Zitto, Ngeleja ‘kupimana vifua’ udiwani Mwanza

Jamii Africa

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe Jumamosi Machi 31, 2012 wanatarajiwa kukabana ‘koo’ katika mikutano yao ya kufunga kampeni za wagombea udiwani katika Kata ya Kirumba Jijini Mwanza.

Zitto Kabwe

Vigogo hao wanatarajiwa kuhutubia maelfu ya wakazi wa Kata hiyo ya Kirumba katika mikutano yao ya kufunga kampeni, zitakazofungwa Jumamosi Machi 31 kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Uchaguzi nchini (Nec), ambapo Jumapili wananchi hao watapata fursa muhimu ya kupiga kura kumchagua mgombea wanayemtaka kati ya wagombea watano wanaochuana katika kata hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ijumaa Machi 30, 2012 jijini Mwanza, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Wilson Mushumbusi alisema Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ndiyo atayefunga kwa kuongoza mkutano huo wa kampeni utakaofanyika viwanja vya Magomeni Kirumba.

Kwa mujibu wa Katibu Mushumbusi, Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ataongozana na viongozi mbali mbali wa Chadema, wakiwemo mbunge wa Ilemela, Nyamagana, Ukerewe, pamoja na makada wa chama hicho.

“Zitto Kabwe ndiyo anakuja kufunga kampeni za Chadema hapa Kirumba, atamnadi mgombea wetu wa Chadema, Dany Bahati Kahungu. Mkutano wetu utafanyika uwanja wa Magomeni…naamini kesho ndiyo tunaizika kabisa CCM!.

“Chadema hatuna presha, ushindi ni wetu maana wananchi wa leo hawadanganyiki na propaganda za CCM. Ninachowaomba wananchi wa Kirumba waje kwa wingi kusikiliza sera nzuri na zenye tija siku hiyo, ili Aprili Mosi wakamchague kwa moyo mweupe mgombea wetu wa Chadema, Kahungu”, alisema Mushumbusi.

William Ngeleja

Kwa upande wake, Waziri Ngeleja alisema ujio wake huo ni wa ushindi kwa mgombea wa CCM, Jackson Robert, maarufu kwa jina la ‘Jack Masamaki’, na kwamba Chadema hawatoki katika uchaguzi huo kwani wananchi bado wanaimani na chama tawala kinachoongoza Serikali.

“Nimekuja kuongeza nguvu na kusherehesha ushindi wa mgombea wa CCM. Naamini wananchi wa Kirumba hawatarudia makosa, maana wanajua pumba ni Chadema na mchele ni CCM”, alitamba Waziri Ngeleja huku akisisitiza ushindi kwa mgombea wa CCM ni asilimia 99.9.

Alisema, kimsingi wananchi wa kata ya Kirumba wanapaswa kutokudanganyika na kelele za wapinzani, kwani hawana lengo jema la kuwaletea maendeleo, bali ni CCM pekee ndiyo yenye dira na shabaha halisi ya kuwaletea maendeleo ya kimaendeleo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Nishati na Madini, iwapo wananchi wa Kirumba watamchagua Robert matatizo yao yatatatuliwa kwa muda mfupi ikiwa ni pamoja na kuletewa huduma ya maji, umeme wa uhakika, barabara pamoja na huduma za afya kuboreshwa.

Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumm – FkraPevu, Mwanza

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *