SIKU YA MAJI DUNIANI: Tusiruhusu madhila ya maji Cape Town yakaikumba Dar

Jamii Africa

Mara nyingi mgeni anapoingia mahali, imezoeleka kupokewa kwa shangwe na maneno mazuri ya kumkaribisha, ili ajisikie yuko salama na eneo salama.

Maneno yanayosikika kutoka kwa wenyeji ni “karibu, pole kwa safari” na mengine yanayofanana na hayo.

Hata hivyo, hali ni tofauti sana kwa wageni wanaoingia Cape Town, Afrika Kusini kwa sasa. Hawa hawapokelewi kwa maneno mazuri tena. Wanakumbana na maneno ya kuwaonya kuhusu matumizi ya maji.

Kila mahali, kuanzia ndani ya ndege kuelekea Cape Town, baada ya salamu, yanafuata maneno na kauli za kuonya wageni kwamba wasitumie maji hovyo. Maji hayatoshi.

Mgeni anaposhuka ndani ya ndege na kwenda maeneo ya wageni kujisajili, anakumbana na mabango yaliyojaa maneno hayohayo. Kwamba anakaribishwa, lakini asitumie maji hovyo.

Pembezoni mwa barabara, mabango yaliyosambaa ni kuhusu onyo kutumia maji. Hotelini na kila nyumba ya wageni, mapokezi ni “Cape Town hakuna maji ya kutosha, tumia kwa uangalifu.”

Fikra Pevu imeshuhudia kuwepo kwa matangazo ya aina hiyo ndani ya vyumba vya wageni na sehemu za maliwato.

“Cape Town, pamoja na uzuri na ukarimu wake kwa wageni, lakini inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, hivyo kuwa mwangalifu unapotumia maji; iwe kuoga, kupiga mswaki, kunawa na matumizi mengine muhimu ya maji,” yanasomeka baadhi ya matangazo hayo.

Meya wa Jiji la Cape Town, Patricia de Lille,  anasema kuwa kuanzia Aprili mwaka huu, wananchi watalazimika kupunguza matumizi ya maji kwa asilimia 40 na kuruhusu lita 50 tu kwa mtu mmoja kwa siku, wakati jiji hilo likikabiliana na hali mbaya zaidi ya ukame kuwahi kulikumba katika karne hii.

Ameonya kwamba endapo mvua hazitanyesha na jitihada za kupunguza matumizi ya maji hazitafanikiwa, basi usambazaji maji ya kawaida utafungwa.

Ikiwa hilo litatokea, basi wakazi wa Cape Town watalazimika kupanga foleni kwenye vituo vya mabomba ya maji ya umma kwa mgao ambapo kila mtu ataruhusiwa kupata lita 25 za maji kwa siku. 

Meya huyo amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kuwaeleza wananchi kutumia maji kwa uangalifu, lakini hali bado mbaya na hakuna matokeo mazuri katika hifadhi ya maji.

Jiji hilo ambalo huvutia mamilioni ya watalii kila mwaka, limeimarisha udhibiti mkubwa wa majitaka ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku umwagaji wa maji kwenye mabwawa ya manispaa na kuwapeleka mahakamani wamiliki wa nyumba wanaofuja maji.

Jiji la Cape Town lenye wakazi wanaoelezwa kukaribia milioni 4, linakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji tangu mwaka jana. Na hali inaendelea kuwa mbaya.

                   Cape Town huenda likawa jiji la kwanza duniani kukosa maji kabisa ifikapo mwishoni mwa Aprili 2018

Tatizo la maji Cape Town limeonesha kwamba majanga ya asili hayabagui taifa, rangi ya watu, hali zao matajiri au maskini. Wazungu na “weusi” wanaonekana wakipaga foleni kuteka maji katika mabomba ya umma.

Tayari vituo vya mabomba ya umma 200 vimetengwa na serikali ya jiji hilo kwa ajili ya kuukabili uhaba mkubwa wa maji uliopo sasa.

Kadri siku zinavyosonga, dalili za kunyesha mvua hazionekani kuwa karibu na jiji limetangaza kuwa mgawo utaweza kufikia hadi lita 5 kwa siku.

Cape Town huenda likawa jiji la kwanza duniani kukosa maji kabisa ifikapo mwishoni mwa Aprili 2018. Inaelezwa na uongozi wa jiji kuwa tarehe 29 ya mwezi huo, mabomba yote hayatakuwa na maji na mitambo ya kusukuma maji itazimwa.

Wataalamu wanaonya kwamba kama hatua sahihi dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi hazikuchukuliwa, basi miji mingi barani Afrika, itakumbwa na hali hiyo ya kukosa kabisa maji katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano ijayo.

Kutokana na hali hiyo, ni vyema sasa kila nchi ikajipanga kuhimiza matumizi bora ya maji na kulinda vyanzo vyake ili haya yanayotokea Cape Town sasa, yasitokee.

Pamoja na adha ya maji kuonekana kwa wenyeji, upungufu huo mkubwa wa maji Cape Twon, unaelezwa kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii. Jiji hilo linaloongoza kuwa na watalii wengi, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato.

Tayari hoteli za kitalii zimebandika matangazo yanayowataka wateja kutooga kwenye mabafu, wasioge maji ya bomba-rasharasha (shower) kwa muda mrefu, kubadilishiwa shuka lazima waombe, watumie maji kidogo kuswaki na kwamba maji ya mabwaya ya kuogelea (swimming pool), hayatabadishwa mara kwa mara.

Katika kuonesha ukali wa tatizo hilo la maji, wageni kutoka miji mingine wanaokwenda Cape Town kwa shughuli za michezo, mikutano na mambo mengine, wanatakiwa kubeba maji yao ya kunywa.

Inaripotiwa kwamba ukame unaolikumba jiji la Cape Town hivi sasa, haujawahi kutokea katika karne moja.

Sayansi ya tabia nchi inatabiri kwamba ikiwa tatizo la ukosefu wa maji katika eneo hilo utaendelea, basi hali hiyo itakuwa inajirudiarudia katika kila miaka 100 ijayo.

Uhaba wa maji ni tatizo la dunia. Kila mamlaka katika nchi mbalimbali, ikiwamo Tanzania, zinapaswa kuchukua hadhari na kuepusha jambo hilo lisitokee kwa kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji, kukinga na kuhifadhi maji ya mvua, kulinda vyanzo vya maji ya juu na chini ya ardhi na kuwa na matumizi bora endelevu ya umwagiliaji wa mashamba.

Yapo mengi ya kujifunza kutoka Cape Town kwa Tanzania, kwani taarifa zinaonesha, nchi hiyo ya ukanda wa Afrika Mashariki imekuwa na matumizi mabaya ya maji na kuruhusu kupotea kwa kiasi kikubwa cha maji yanaposafirishwa kwa matumizi ya umma.

Mamlaka za maji za miji ya Tanzania zimekuwa zikiripoti kupotea kwa kiasi kikubwa cha maji yanapokuwa akisafirishwa. Kwa Dar es Salaam pekee, zaidi ya asilimia 37 ya maji yanayosafirishwa hupotea njiani kabla ya kuwafikia watumiaji. Hali hii ni hatari. Tusiruhusu itokee.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *