ya mbolea kwa pamoja ili kuongeza upatikanaji na kupunguza bei ya mbolea kwa wakulima.
Hali hiyo, kwa mujibu wa uchunguzi, itaepusha uwepo wa mbolea zisizo na viwango na kudhibiti mfumo wa bei ambao unawaathiri wakulima wanaoshindwa kumudu gharama za pembejeo.
Chini ya TFRA, mfumo huo utasaidia kuimarisha usambazaji wa mbolea ambapo wadau watapata mbolea kwa ushindani na utawawezesha wafanyabiashara wadogo kukua na kushiriki katika biashara hiyo na kuimarisha mtandao wa usambazaji hadi ngazi ya mkulima.
“Mfumo huo utadhibiti bei ya mbolea iwapo kutajitokeza ongezeko lisilo na sababu na utaongeza ufanisi wa kudhibiti mbolea kutoka nje ya nchi kwa kuingiza mara chache kwa kiwango kikubwa,” alisema Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba.
Akiwasilisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2017/2018 Bungeni mjini Dodoma hivi karibuni, Dkt. Tizeba alisema Mamlaka hiyo ina jukumu la kusajili mbolea na kutoa vibali kwa kampuni na mawakala wa mbolea nchini.
Dkt. Tizeba aliongeza kusema kuwa Mamlaka hiyo itakuwa na jukumu la kudhibiti soko la pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam kwa Serikali na Taasisi zinazojishughulisha na masuala ya kilimo na mbolea.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Lazaro Kitandu, alisema kwamba, kabla ya kuanzishwa Mamlaka hiyo kulikuwa na matatizo ya utunzaji na utumiaji wa mbolea yenye kiwango kinachotakiwa na hivyo kufanya kuwepo kwa tatizo la upatikanaji wa mbolea bora ambayo inakidhi viwango.
Kaimu Mkurugenzi huyo alieleza kwamba, Mamlaka hiyo imeundwa mahsusi kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa bidhaa hii ya mbolea kuanzia inapotengenezwa, kusafirishwa hadi kutumiwa na wakulima.
“Mamlaka inafanya ukaguzi katika maghala, maduka na Mawakala wa mbolea hapa nchini ili kuhakikisha kuwa mbolea waliyonayo ina ubora unaotakiwa kabla ya kuwauzia wakulima,” alisema Kitandu.
Akizungumzia namna TFRA inavyofanya kazi ya udhibiti, Kitundu alisema kuwa mbolea inapoingizwa nchini wanapima sampuli katika maabara zilizopo katika vituo vya utafiti wa kilimo vya hapa nchini.
Alizitaja maabara hizo kuwa ni pamoja na vituo vya TPRI na Seliani vilivyopo mkoani Arusha, Mlingano Tanga, Sokoine Morogoro, na maabara ya TORITA iliyopo Tabora ambayo ni maalumu kwa ajili ya kupima mbolea ya tumbaku.
“Kabla ya kuwafikishia wakulima, wafanyabiashara na wakala wanawajibika kufikisha sampuli za mbolea katika maabara ambazo zipo karibu nao,” alisema Kitandu.
Alifafanua kwamba, tasnia ya mbolea hapa nchini bado ipo chini kwani asilimia 90 ya mbolea yote inayotumika inatoka nje ya nchi ambapo makampuni na mawakala binafsi ndio waingizaji wa mbolea hiyo.
Makampuni yanayoleta mbolea hapa nchini ni Premium Agrochem Ltd, ETG Inputs Ltd, TFC, DRTC Trading Company, STACO, Elia-gro Company Ltd, TATA Africa Holdings, Mohamed Enterprises (T) Ltd, Yara (T) Ltd, Swiss Singapore Overseas Enterprises Ltd na Rubuye Agro-business Company Ltd.
Makampuni mengine ni Agrichem Africa (T), Bajuta International (T) Ltd, Flue and Dark Tobacco Company, Crop Care (T) Ltd,One AcreFund , Nutri care (T) Ltd na Ludod Agro Industy Comp Ltd.
Aidha, Kitandu alisema, nchini Tanzania kuna kiwanda cha mbolea cha Minjingu mkoani Manyara na kinazalisha mbolea kwa matumizi ya ndani na mara chache kinazalisha kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi ambapo mwaka 2016 kiwanda hicho kilisafirisha kiasi kidogo cha tani 74,000 nje ya nchi.
Akizungumzia namna ambavyo wakulima wanaweza kujua kuwa mbolea ipo chini ya kiwango, Kitandu alisema kuwa wanapaswa kuangalia kibandiko kilichopo katika mfuko wa mbolea ambacho kinaonesha muda wa mwisho wa matumizi na virutubisho vilivyomo katika mbolea hiyo.
Sababu zinazofanya mbolea kuwa chini ya kiwango kuwa ni pamoja na kuwekwa juani, kuwekwa katika ghala linalovuja, kuwekwa mahali pa wazi na kufungua mifuko ya mbolea na kuuza kwa ujazo mdogo hivyo kusababisha kupoteza virutubisho.
Kitandu amesisitiza kuwa mtu yoyote anayebainika kuchakachua mbolea au kuuza mbolea ambayo ipo chini ya kiwango atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa leseni, kutozwa faini na kutumikia kifungo jela.
Ameongeza kusema kuwa tangu Mamlaka ianze kufanya kazi, tatizo la mbolea zisizokuwa na kiwango na zilizochakachuliwa limekwisha na amewataka wakulima kutokuwa na wasiwasi na mbolea wanayotumia kwa sasa.
“Tunafanya kazi kwa kushirikiana na Halmashauri zote hapa nchini, hivyo tuna wataalamu kila kijiji, wilaya, na mikoa. Wataalamu hawa wanashiriki katika kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea inayoendana na ukubwa wa eneo” alisema Kitandu.
Akizungumzia mbolea zinazotumika kwa wingi hapa nchini, Kitandu amezitaja kuwa ni mbolea aina ya DAP ambayo ni ya kupandia na UREA ambayo ni ya kukuzia.
Pamoja na ktumika mbolea hizo, Kitundu amesema kuwa mbolea hizo zinatumiwa kwa zaidi ya asilimia 50 ya mbolea zote.
Aina nyingine ya mbolea zinazoingizwa na zinazotumiwa kutoka nje ya nchi ni pamoja na NPK, CAN, SA, MOP, TSP, Biofertilizer na mbolea za maji aina ya “foliar”.
Kuhusu mahitaji ya mbolea nchini Tanzania, Kitandu alisema kuwa yameongezeka tofauti na miaka 10 iliyopita ambapo mwaka 2016 jumla ya tani 380 ziliingizwa na inakadiria kuwa mwaka huu mbolea itakayoingizwa nchini itafikia tani 400 hadi 450.
Taarifa ya Mpango wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017 hadi 2020/2021 inaonyesha kuwa sekta ya kilimo ambayo ni tegemeo kubwa la Watanzania walio wengi imeajiri takriban asilimia 66.9 ya Watanzania wote na inachangia asilimia 23 ya pato la Taifa.
Ni dhahiri uwepo kwa mamlaka ya udhibiti wa mbolea utachochea kukuza kilimo chenye tija kwa kuongeza wingi wa mazao yaliyo bora na kuinua uchumi wa nchi.
Mamlaka ya Kudhibiti Mbolea ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 9, ya Mwaka 2009, na ilianza kufanya kazi rasmi mwaka 2012.