Sinza: Vigogo wavamia maeneo ya wazi, Diwani wa CHADEMA awakamia

Jamii Africa

BAADHI ya maeneo ya wazi jijini Dar es Salaam, yamevamiwa na watu mbalimbali wakiwamo vigogo ndani ya serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM), FIKRA PEVU imefahamishwa.

Maeneo hayo yamevamiwa na kugeuzwa ya kibiashara na kuharibu kabisa malengo ya kutengwa kwake ikiwamo michezo na mikutano ya hadhara.

Diwani wa Kata ya Sinza Renatus Pamba, (CHADEMA) amesema atahakikisha kuwa jumla ya maeneo 18 ya wazi katika kata yake yaliyovamiwa na kujengwa yanaachwa huru.

Diwani huyo amesema baadhi ya watu wameyafanya ni sehemu ya kujinufaisha kibiashara. Amesema amesikitishwa sana kuona baadhi ya viongozi na wafanyabiashara wakubwa tena wenye nyadhifa wanadiriki kugawa na kujiuzia maeneo ya wazi bila kujali yametengwa kwa ajili ya shughuli maalumu.

“Nimegundua kuwa kuna baadhi ya watu wenye madaraka serikalini wameamua kuvamia maeneo hayo yaliyopo katika kata yangu sasa nina mkakati wa kuwatimua ili wapishe maeneo hayo kwa ajili ya shughuli za kijamii kama kuendesha mikutano au midahalo na viwanja vya michezo,

“Pia wanatumia maeneo hayo kwa ajili ya kuegesha magari yao wakati wa  usiku hii sio sahihi hata kidogo ni makosa makubwa kwani watoto wanakosa fursa ya kucheza kwa uhuru matokeo yake wanaenda vichochoroni na huko wanaweza kupata madhara makubwa kama kubakwa,” alisema Pamba.

sinza

Eneo la Sinza – Dar

Aidha aliwataka Madalali wa Sinza wanaotumiwa vibaya kwa kuuza maeneo ya wazi kuacha kabisa tabia hiyo kwani wanadanganywa na watu wachache kwa ajili ya kujinufaisha wao wenyewe ilimradi wakidhi matakwa yao na kudidimiza wananchi wenye kipato cha chini.

Pamba amesema kwa sasa anawaahidi wananchi wa Kata yake kuwajengea kituo kidogo cha polisi ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mali zao kwani vituo vilivyopo havitoshi ni vichache hivyo kushindwa kumudu matukio ya uhalifu kama wizi uliokithiri na kuvunjiwa nyumba unaotokea katika maeneo mbalimbali ya Sinza.

“Tayari ninavyo zungumza hapa nimeshapata eneo la kujenga kituo hicho hivyo ninachoomba ni ushirikiano wenu ili niweze kuanza ujenzi mapema kata yangu ina idadi kubwa ya watu hivyo vitendo vya uhalifu vinaongezeka watu kuibiwa na kuporwa mali hivyo inabidi vithibitiwe,” alisema Diwani.

Vile vile amelitaka Jeshi la Polisi kufanyakazi bila kuangalia chama, dini, wala kabila kwani imeonekana Chama cha CHADEMA kinapoomba kufanya mikutano ya hadhara huwa wanakataa kutoa kibali na visingizio visivyokuwa na maana.

“Sisi sote tunaimani na wananchi kwani hata mimi nipo hapa kwa ajili ya kuwatetea na kufanya jitihada ili maisha yawe bora kusiwe na ongezeko kubwa la wasio nacho,” alisema Pamba

Habari hii imeandikwa na Maneno Selanyika, FikraPevu Dar

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *