Mbunge Kiwia ampiga ‘stop’ mkandarasi

Sitta Tumma

MBUNGE wa Jimbo la Ilemela Jijini Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA), ameizuia kampuni ya Nyanza Roadworks ya jijini hapa, kujenga daraja la Bigibaiti lililopo Kilimahewa, baada ya kampuni hiyo kushindwa kutengeneza njia mbadala kwa ajili ya shughuli za kijamii katika eneo la mradi, kinyume cha mkataba.

Mbunge Kiwia (pichani), amefikia maamuzi hayo hii leo, baada kufanya ziara ya kushtukiza akiwa na jopo la waandishi wa habari katika mradi huo, ambapo wanahabari walijionea adha kubwa inayowapata wananchi yakiwemo magari ya abiria, mizigo na binafsi ambapo alimtaka Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli amwajibishe mara moja mkandarasi anayejenga daraja hilo lililopo katika mradi wa barabara ya lami kutoka Pasiansi, Kiloleli, Sanga hadi Nyakato Buzuruga, kwani ameonesha udhaifu mkubwa katika kusimamia mradi huo.

Alisema, mkandarasi huyo aliyepo chini ya kampuni ya Nyanza Roadworks ameonekana kukiuka kwa makusudi mkataba wa ujenzi wa mradi huo, na kwamba anajenga mradi huo kama anatoa msaada wakati amelipwa mamilioni ya fedha za Watanzania kujenga daraja la barabara hiyo, inayotarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 7.5, ikiwa ni ufadhili wa Benki ya Dunia (WB), kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania.

"Kuanzia sasa, ujenzi wa daraja hili nataka usimame hadi mkandarasi huyu atakapojenga barabara mbadala kwa ajili ya wananchi na magari. Kazi anayoifanya ni ya kihuni…maana ameziba njia kwa sababu ya ujenzi wa hili daraja, halafu hajatengeneza njia mbadala kwa ajili ya wananchi," alisema .

Mmoja wa wasimamizi wa mradi huo kutoka kampuni hiyo ya Nyanza Roadworks ambaye hakuweza kutaja jina lake, alikiri kuwepo kwa adha hiyo, ambapo alimweleza mbunge huyo kwamba, kampuni hiyo haijashindwa kujenga njia mbadala kwa ajili ya kupita magari na wananchi kwa ujumla, bali njia iliyojengwa bado inahitaji kuboreshwa zaidi, na kwamba njia hiyo mbadala lazima iwepo.

Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza

2 Comments
  • Ndugu Kiwia,simamia masilahi ya wana Nchi ndiyo sera ya chama chako,kwa hiyo sikupongezi bali nasema hii ndiyo sehemu ya majukumu ambayo watanzania wanategemea usimamie kwa umakini zaidi,Hamia na ziwani,mapato ya jiji,kirumba n.k.

  • Razima tuwafundishe sheria na utaratibu, wamezoea kuchakachua haki za raia walionyimwa elimu ya kuwakomboa. bali hupigwa msasa tu, ndo maana wasomi hawana thamani (digrii=300000@month ni aibu kwa taifa la ujamaa)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *