TAHADHARI: Waishio jirani na viwanda Dar hatarini kupata magonjwa ya kudumu

Aisi Sobo

Wananchi wanaoishi jirani wa viwanda jijini Dar es Salaam wapo hatarini kupata magonjwa  ya mfumo wa upumuaji, ngozi na kansa kutokana na kuvuta vumbi, moshi na harufu inayosemekana kuwa na kemikali zenye sumu inayotoka kwenye viwanda hivyo.

Mtaalam wa magonjwa yatokanayo na kazi, kutoka hospitali ya  Taifa ya  Muhimbili  (MNH), Hussein Mwanga anathibitisha kuwepo kwa athari za muda mfupi na mrefu kutokana na kuvuta vumbi na hewa iliyochanganyika na kemikali kutoka viwandani.

Vipo viwanda vingi jijini Dar es salaam lakini mwandishi wa habari hizi alielekeza uchunguzi wake katika viwanda vitatu; kiwanda cha saruji Camel kilichopo Mbagala, Kiwanda cha kuchakata Gesi cha Salima Oxygen kilichopo Mbagala na kiwanda cha sabuni ya unga cha Royal kilichopo Mabibo.

Wananchi wanaoishi pembezoni na viwanda hivyo wamelalamika kuwepo kwa madhara ya kiafya kutokana na kuishi maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuugua mafua na vikohozi vya mara kwa mara.

 

Naye Dkt. Elisha Osati,  Mtaalamu wa magonjwa ya ndani ya mwili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anasema kuwa mtu anayevuta hewa iliyochanganyika na vumbi lenye kemikali anauwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya njia ya hewa yasiyokuwa na tiba.

Pamoja na maelezo hayo kutoka kwa wataalam, takwimu zilizopatikana kutoka kwenye Hospitali ya serikali ya Zakhem iliyopo jirani na eneo la viwanda Mbagala zimeonesha kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka 2017 kutoka Januari hadi June.

 

                  Wagonjwa wa mfumo wa hewa waliotibiwa katika hospitali ya serikali ya                     Zakhem – Mbagala (Januari hadi Juni 2017) 

Hata hivyo  uchunguzi huu haukuweza kuthibitisha kuwa wagonjwa wote waliopata maradhi hayo ni kutokana na kuishi karibu na viwanda  hivyo vinavyatoa moshi unaosemekana kuwa na kemikali hatarishi kwa afya za binadamu.

 

Umbali wa Kiwanda na makazi

Sheria ya Afya ya Umma ya mwaka 2009 kifungu cha 84(1)  inazitaka Halmashauri za Miji kuhakikisha ujenzi na shughuli za viwanda vinavyozalisha vumbi na gesi taka vinajengwa mbali na makazi ya watu. Lakini sheria hiyo haijasema ni umbali gani unaopaswa kuwepo kati ya makazi ya watu na viwanda.    

Pamoja na mapungufu hayo katika sheria, mwaka 2011 Serikali ilipitisha kanuni za Mipango Miji kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji sura namba 355 chini ya kifungu cha 77(1) kuhusu utaratibu wa ujenzi, vipimo na viwango vya nafasi za majengo pamoja na viwanda.

Wakati sheria inavitaka viwanda kujengwa mbali na yalipo makazi, uchunguzi umebaini kuwa  kiwanda cha sabuni ya unga cha Royal kipo mita tatu kutoka makazi ya watu, kiwanda cha Salima Oxygen kipo mita 10 kutoka makazi ya watu na kiwanda cha saruji Camel kipo umbali wa mita 50 kutoka makazi ya watu.

Baada ya kujiridhisha kuwa viwanda hivyo viko karibu na makazi ya watu na vinaathiri afya zao, Mwandishi wa makala haya  aliwatafuta wahusika wa viwanda hivyo ili   kujua undani wa suala hilo.

Akijibu malalamiko kuhusiana na kiwanda kutoa vumbi lenye sabuni Meneja Uendeshaji wa kiwanda cha Royal,  Ntunta Shallanda amekiri kuna wakati mitambo hupata hitilafu na kusababisha vumbi jepesi la sabuni kufika katika makazi ya watu.

“Yapo malalamiko kuhusu vumbi lakini huwa tunajitahidi kufanya marekebisho, tunatambua kuwa hakuna kemikali isiyoleta madhara kwa binadamu hivyo huwa tunachukua tahadhari za kutosha ili kuwalinda.” ameeleza Shallanda.

Hata hivyo, Meneja Rasilimali watu wa kiwanda cha saruji Camel amekanusha kuwepo kwa malalamiko yoyote ya wananchi juu ya kiwanda chao kutoa vumbi na kuleta madhara kwa wakazi.

                                                                                          Kiwanda cha saruji camel mbagala

 

Naye Meneja Mkuu kiwanda cha Salima Oxygen, Damas Mkenda amekanusha kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wakazi waliopo jirani na kiwanda hicho na kulingana na sheria  kipo katika eneo sahihi.

“Hakuna harufu inayotoka katika kiwanda chetu kufika kwa wananchi na hatujawahi kupata malalamiko yoyote na hata wafanyakazi wetu wanafahamu namna ya kujikinga na majanga ikiwa ni pamoja na moto” amesema Mkenda

 

Kauli kutoka serikalini

 Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira,  January Makamba ameitaja Idara za Mipango Miji kuruhusu viwanda kujengwa katika makazi na kusababisha migogoro ya uchafuzi wa mazingira na afya za watu.

Amezitaka mamlaka husika kuzingatia sheria na kuhakikisha shughuli za viwanda hazihatarishi afya za wananchi wanaoishi jirani na viwanda.

 Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Mbagala, Jumanne Kambangwa amesema uwepo wa kauli za ulaghai kutoka kwa mmiliki wa kiwanda cha saruji Camel kuwa ndio chanzo cha kuwepo kwa athari za kiafya zinazoendelea kuwapata wananchi wa eneo hilo.

“Kabla ya kiwanda kuanzishwa walituambia kuwa kingekuwa na teknolojia kutoka China ya kuzuia vumbi na wakawachukua baadhi ya viongozi lakini kabla hawajarudi kutoka china kiwanda kikaanza kufanyakazi na tangu wakati huo mpaka leo hakuna unafuu wa vumbi” anaelezea Diwani Kambangwa.

Uongozi wa serikali za mitaa ambako viwanda vipo wamethibitisha  kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi huku wakizishutumu mamlaka za juu kuwapuuza pale wanapopeleka malalamiko yao.

Afisa Afya wa kata ya Mbagala, Anna Mushi amekanusha kuwepo kwa malalamiko ya wananchi kuhusiana na vumbi litokanalo na kiwanda cha saruji Camel na kwamba hajawahi kuona wala kusikia adha ya vumbi kutoka kiwanda hicho.

Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba baada ya kufanya mahojiano na mwandishi wa makala haya ofisini kwake.

Suluhisho

Jamal Juma, Mwanasheria wa  timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) amethibitisha kuwepo kwa mapungufu katika sheria na sera kwa kukosekana mahali ambapo imetamkwa umbali wa kuachwa kutoka kilipo kiwanda na makazi ya watu.

Amezitaka mamlaka za serikali kuzifanyia marekebisho sheria za mipango miji ili kuokoa afya za wananchi wanaoishi karibu na viwanda hivyo, ikiwemo kutamka ni umbali gani unatakiwa kuwepo.

Hata hivyo, amehimiza kujenga nyumba kwa kuzingatia mipango miji na kuhakikisha shughuli zote za viwanda haziingiliani na makazi ya watu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *