Sheria ya Makosa ya Mitandao ni mtego wa panya, hakuna aliye salama!

Daniel Mbega

UJIO wa Sheria ya Makosa ya Mtandao (The Cyber Crimes Act, 2015) ambayo ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano karibu saa 6 usiku Jumatano, Aprili Mosi, 2015, hauna tofauti na mtego wa panya.

Sheria hiyo, ambayo tayari imekwishaanza kutekelezwa kwa ‘nguvu zote’, ilipitishwa maalum ikiwalenga zaidi wanahabari na hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Lakini hata walioipitisha, ambao walitumia nguvu kubwa na hoja za nguvu badala ya nguvu za hoja, hawakujua kama inawahusu hata wao.

Nitawakumbusha kuhusu kisa maarufu cha Mtego wa Panya, ambao unaingia waliomo na wasiokuwamo. Panya, mnyama mdogo anayeishi porini na nyumbani, anafahamika kwamba ni mharibifu japokuwa ukweli ni kuwa, yeye huwa anatafuta riziki yake bila kujua kwamba anaharibu. Siku moja panya akaubaini mtego aliowekewa uvunguni mwa kitanda na mwenye nyumba ili umnase.

Kwa kujua madhara yake kwamba maisha yake yalikuwa hatarini, akamwendea jogoo wa mwenye nyumba akimuomba amsaidie kuutegua kwa sababu ulikuwa na madhara kwa wote. 

Lakini jogoo akajibu: "Ondoka zako, miye mtego wa panya unanihusu nini wakati sina kawaida ya kufika uvunguni mwa kitanda! Huo ni wako mwenyewe uliyezowea kuchokonoa na kuharibu vitu vya watu."

Panya akamwendea mbuzi wa mwenye nyumba, akasema: "Ewe mbuzi mwema, unajua kuna mtego wa panya uvunguni mwa kitanda cha mwenye nyumba. Tusaidiane mawazo ya kuutegua kabla haujatudhuru wote". 

Mbuzi akajibu: "Tangu lini ukaniona nikiingia chumbani kwa mwenye nyumba, sembuse huko uvunguni mwa kitanda? Mtego huo wa panya haunihusu miye mbuzi".

Panya hakuchoka, akamwendea ng'ombe wa mwenye nyumba, akisema: "Ewe ng'ombe wa bwana, kuna mtego wa panya umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane mawazo namna ya kuutegua kabla haujatuletea madhara".

Ngombe akacheka sana: "Sijapata kusikia jambo la ajabu kama hilo. Yaani, miye ng'ombe nidhurike na mtego wa panya ulio uvunguni mwa kitanda! Mimi na mtego wa panya wapi na wapi! Hilo halinihusu." 

Panya akakosa msaada, lakini akaendelea kuishi kwa mashaka na tahadhari. Ikatokea usiku mmoja nyoka akaingia chumbani kwa mwenye nyumba na katika kutambaa kwake uvunguni mwa kitanda, mkia wake ukanasa mtegoni. Kishindo kilisikika.

Mwenye nyumba, akiamini tayari panya mharibifu amenaswa, bila kujua kwamba ni nyoka aliyenaswa mkia na ana hasira dhidi ya mtu aliyeuweka, yeye akapeleka mkono chini ya vungu wa kitanda ili auchukue mtego huo wenye panya. Hamadi! Nyoka yule mwenye hasira na sumu kali akamng’ata, na jitihada za kuokoa maisha yake zikashindikana, akafa. Usiku huo majjirani wakafika msibani na kesho yake watu wachache wakafika ili kupanga taratibu za mazishi. Wakahitaji kitoweo, hivyo wakamkamata jogoo wa mwenye nyumba na kumchinja. Siku ya pili watu wakaongezeka na kitoweo pia kilihitajika, wakamchinja mbuzi wa mwenye nyumba. 

Siku ya maziko, kwa kuwa watu walikuwa wengi zaidi, akakamatwa ng'ombe wa mwenye nyumba na kuchinjwa! Ni jogoo, mbuzi na ng'ombe wa mwenye nyumba walioamini kuwa madhara ya mtego ule wa panya yasingewahusu wao. Walikosea. Panya alikuwa sahihi, na wala mtego haukumdhuru panya!

Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao haukuwahi kujadiliwa na ulipelekwa Bungeni kwa Hati ya Dharura. Vyombo vya habari viling’amua mapema na kuanza kuupigia kelele kwamba ni mtego ambao utawanasa wote, waliomo na wasiokuwamo.

Wanahabari na Asasi za kiraia walieleza ubaya wa sheria hiyo lakini wakabezwa, wakapuuzwa na kukejeliwa, huku baadhi ya wanasiasa, hasa wenye dhamana ya kutunga sheria, wakiona hiyo ndiyo ilikuwa fursa muhimu ya ‘kuwaminya wambeya’ ambao ‘wanafuatilia mambo yao’, wakaipigia vigelegele.

Wanasiasa wa upinzani pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu waliungana na wanahabari kupiga kelele kuhusu ujio wa sheria hiyo, nao hawakusikilizwa. Hata ile maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu muswada huo yaliyosomwa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mohammed Habibu Mnyaa, Aprili Mosi, 2015, kamwe hayakusikilizwa.

Mvutano mkubwa ukatokea, wabunge wa upinzani wakasusia kikao na kutoka nje, wakabaki wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao waliamua kukaa hadi usiku na kupitisha sheria hiyo. Wakaweka mtego wa panya kwa sababu wao ‘hauwahusu’. 

Nakumbuka Agosti 27, 2015 Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN) iliwaita baadhi ya wahariri na waendesha blogu (bloggers) nchini kujadili ujio wa sheria kadhaa zinazowabana, si waandishi tu, bali Watanzania wote wanaotumia mitandao ya kijamii.

Sheria hizo ni hiyo ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Takwimu, ambazo zilianza kutumika Septemba Mosi, 2015 huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikitangaza kiama kwa wale wanaotumia vibaya na wahalifu wote wa mitandao nchini.

Siyo siri, kwamba, kupitishwa kwa sheria hizo mbili kumeifanya Tanzania kuingia kwenye orodha ya mataifa yenye sheria kali za utumiaji wa mtandao na kuunyonga kabisa uhuru wa kupashana habari.

Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media inayoendesha jukwaa maarufu duniani la JamiiForums pamoja na tovuti ya FikraPevu, ambaye alikuwa mmoja wa wawezeshaji kwenye warsha hiyo, alisema hicho kilikuwa kiama kwa Watanzania wote na hakuna ambaye atabaki salama.

“Lengo la Sheria ya Makosa ya Mitandao ni kuangalia makosa kama vile kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na pia kusambaza picha za utupu za watoto na hata marehemu,” alisema.

Maxence ambaye ni mhandisi wa ujenzi kitaaluma, lakini mpigania uhuru wa kupashana habari hususan katika upande wa uandishi wa mitandaoni, alisema ingawa Watanzania walio wengi hawafahamu Sheria hiyo inawahusu kwa namna gani, lakini kwa lugha rahisi ni kuwa itamuathiri mtu yeyote anayetumia mtandao wa intaneti kwa kutumia kifaa chochote – iwe kompyuta kubwa au vifaa vyenye uwezo wa kufanya kazi kama kompyuta kama simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyoendana na hivyo.

Malengo ya Sheria hii ni kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.

Matumizi ya mitandao yote mikubwa kama Twitter, Instagram, JamiiForums, Facebook, Barua pepe, WhatsApp, blogu na data zote zilizo katika kifaa chochote cha kielektroniki yanaathiriwa kwa kiwango kikubwa na Sheria hii. Hiyo inamaanisha kwamba, jitihada za kuufanya mtandao wa intaneti kuwa wazi ili kila mtu awe na uhuru wa kuunganishwa, kuwasiliana, kuandika, kusoma, kutazama, kuzungumza, kusikiliza, kujifunza, kuunda na kubuni nazo zinafikia kikomo.

Mbaya zaidi ni kwamba, sheria hiyo haijaeleza kuhusu kulinda uhuru wa kugundua na kuunda bila kulazimika kuomba idhini, hatua ambayo itawafanya wanasayansi chipukizi kuogopa kufanya ugunduzi wowote kwa kuhofia kuingia matatani. TCRA inasema Tanzania inaongoza kwa kuwa na watumiaji vibaya wengi wa mitandao ya kijamii, jambo linalosababisha taarifa nyingi za mitandao kutoaminika hadi nje ya nchi kutokana na kujaa uzushi, uongo, uchochezi na lugha na picha za matusi.

Kimsingi hakuna anayepingana kuwepo kwa sheria ya mitandao ambayo itadhibiti baadhi ya mambo, lakini tatizo kubwa lipo kwenye adhabu zinazoendana na sheria hiyo. 

“Sheria ni muhimu iwepo matumizi mabovu ya mtandao, hata hivyo adhabu zake ni kubwa kiasi kwamba hakuna Mtanzania wa kawaida, ambaye ndiye mtumiaji mkubwa wa mitandao hii, atakayemudu kulipa faini tajwa, vinginevyo mamia kwa maelfu wataishi gerezani,” alisema Maxence.

Akaongeza: “Sheria inapoeleza kwamba utalipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu, au kifungo kisichopungua miezi sita, tafsiri yake halisi ya kisheria ni kwamba unaweza ama kuhukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni hamsini au ukatumikia kifungo cha miaka 10 jela kwa sababu imeelezwa ‘isiyopungua’ na siyo ‘isiyozidi’.”

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu atakayepatikana na hatia ya kusambaza picha za ngono, matusi, uasherati atalipa faini isiyopungua Shs. 30 milioni au kutumikia kifungo kisichopungua miaka 10 au vyote. James Marenga, Mwanasheria kutoka taasisi ya kisheria ya Nola, akielezea Sheria ya Takwimu, alisema nayo itawapeleka wengi gerezani.

“Kwa mujibu wa sheria hii, hakuna takwimu ambazo zitatolewa bila idhini ya mamlaka husika, na endapo mtu atatenda kosa hilo ataingia matatani,” alisema Marenga, ambaye pia ni mwanahabari na wakili wa Mahakama Kuu.

Ni kutokana na udhaifu na ukandamizaji uliomo kwenye Sheria hiyo ya Makosa ya Mtandao ndiyo maana kampuni ya Jamii Media mapema mwaka huu 2016, ikaamua kufungua Mahakama Kuu Kesi ya Kikatiba kuipinga sheria hiyo ikitaka baadhi ya vifungu virekebishwe.

Wakati hukumu ya kesi hiyo ikiwa bado kutolewa, serikali kupitia Jeshi la Polisi ikaamua kumkamata Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo, na kumfungulia mashtaka kwamba amekiuka sheria hiyo ambayo anaipinga mahakamani na mshtakiwa mmojawapo likiwa Jeshi la Polisi. 

Siwezi kuzungumzia kwa undani kwa sababu tayari kesi hizi ziko kwenye mahakama za kisheria, lakini kimsingi ni kwamba, sheria hii kandamizi haiwezi kumuacha yeyote. Kumkamata Maxence na kumweka mahabusu kwa saa 144 bila dhamana ni dalili tosha kwamba mamlaka hazina mzaha licha ya ukweli kuwa ulimwengu wa sasa ni sawa na kijiji hasa katika zama hizi mpya za habari.

Leo hii kuna Watanzania milioni 23 ambao wanatumia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, JamiiForums, WhatsApp, Viber, Twitter, Instagram, Skype na kadhalika, ambao kwa sheria hii watalazimika kurudi kwenye zama za analojia kwa sababu hawako salama.

Nakumbuka wiki moja kabla Maxence hajakamatwa na polisi, aliwaeleza wanahabari na wamiliki wa blogu nchini wakati wa semina ya siku mbili: “Tujiandae kukamatwa na dola, kwa sababu Sheria ya Makosa ya Mtandao imewapa nguvu polisi, kuanzia mkuu wa kituo (mwenye cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi) kukukamata na kukufungulia mashtaka kama anaona – kwa mtazamo wake – taarifa uliyoichapisha inahatarisha usalama wa nchi.”

Akabainisha pia kwamba, kwa sheria hiyo, polisi wanaweza kukukamata na kukulazimisha uwape taarifa za vyanzo vyako vya habari.

Kwa hakika, jambo ambalo ni dhahiri linakwenda kinyume na taaluma ya habari pamoja na haki za binadamu, hususan uhuru wa kujieleza, kama inavyotamkwa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *