April 7 ya kila mwaka ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ambaye alizaliwa mwaka 1905 na kufariki 7 Aprili 1972.
Hayati Mzee Karume ambaye ni Mmoja wa Waasisi wa Taifa, aliiongoza Zanzibar baada ya mapinduzi yaliyomwangusha Sultani aliyekuwa akitawala Zanzibar hadi mwanzoni mwa mwaka 1964. Baada ya miezi mitatu Zanzibar iliungana na Tanganyika iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, na ndipo Muungano wa nchi hizi mbili ukazaa Tanzania.
Mzee Karume alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na aliitawala Zanzibar kwa miaka 8 tu mpaka mauti ilipomkuta Aprili 7, 1972 kwa kupigwa risasi na wabaya wake Kiswandui mjini Unguja.
Historia ya Hayati Karume
Kumbukumbu ya Zanzibar haiwezi kukamilika bila ya kumtaja Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume. Sheikh Abeid Karume alizaliwa tarehe 4 Agosti, 1905 katika Kijiji cha Pongwe eneo la Mwera Kisiwani Unguja. Ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watano wakiwemo wanaume watatu na wanawake wawili. Wote hao ni marehemu.
Historia inaeleza kuwa Abeid alikuwa mtoto wa mkulima, mwenye asili ya kutoka Nyasaland (sasa Malawi) kwa upande wa baba ake bwana Amani Karume na mama Bi Amina binti Kadudu, Mnyarwanda kutoka nchini Rwanda. Wazazi hao walikutana Unguja katika harakati za biashara na hatimaye kufunga ndoa na kuj
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Idara ya Habari Maeleza Zanzibar, Dkt. Juma Mohammed Salum katika maandiko yake ameeleza kuwa, Abeid alikuwa mtoto mtiifu na mnyenyekevu kwa wazazi na mpenzi kwa watoto wenziwe na wakubwa kijijini kwao.
Alipofikisha umri wa miaka minane (8) alipatwa na msiba wa kufiwa na baba mzazi, Amani Karume. Mzee Amani alikuwa ni muhimili wa Abeid kati ya mihimili yake miwili katika malezi yake; baba na mama.
Dkt. Salum anafafanua kuwa, “Haki mojawapo ya msingi ya kupata elimu shuleni iliyumba ingawaje Abeid alianza shule ya msingi Mwera akiwa na miaka minane, haikufua dafu. Mama yake alimpeleka mjini Unguja kwa mjomba wake akaendeleze kisomo chake, nako kulimtupa nje ya shule. Mtoto Abeid Amani Karume hakupata masomo shuleni zaidi ya miaka mitatu, lakini alipata masomo ya ulimwengu zaidi ya miaka ishirini na hivyo kumtia katika kundi la wasomi wa ulimwengu na kufanya vyema masomo ya Maarifa, Historia, Jiografia, Siasa na Haki”.
Marehemu Karume akiwa na baadhi ya wanajeshi baada ya Mapinguzi ya Zanzibar, 1964
Kutokana na kukosa elimu ya darasani, ilimlazimu kutafuta kazi katika bandari ya Zanzibar na baadaye alifanikiwa kuwa baharia ambaye alisafiri katika nchi mbalimbali duniani.
“Utambuzi huo ulimtia katika biashara na uchuuzi mdogo wa bidhaa mjini Unguja na mwisho kuzama katika kazi ya ubaharia ndani ya meli ya Golden Crown mwaka 1920 na kuendelea kuwa baharia katika meli mbalimbali hadi Septemba 23, 1941 alipoacha kazi ya ubaharia”, ameeleza Dkt. Salum katika jarida la Mwendo.
Baada ya kuacha kazi ya ubaharia, Abeid Karume alijiunga na vijana wenzake katika biashara, uchuuzi na kuthubutu kuunda vyama vya michezo, siasa na umoja wa kutetea haki za wafanyakazi na wakulima wa Unguja na Pemba. Hapo ndipo tunu za uongozi zilianza kujitokeza ndani ya akili yake katika kupinga dhuluma zote.
Mwaka 1931 ilianzishwa klabu ya michezo African Sports na baadaye kubadili taratibu za michezo kuwa za siasa chini ya The African Association mwaka 1934 na hatimaye kuunganisha nguvu na kuunda chama cha Afro-Shirazi Association mnamo Februari 5, 1957 ambacho Karume alikuwa mmoja wa viongozi waandamizi.
Dkt. Salum anaeleza kuwa, Chama Cha Afro-Shirazi (ASP) chini ya uongozi wa Sheikh Abeid Amani Karume kilipambana na utawala wa kisultani kupinga uonevu, dhulma, unyonyaji na kudai haki na uhuru wa Mwafrika ndani ya nchi yake.
Kutokana na uonevu wa Sultani, ASP ikishirikiana na Umma Party iliyoongozwa na Abdulrahman Babu, waliunda kamati ya mapinduzi iliyoongoza na kufanikisha mapinduzi ya Januari 12, 1964. Baada ya mapinduzi, ASP na Serikali yake, vikiongozwa na Sheikh Abeid Amani Karume viliweka mapinduzi katika uchumi, elimu, kilimo na afya na kuweka hali za wananchi sawa. Ujenzi wa majengo bora na ya kisasa ulipata kasi ya maendeleo.
Nyumba za maendeleo Michenzani
Ndoto ya kuiongoza Zanzibar yafifia
Ndoto na dhamira yake ya kuleta maendeleo ilikatishwa ghafla siku ya April 7 1972. Sheikh Abeid Amani Karume aliuwawa na wanaotajwa kuwa ni ‘wapinga mapinduzi’ na maendeleo mema ya visiwa vya Unguja na Pemba ambao walitumia mtutu wa bunduki kutoa uhai wa kiongozi huyu mjini Unguja.
Mwandishi na Mchambuzi wa masuala ya kihistoria, Ali Shaban Juma anaeleza kuwa, akiwa ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Chama Cha AfroShirazi (ASP) Kisiwandui mjini Unguja akicheza bao na viongozi wenzake, ghafla alishambuliwa kwa risasi na muuaji aliyedhamiria kufanya uovu huo.
Anaeleza katika moja ya maandishi yake kuwa waliotetekeleza uharifu huo hawakupendezewa na aina ya uongozi wa Hayati Karume wa kuwajali watu maskini na wanyonge kwa kuwaboreshea maisha yao.
Sheikh Abeid Karume akiwa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wao
Miaka 8 ya utawala wake
Katika siku za kuishi kwake, Hayati Karume alikemea zaidi ukabila na kuhimiza utaifa, umoja baina ya wananchi chini ya sera za ujamaa. Katika moja ya hutuba zake anaeleza, “Mwenyezi Mungu hataki viumbe vyake waishi kwa ukabila lakini tuliishi hivyo kwa miaka mingi sana. Kabila lilifika mpaka kuweka binadamu wenziwao katika hali ya utumwa, ikawa kabila moja ni la mabwana na wengine watumwa.
“Wanadamu sote sawa. Sisi ni wamoja, tena wote ndugu, wanadamu wote tuna heshima moja. Hakuna mwanadamu fungu lake limezidi mwenziwe, lakini baadhi ya wanadamu walikuwa wakitumia ukabila”.
Daima alitambua nguvu ya vijana katika ujenzi wa taifa. “Vijana tufanye kazi kwa bidii; tujenge Taifa letu; tujenge imani yetu, tuondoe tofauti zetu; tuwaonyeshe watu nini wanadamu wanaoishi katika utawala wao wana uwezo wa kufanya”.
Katika miaka nane ya utawala wake alifanikiwa kufanya mambo mengi, lakini jambo ambalo wazanzibari wengi wanamkumbuka Hayati Karume ni kuwajengea wananchi wake nyumba za kisasa za kuishi. Mradi huo ilianza Mei 1970 katika eneo la Michenzania ambako ulisambaa katika maeneo mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba.
“ Hapo ndio ulikuwa mwanzo wa urithi muhimu uliotapaa maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba wa ujenzi wa Majumba ya Maendeleo aliotuachia Karume. Jumba lile la mwanzo liligharimu jumla ya shilingi Milioni nne laki saba na hamsini na mbili elfu na lina fleti 132”, ameeleza Dkt. Salum.
Hayati Sheikh Karume ataendelea kuenziwa, kukumbukwa kwa mambo mema aliyoyafanya katika kuwatetea wanyonge na kuboresha maisha wa watu wa Zanzibar. Lakini pia uwezo wake wa kujenga hoja, umoja na ushirikiano katika Muungano wa Tanzania.