Tahariri: Watanzania tutume SMS kwa watawala kuhusu Mgomo

Jamii Africa

Katika demokrasia ya kweli wananchi ndio wenye sauti ya mwisho. Siyo wanasiasa, siyo majeshi, siyo wataalamu au kikundi kimoja cha watu. Huu ndio msingi wa kweli wa demokrasia. Na katika demokrasia hiyo ni vyombo vya habari huru vinavyoweza kuwakilisha maoni ya wananchi  hao na kuwa vipaza sauti vya wananchi hao.

Tunaamini hadi hivi sasa hakuna chombo cha habari ambacho kimeweza kweli kuakisi sauti za Watanzania kufuatia mgomo wa madaktari ulivyoanza na baadhi ya vyombo ambavyo viliaminiwa kuwa ni vya “umma” vimegeuka kuwa vyombo vya kuharibu habari vikifanya kwa makusudi upoteshaji ili kutoifanya serikali ionekane vibaya. Tunaamini msimamo wa vyombo hivyo wa kuwa walinzi wa serikali na watetezi wa watawala unafanya vyombo hivyo kupoteza hadhi yao ya kuwa vyombo vya kupasha habari na kugeuka kuwa kuwa vyombo vya kutengeneza habari.

Na kwa vile katika demokrasia vyombo vya habari kupitia tahariri zake vinaruhusiwa kuchukua msimamo rasmi tunaamini wakati umefika kwa Fikra Pevu kuchukua msimamo katika suala la mgomo huu tukiamini kuwa tunawakilisha hisia, matamanio na fikra za Watanzania wengi. Hatudai hata kidogo kuwa tunawakilisha maoni ya kila Mtanzania. Tangu mgomo uanze tumetoa taarifa sahihi za wazi na bila kujaribu kuzipamba kuhusiana na mgomo huu. Lakini sasa tunaamini yatupasa tuchukue msimamo thabiti ambao tunaweza kuusimamia.

Mgomo huu ni fedheha na aibu ya serikali. Kushindwa kupatia ufumbuzi wa msingi wa madai ya madaktari kwa sababu tu kwa kufanya hivyo kutawapa madaktari nguvu na hata kuweza kuchochea wengine wagome ni udhaifu mkubwa wa uongozi wetu. Madai ya msingi ya madaktari na malalamiko yao dhidi ya viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yalipaswa kupewa umakini mkubwa na kushughulikiwa mara moja. Hata hivyo, katika hali inayoonesha kutegeana, kutokuwajibika na kulindana serikali imeendelea kusubiri kwa kutaka madaktari waoneshe wanaiheshimu na kuiogopa.

Huu ndio msingi wa hotuba ya Waziri Mkuu na baadaye uamuzi wake wa kwenda mahali ambapo alikuwa anajua madaktari hawapo ili tu kuwaonesha kuwa hawakuja na hawakumuonesha “heshima”. Waziri Mkuu na serikali imeanza kuwa kama ya kifalme ambapo mfalme akenda basi watu wake nao wapaswa kwenda. Katika demokrasia wananchi wanayo haki ya kukataa kukutana na kiongozi yeyote kama kwa kufanya hivyo wanaamini watakuwa wanajiweka matatani au hata kujichongea. Madaktari walitoa pendekezo mapema la kumuomba Waziri Mkuu kukutana naye Jumapili lakini kwa dharau pendekezo lao likapuuzwa na uamuzi wa kamatakamata na lazimisha ukafanyika. Tunaamini huu ni ukosefu wa hekima kwa viongozi wa serikali yetu.

Hivyo basi, tunaamini mgomo huu unaweza kumalizwa mara moja endapo serikali itaonesha kuyapa uzito madai ya madaktari. Kitendo cha Waziri wa Afya ambaye anatuhumiwa na madaktari kusababisha mgomo huo kuendelea kuzungumza kwa mamlaka ni dharau ya wazi kwa hoja za madaktari. Dr. Mponda Hadji anapaswa kujiuzulu ili Waziri mwinge aweze kuzungumza kwa niaba ya Wizara. Katibu Mkuu Bi. Blandina Nyoni naye anapaswa kuondoka kwa kushindwa kuonesha uongozi katika sakata hili huku akiweka dharau yake kwa madaktari wanaolalamika wazi. Na pamoja na hao wawili ni Mganga Mkuu wa taifa Dr. Deo Mtasiwa ambaye naye ameendelea kulalamikiwa siyo katika sakata hili tu bali pia masuala mengine ya kashfa huko nyuma. Hawa watatu wanatakiwa wajiuzulu mara moja au kufukuzwa kazi ili mazungumzo yaweze kuanza ya madai mengine ya Madaktari.

Uongozi wa madaktari walio katika mgomo kwa upande wao wawe tayari mara moja kutoa agizo la madaktari wote kurudi kazini mara tu viongozi hao watatu watakapojizulu au kufukuzwa. Na kutoka hapo uongozi wao upange mpango wa mazungumzo na serikali ya hoja zao nyingine mbalimbali wakiwa kazini na kwa kupitia wawakilishi wao. Serikali isipange wala kuchukua hatua zozote za kulipiza kisasi dhidi ya madaktari waliogoma au viongozi wao. Mazungumzo hayo na serikali yawe yamefikia mwisho na makubaliano kuwekwa wazi ndani ya miezi mitatu ili matokeo yake yaweze kuingizwa kwenye bajeti ijayo.

Ili hili lifikiwe Watanzania wanapaswa kupaza sauti zao kwa watawala wao ili wajue kilio na matamanio yao. Ni kwa sababu hiyo sisi kama chombo cha habari tunatoa wito kwa Watanzania wote wanaoataka mgomo huu ufikie hatima yake mapema zaidi kutuma ujumbe wa SMS kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Bw. Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu wa Muungano Bw. Mizengo Pinda pamoja na Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi. Anna Makinda. Ujumbe huu mfupi utumwe kwao bila kuweka maneno mengine ya hisia, kejeli au dharau. Ujumbe uwe wazi kile ambacho Wananchi wanakitaka.

“Mhe.(weka jina la unayemtumia) .. mimi kama Mtanzania nimechukizwa na kitendo cha serikali kushindwa kutatua kwa haraka mgomo wa madaktari unaondelea. Nakusihi utumie uwezo wako wote kuhakikisha kuwa mgomo unamalizwa kwa njia ya staa, heshima na utu ili kuhakikisha madaktari wetu wanarudi kufanya kazi mara moja, maslahi yao yakilindwa na uongozi wa Wizara ukiwajibishwa kwa mgomo huu. Asante”.

Namba za simu:

Rais Kikwete: 754 777775.

Waziri Mkuu Pinda: 754 301 630

Spika Anna Makinda: 754 465226

Tunaamini kuwa bila wananchi kuwafanya watawala wetu wajue hisia zetu ndivyo hivyo wao hutenda bila kuzingatia sana wnanchi wanahisi nini. Katika demokrasia hakuna hatari kubwa kama wananchi wasiowaambia watawala wao ukweli wa maisha yao. Watanzania tuwatumie ujumbe au hata kuwapigia simu wajue mgomo huu umetokana na wao kushindwa kuongozi.

MHARIRI

3 Comments
  • Nadhani serikali imekosea sana na imeonesha kutojali maisha ya watanzania. Kilichonishtua zaidi ni pale waziri mkuu alipoyakataa madai ya madaktari then kesho yake anauambia uma Raisi kaongeza posho za wabunge. Hii ni dharau kwani hajaonesha dhamira ya dhati kutatua changamoto hii ya afya badala yake ameona maslahi ya wabunge ni muhimu zaidi labda kwa kuwa naye ni mbunge

  • Wahariri wengi wamewekwa mfukoni na serikari.Hawawezi kufanya lolote dhidi ya serikari kipofu kwasababu wameamua makusudi kuweka blanketi machoni mwao ili wasione uovu wowote wa serikari.Inauma sana .

  • Inauma na inackitisha sana tena saana kuona kiongoz mkuu wa selikali km wazili mkuu kuona hakugusi wala hashtushwi na maumiv na cmanz za watanzania tunaopoteza ndugu wazaz hasa tegemez wa familia zetu mahospitalin inauma inackisha nahata kutukatisha tamaa na selikali yetu ok mungu atatufikisha pale wanapotaka ila naamin watanzania tomechoka kwahili mwisho unakalibia,, ok tunawashukur viongoz wetu nafkir hichi ndicho mnachokiongoza,,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *