Kagera waanza kuchangamkia kilimo cha alizeti, waitelekeza kahawa

Jamii Africa

BAADA ya bei ya kahawa kudorora katika soko la dunia na bei yake kutokuwa na uhakika Tanzania, kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, wakulima wengi wa  Mkoa wa Kagera wameanza “kuchangamkia” kilimo cha alizeti.

Kahawa ndiyo limekuwa zao kuu la biashara kwa wakazi hao, ingawa wengi sasa wanakata tamaa baada ya kile wanachieleza kuwa ni “kukatishwa tamaa na bei ndogo ya zao hilo” ikinganishwa na mazao mengine yanayolimwa maeneo mbalimbali nchini.

Sababu za mdororo

Baadhi ya sababu zinazotajwa na wataalamu kuchangia kudorora kwa biashara ya zao la kahawa ni pamoja na ubora hafifu unaochangiwa na maandalizi duni kuanzia hatua ya kutayarisha shamba hadi uvunaji.

Wakihojiwa wa FikraPevu baadhi ya vijana wa Wilaya ya Muleba wamesema kuwa kilimo cha kahawa hakiwezi kuwakomboa tena kiuchumi kutokana na bei inayokatisha tamaa na badala yake wameanzisha kilimo cha alizeti.

Mmoja wa viongozi anayeratibu uanzishaji wa vikundi vya kulima zao hilo katika Kata za Kishanda na Buganguzi, Godfrey Kibandwa alisema kuwa tayari wamepata ardhi kupitia serikali za vijiji na hatua inayofuata ni kupata mafunzo.

Alisema kuwa zao la alizeti hata usindikaji wake ni rahisi kwa ajili ya kupata mafuta na soko lake linaaminika ndani na nje ya nchi, tofauti na zao la kahawa ambalo mkulima hapewi nafasi ya kupanga bei pamoja na kutumia gharama kubwa.

Kibandwa aliiambia FikraPevu kuwa tayari vijana wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuunda vikundi vya kuanzisha kilimo cha alizeti na baadhi ya serikali za vijiji katika kata hizo zimeunga mkono wazo lao kama njia ya kujikomboa kiuchumi.

Kijana mwingine ambaye tayari amejiunga na kikundi cha ulimaji wa alizeti, Nikoodemu Benjamin, alisema kuwa kilimo cha alizeti kinachukua muda mfupi na soko lake ni kubwa ikilinganishwa na mazao mengine ya biashara.

KCU waunga mkono

Wazo la vijana hao pia linaungwa mkono na azimio la mkutano wa wakulima wa kahawa kwa mwaka 2016/2017 kupitia Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Kagera(KCU)1990, kilichowataka kujielekeza katika zao mbadala la alizeti

Taarifa ya bodi ya chama hicho iliyowasilishwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama mjini Bukoba na mwenyekiti wake, Frank Muganyizi alisema alizeti itawawezesha wakulima kuwa na kipato mbadala baada ya bei ya kahawa kushuka kila siku

‘’Umefika wakati wa kuanzisha kilimo cha alizeti kama zao mbadala kwa wanachama na wakulima wetu, kwa kuwa bei ya kahawa haiaminiki tena kwa sasa na  inaendelea kushuka kila siku katika soko la dunia, ’’Muganyizi aliueleza mkutano huo.

Pendekezo hilo liliungwa mkono na wanachama wa mkutano huo ambao pia ulipitisha matumizi ya zaidi ya Sh. 100.8 milioni kwa ajili ya ufuatiliaji na usimamizi wa ubora wa kahawa ambapo maandalizi duni yalitajwa kushusha thamani ya zao hilo mnadani.

Bei ya kahawa, alizeti

Katika msimu wa ununuzi wa kahawa wa mwaka jana,  kilo moja ya kahawa ya maganda ilinunuliwa kwa  Sh. 1,100 na ile safi ilinunuliwa kwa Sh. 2,300  huku malengo  ya chama hicho yakiwa ni kukusanya tani 4,000.

Bei ya alizeti imekuwa ikipanda siku hadi siku na soko lake  limesambaa nchi nzima na nje ya nchi, kwani hutumika kutengeneza mafuta ambayo yanaelezwa kutokuwa na lehemu.

Bei hiyo hutofautiana kutoka eneo moja hadi jingine. Hata hivyo katika maeneo mengi, bei ya mbegu za alizeti iliyovunwa muda mfupi shambani kwa kilo ni kati ya Sh. 350 hadi 700 na sokoni ni kati ya Sh. 2500 hadi 3500.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *