Wakati bado kukiwa na mjadala wa kubomolewa kwa nyumba za wakazi wa Kimara jijini Dar es Salaam, Rais John Magufuli ameagiza jengo la Shirika la Umeme (TANESCO) lililopo Ubungo kubomolewa ili kupisha ujenzi wa mradi wa ujenzi wa barabara.
Agizo la rais ni utekelezaji ahadi aliyoitoa wakati akiwa Waziri wa Ujenzi katika serikali ya awamu ya nne, ambapo wakati akihitimisha Bajeti ya Makadirio na Matumizi ya wizara yake (2014/2015) alisema hapaswi kulaumiwa katika suala la bomoabomoa kwa watu waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara kwani sheria zimetungwa ili zitekelezwe.
Alinukuliwa wakati huo akisema, “Hata kama halitabomolewa leo, lazima libomolewe tu kwasababu limo ndani ya hifadhi ya barabara, hata akija mtu mwingine, litabomolewa tu”.
Agizo hilo lilimetolewa leo na rais Magufuli alipotembelea eneo hilo ambapo amesema jengo la TANESCO pamoja na majengo ya Wizara ya Maji yanapaswa kubomolewa kwasababu yako ndani ya mita 30 ambazo zinatambulika kisheria kuwa ni hifadhi ya barabara. Kulingana na Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 inaeleza kuwa mtu haruhusiwi kujenga ndani ya mita 30 kutoka barabara kuu.
Eneo hilo la Ubungo ambako yako majengo hayo, unajengwa mradi mkubwa barabara za juu (Interchange roads) ambao umefadhiliwa na Benki ya Dunia na unalenga kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam. Pia mradi huo unalenga kuibadilisha sura ya jiji la Dar es Salaam kwa kujenga barabara za kisasa ili kukuza uchumi ambao unakwamishwa na uchache wa miundombinu inayoingia katikati ya jiji.
Agizo hilo la rais limeibua mjadala mpana kwa wananchi ikizingatiwa kuwa wakati rais Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi na Miundombinu katika awamu ya nne alisisitiza kubomoa majengo yote yaliyo ndani ya hifadhi ya barabara lakini alipata upinzani mkubwa kutoka kwa mabosi wake na hakufanikiwa kutekeleza kwa kiwango alichotaka.
Bomoa bomoa hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa sheria ya mita 30 ambao unaendelea nchi nzima na hivi karibuni wakazi wa Kimara waliojenga katika hifadhi ya barabara waliondolewa na nyumba zao kuvunjwa ili kupisha mradi wa barabara.
Ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara inahusisha miradi mingine 5 ya barabara katika maeneo ya TAZARA, Kamata, Fire, Chang’ombe na Magomeni inayoratibiwa na serikali kwa ushirikiano na wahisani wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia (WB).
Ikizingatiwa kuwa Dar es Salaam ni mji wa kibiashara na viwanda unaochangia asilimia 60 ya mapato yote ya nchi, suala la kutatua changamoto ya foleni ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa jiji hilo ambalo linaakisi sura ya maendeleo ya Tanzania.
Kulingana na ripoti ya uchunguzi ya Twaweza (2010) iliyoangazia njia za kupunguza foleni katika jiji la Dar es Salaam hasa kuzuia magari ya mizigo yanayozidi tani 10 kupita katika barabara zenye msongamano zikiwemo barabara za Bagamoyo, Morogoro, Nyerere na Mandela. Pia kuweka askari wa kutosha katika makutano ya barabara ili kuzuia msongamano usio wa lazima lakini hili linawezekana ikiwa njia za kuingia barabara kuu zitathibitiwa na kuhakikisha magari hayapiti pembezoni.
Pia imeshauri kujenga barabara nyingi za pembezoni ili kuunganisha na barabara kuu ambazo zinakuwa na msongamano mkubwa wa magari.
Maoni ya Wananchi
Hata hivyo, wananchi wametoa maoni yao juu ya uamuzi huo wa rais ambao ni historia kwa majengo makubwa mawili ya serikali kubomolewa ikiwa ni utekelezaji wa sheria.
Mchangiaji wa Mtandao wa JamiiForums anayejulikana kwa jina la Ubungoubungo ameandika, “ Hivi kuvunja lile jengo la Tanesco pale ubungo tukajenga ‘flyovers’ ya uhakika itakayorahisisha barabara zote nne zinazokutana pale ubungo mataa, na kubaki na jengo lile bila flyovers na kukiwa na foleni ya ajabu vilevile, kipi chenye maana zaidi kwa nchi yetu?”
“kipi kinaleta hasara zaidi kuliko kingine? je?, kubaki na lile jengo lakini watu wanachelewa maofisini kutoka Mbezi, kimara na mabasi au magari yanayoelekea mkoani na watu wanafika maofisini kwa kuchelewa hivyo wamepunguza mda wa kufanya kazi na kuendeleza nchi…kipi chenya faida kuliko kingine?”.
Naye WATANABE ameandika, “ Fly over moja haiwezi kutatua tatizo la foleni. Unaweza kuvunja jengo hilo ukajenga fly over Ubungo na magari kuvuka hapo kwa kasi lakini magari hayo yote yatakutana Shekilango, Magomeni, Fire kwa barabara ya Morogoro. Pia yatakutana Buguruni, Tazara barabara ya Sam Nujoma”,
“Suluhisho la msongamano katika jiji hili ni kujengwa kwa barabara za pembezoni kwa kiwango cha lami (Ring roads) ili isiwe lazima kwa magari yote kukutana katika eneo la Ubungo na makutano mengi kama hayo.Hivyo sio busara kuvunja jengo hilo”.