Songea: Watumia dawa za kulevya waongoza kwa maambukizi ya UKIMWI

Jamii Africa

MADHARA ya kutumia dawa za kulevya ni mengi. Na yote ni mabaya. Hakuna jema hata moja.

Wanaotumia dawa hizo, ikiwamo Cocaine, Heroine, bangi na nyingine, hupata hasara ya mwili kukosa nguvu, hivyo kushindwa kufanya kazi, kuugua magonjwa ya akili na madhara mengine ya kiafya.

Miongoni mwa magonjwa yanayowakumba wanaotumia dawa hizo ni Ukimwi. Huu ni ugonjwa usiokuwa na tiba wala chanjo hadi sasa.

Wakati serikali inaongeza nguvu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, utafiti umebaini  katika Manispaa ya Songea, Ruvuma, watu wanaotumia dawa za kulevya wanaongoza kwa maambukizi ya UKimwi.

Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu kwa wiki mbili, umebaini makundi ya watumiaji dawa za kulevya sasa yanaongoza kwa kiwango kikubwa cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Hii ni asilimia 36 ya watu hawa wanaotumia dawa za kulevya, sawa na watu 36 kwa kila watu 100 wana virusi vya Ukimwi.

Hata hivyo, kiwango cha maambukizo cha watu wa kawaida ni asilimia tano; sawa na watu watano wana Ukimwi kwa kila watu 100.

Mratibu wa UKIMWI na tiba katika Manispaa ya Songea Dk. Felista Kibena anayataja makundi hayo kuwa  watu wanaofanya biashara ya ngono, wanaofanya ngono  ya jinsia moja na watu wanaojidunga sindano na wale wanaotumia dawa za kulevya.

“Maambukizo ya virusi vya Ukimwi yanachangiwa na watu wanaofanya ngono kinyume cha maumbile,watu wanaofanya biashara ya ngono, wafungwa na watumiaji dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano au kubwia,’ anasema.

Kibena anasema kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wa dawa za kulevya, idara yake imeamua kutoa elimu ya ukweli kuhusu Ukimwi katika makundi hayo baada ya tatizo kuongezeka kwa kasi.

Hata hivyo, anasema tayari watumia unga  wapatao 80 katika Manispaa ya Songea wamejitokeza kupata mafunzo maalum ya kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

FikraPevu imeshuhudia watumia dawa za kulevya na wanaofanya biashara ya ngono  wakipata mafunzo hayo ambapo mada mbalimbali zilitolewa, ikiwemo ukweli kuhusu virusi vya Ukimwi(VVU) na Ukimwi, matumizi sahihi ya kondom ya kike na kiume na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.

Kibena amezitaja njia kuu ambazo zinaongoza kwa kusababisha maambukizi mapya ya Ukimwi kuwa ni  kupitia ngono isiyo salama, kutoka kwa mama aliyeambukizwa kwenda kwa mtoto, maambukizi wakati wa kunyonyesha maziwa ya mama na Kupitia utiaji wa damu na bidhaa za damu zilizosibika.

Njia nyingine anaitaja kuwa ni kupitia sindano zilizoambukizwa kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya sindano, kupitia njia ya ulawiti na kupitia uchangiaji wa vifaa vya kuchanjia au kudungia, wakati wa tohara au uchanjaji chale.

Mtaalamu huyo wa afya amewaasa watumiaji dawa za kulevya kuacha tabia ya kujidunga sindano kwa kuchangia sindano moja hali ambayo inaongeza maambukizo mapya na kwamba waanze mchakato wa kuacha kabisa matumizi ya dawa za kulevya.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa matumizi ya dawa za kulevya hasa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 45, bado ni tatizo kubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Takwimu zilizopo katika Manispaa hiyo zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 manispaa hiyo ilikuwa na waathirika wa dawa za kulevya 145, kati ya hao – wanaume ni 138 na Wanawake ni saba.

Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei, 2016 Manispaa ya Songea ilikuwa na jumla ya waathirika wa dawa za kulevya 97,  kati yao wanawake wawili na wanaume  95 ambapo waathirika wote wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 45.

“Natoa rai ya kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kujenga  jamii na maisha na utu wa mtu bila matumizi ya dawa za kulevya tatizo linalowakabili vijana wengi katika nchi nzima,’’ anasisitiza Dk. Kibena.

Takwimu zinaonesha kuwa katika Manispaa ya Songea zaidi ya watu 21,000, wanaishi na virusi vya Ukimwi, ambapo watu zaidi ya 10,000 ndiyo katika manispaa hiyo wanaugua ugonjwa wa Ukimwi.

Dk. Kibena amezitaja kata ambazo zinaongoza kwa maambukizo ya virusi vya Ukimwi katika Manispaa ya Songea kuwa ni Bombambili, Mateka, Ruvuma na Lilambo ambapo maambukizi ya virusi hivyo ni asilimia nne.

Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya tano kitaifa ukiwa na maambukizi ya asilimia saba, ambapo mkoa wa Njombe ndiyo unaongoza kitaifa ukiwa na asilimia  14.5, nafasi ya pili inashika na Mkoa wa Iringa, ikifuatiwa na Mkoa wa Mbeya kwa nafasi ya tatu na Mkoa wa Rukwa ukiwa nafasi ya tano.

Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2013 hapa nchini, watu milioni moja na nusu walikuwa wanaishi na virusi ambapo kwa mwaka 2014 pekee takwimu zinaonesha kuwa katika Tanzania watu 74,000 wameambukizwa virusi na zaidi ya watu laki tano walikuwa wanatumia dawa za ARV.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani  (WHO) watu milioni 35 wanaishi na virusi vya Ukimwi hadi kufikia mwaka 2013 kati yao  watu milioni 24 sawa na asilimia 71 walitoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ambapo watu milioni moja na nusu wamekufa hadi kufikia mwaka 2013 na watu milioni 12 wanatumia dawa za ARV.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *