ASASI ya TCSD inayojishughulisha na uangalizi wa miradi inayotekelezwa na LVEMP II, imesema zaidi ya tani 40 za uchafu huwa zinamwagwa kila mwaka katika bonde la Ziwa Victoria, jambo linalohatarisha maisha ya wananchi wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, zinazotegemea maji ya bonde hilo.
Kulinana na hali hiyo, imeelezwa kwamba zaidi ya watu milioni 150 wa ukanda wa nchi hizo za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda wanaotegemea maji hayo ya bonde la Ziwa Victoria, wapo hatarini kuathiriwa na uchafu huo iwapo mikakati thabiti na endelevu haitachukuliwa kwa haraka.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini Magu mkoani Mwanza, na Mratibu wa Asasi hiyo ya TCSD, Dk. Sam Kasulwa wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha robo mwaka cha wadau wa LVEMP, kilichowashirikisha maofisa watendaji wa kata, vijiji amoja na wenyeviti wa vijiji wilayani humo, kilichofanyika ukumbi wa Uwama Magu mjini.
Alisema, takwimu za kitaalamu zinaonesha kwamba, upo ulazima wa jamii ya wilaya hiyo ya Magu na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kushirikiana pamoja kupiga vita uchafuzi wa mazingira katika bonde hilo la Ziwa Victoria, na kwamba kufanya hivyo ni kwenda sambamba na sera zilizoridhiwa Kimataifa katika kutokomeza uchafuzi huo wa mazingira.
Kwa mujibu wa mratibu huyo wa TCSD, Dk. Kisulwa, uchafuzi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya watu katika wilaya ya Magu na kwingineko nchini ni chanzo kikuu kinachosababisha kupungua kwa hewa ya Oksijeni, hivyo kuhaliru mazalia ya samaki na kusababisha rasilimali hiyo kuanza kupungua tofauti ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Taarifa za kitaalamu zinaonesha kwamba, kila mwaka zaidi ya tani 40 za uchafu humwagwa ndani ya bonde hili la Ziwa Victoria. Hii ni hatari sana kwa maisha ya watu wa nchi zinazotegemea maji ya bonde hili.
“Waathirika wakubwa katika hili ni nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Maana inakadiriwa kuna zaidi ya watu milioni 150 wanategemea maji ya bonde hili…kwa hiyo lazima tushirikiane kwa pamoja kusimamia miradi ya LVEMP kwa kukomesha uchafuzi wa mazingira”, alisema mratibu huyo wa Asasi ya TCSD, Dk. Kisulwa.
Hata hivyo, Dk. Kisulwa aliwaomba viongozi wa Serikali, taasisi, mashirika, makampuni pamoja na wananchi wa wilaya ya Magu kushirikiana pamoja katika kutekeleza miradi inayoratibiwa na LVEMP na kusimamiwa na sasi yake hiyo ya TCSD, kudhibiti kabisa uchafuzi mkubwa wa mazingira katika bonde la mto Simiyu na Ziwa Victoria.
Alisema, hivi sasa yametokea mabadiliko ya tabia nchi yanayozikumba karibu nchi zote duniani, na kwamba athari hiyo inatokana na hewa na ukanda wa ozon kuharibiwa vikali na kemikali za uchafu zinazozalishwa kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira unaofanywa na binadamu vikiwemo viwanda katika mataifa mbali mbali yaliyoendelea na yanayoendelea duniani.
Kwa upande wake, ofisa utawala na fedha wa Asasi hiyo ya TCSD iliyopewa na Serikali ya Tanzania jukumu la kusimamia na kufuatilia utekelezwaji wa miradi ya LVEMP II, Godwin Kalokola alisema: “Mradi huu utafanya kazi zake kwa muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka huu. Tutatekeleza sera ya mabadiliko ya tabianchi ya Afrika Mashariki ya mwaka 2010”.
Alisema, Asasi hiyo itahakikisha inasimamia, kufuatilia na kutetea uhalisia wa matokeo yanayotarajiwa kufikiwa na LVEMP II, na kwamba utendaji kazi wa asasi hiyo ya TCSD utajikita zaidi katika ngazi ya kanda kwa kushirikiana na tume ya bonde la Ziwa Victoria, ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa na LVEMP II ifnafanyika kwa wakati uliopangwa.
“Ili kufanikisha hayo, mradi pia utaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbali mbali, vikiwemo vyombo vya habari, ili kusaidia uibuaji wa miradi na kuiandaa jamii yetu iweze kufaidika na miradi yote inayotekelezwa na LVEMP chini ya usimamizi wa TCSD”, alisema ofisa utawala na fedha huyo wa TCSD, Kalokola.
Naye ofisa utawala wa TCSD, Careen Maisala aliyataja baadhi ya matokeo yanayotarajiwa katika usimamizi wa mradi huo kwamba kuwa ni kanuni za kisheria, ukusanyaji na kubadilishana taarifa, usimamizi endelevu wa ardhi, kupunguza mmomonyoko wa udongo, usimamizi wa maliasili unaoongozwa na jamii.
Matokeo mengine ni kusimamia kilimo kinachozingatia matumizi bora na endelevu ya ardhi, kupunguza vyanzo vya uchafuzi wa mazingira katika bonde zima la Ziwa Victoria, kukusanya takwimu na ushuhuda kwenye familia juu ya matokeo ya utekelezwaji wa miradi ya LVEMP II inayoongeza vipato vya kiuchumi.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza.