‘Stiegler’s Gorge’ na malumbano ya kumaliza tatizo la umeme nchini

Jamii Africa

Benki ya Dunia imesema wananchi milioni 600 hawana umeme kuendesha shughuli zao za maendeleo hali inayokwamisha ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Siku chache zilizopita, Benki ya Dunia imeziboresha takwimu zake za mwaka 2014 kuhusu upatikanaji wa umeme katika nchi za Afrika  na imebaini kuwa jitihada zaidi na uwekezaji unahitajika kwenye sekta ya nishati ili kuwanusuru wananchi wengi wanaokaa gizani.

Takwimu za benki hiyo za mwaka 2014 zinaeleza kuwa watu milioni 600 hawana umeme. Pia imebaini kuwa hadi kufikia 2016 idadi hiyo ya watu wasio na umeme haijapungua wala kuongezeka.

 

Kwa miaka miwili mfululizo tangu 2014 hadi 2016, idadi ya watu ambao hawakuunganishwa kwenye gridi ya taifa ya umeme ilipungua.  Kiuhalisia katika kipindi hicho umeme uliwafikia watu wengine milioni 76 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 5 ya upatikanaji wote wa umeme unaofikia 43%.

Idadi ya watu waoishi bila kuwa na umeme imepungua kwa watu milioni 21 huku takwimu halisi zikionyesha watu milioni 600 hawana umeme.

Lakini zipo dalili za kutia moyo. Asilimia 60 ya wateja waliounganishiwa umeme walikuwa ni wananchi wa vijijini, ambako upatikanaji wa umeme ni changamoto.

Katika kipindi hicho, uunganishaji wa umeme katika maeneo ya mjini uliongezeka kutoka 72% hadi 74% huku vijijini ukiongezeka kutoka 16% hadi 23%. Kuna hatua imepigwa katika maeneo ya vijijini lakini bado hali siyo ya kuridhisha.

 

Hiyo ina maanisha nini?

Sekta ya umeme bado haijasimama imara. Takwimu za Benki ya Dunia zinathibitisha wazi kuwa  upatikanaji wa nishati ya umeme bado ni mgumu na ghali hasa maeneo ya vijini ambako asilimia 60 ya wakazi wanaishi bila ya umeme wa uhakika.

Nchini Tanzania, Upatikanaji wa umeme kitaifa umeongezeka kwa asilimia 21 kutoka mwaka 2006 hadi 2016 lakini umebaki chini ya 30% ya kiwango kinachohitajika.

Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) imeeleza katika taarifa yake ya mwaka 2017 kuwa bado idadi kubwa ya watanzania hawajafikiwa na nishati ya umeme huku mahitaji ya nishati hiyo yakiongezeka kwa kasi.

“Asilimia 70 ya watanzania bado wanaishi bila umeme na mahitaji ya nishati hiyo yanaongezeka kwa kasi”, imeeleza taarifa hiyo iliyojikita kuelezea juhudi za pamoja za wadau wa maendeleo katika kukuza uchumi wa wananchi wa vijijini kwa kuwaunganishia nishati ya umeme katika shughuli zao za uzalishaji mali.

Kwa tafsiri ya kawaida ni kwamba watanzania 7 kati ya 10 hawana huduma ya umeme katika nyumba zao. Kwa muktadha huo umasikini unaowazunguka unaweza kusababishwa na ukosefu wa umeme wa uhakika.

 

Mikakati ya serikali

Benki ya AfDB kwa kushirikiana na Tanzania zimeingia kwenye mazungumzo ya kuikopesha serikali mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 165 kwa ajili ya kujenga bwawa la kuzalisha umeme katika ukanda wa Kaskazini Magharibi mwa nchi  kwenye maporomoko ya maji ya  Stiegler Gorge ndani ya Mto Rufiji.

Kulingana na matokeo ya utafiti uliofanywa na  Shirika la Kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (RUBADA)  yalionyesha kuwa mpalio wa Stiegler’s Gorge una uwezo wa kuhimili mitambo mitatu mikubwa ya kuzalisha umeme.

Mtambo wa kwanza ukizalisha megawati 400 ambao ungefungwa upande wa Kaskazini mwa bwawa, mtambo wa pili ungekuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 800, ambao ungefungwa upande wa chini ya bwawa, na mtambo wa tatu  wenye uwezo wa kuzalisha megawati 900 ambao ungefungwa upande wa kusini mwa bwawa.

Kwa ufupi, jumla ya megawati 2,100 zingezalishwa kutoka Stiegler’s Gorge; kiasi ambacho ni karibu ya mara mbili ya kinachohitajiwa na Tanzania.

Upatikanaji wa umeme wa uhakika ni lengo la saba la Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo Tanzania imeridhia ya kuyatekeleza ifikapo 2030. Serikali imeshauriwa kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye sekta ya nishati ya umeme ili kuharakisha ujenzi wa uchumi wa viwanda na kati ifikapo 2025.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *