Tanzania bado imelala kuhusu madhara ya taka za kielektroniki

Jamii Africa

SERIKALI Kuu imekaa kimya. Haijasikika wala kuonekana ikichukua hatua kuzuia kutupwa hovyo kwa takataka zinazotokana na vifaa vya kielektroniki.

Inawezekana kabisa kuwa serikali inapuuza kuchukua hatua kwa kuwa hazionekani kuwa nyingi. Kila mtu anatupa bidhaa hizo bila kufuata taratibu. Na hata serikali yenyewe inaweza kuwa inatupa vifaa hivyo vilivyokwisha muda wake.

Watu wanakusanya mabaki ya bidhaa hizo na kuzitupa kwenye vyanzo vya maji. Wanatupa kwenye majalala zikiwa zimechanganywa na takataka zingine; ngumu na laini.

Bidhaa zinazozungumzwa hapa ni pamoja na kompyuta mbovu na vifaa vyake vingine, simu za mkononi na mezani, vifaa vya michezo vya kielektoniki na zingine zinazofanana na hizo.

Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu umebaini kuwa Mfuko wa Taifa wa Mazingira hadi sasa haujaanzishwa licha ya kuelezwa na sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kwamba uanzishwe ili kuwa msimamizi mkuu wa masuala kama haya ya takataka na namna bora ya kuzutumia au kuziteketeza.

Kwa miaka 13, hadi sasa serikali imekuwa ikishindwa kuutengea fedha ili uanzishwe kwani ndiyo, sheria inataka, uwe msimamizi mkuu wa masuala ya mazingira.

FikraPevu imegundua kuwa kwa bajeti ya mwaka 2016/17, mfuko huo uliombwewa shilingi bilioni 100. Lakini hadi sasa haujaanzishwa.

“Hatuna fedha za kutosha, hatuwezi kufanya kazi zetu ipasavyo, ni kama tumesimama, tunaandika tu ripoti ambazo hazikamiliki vyema kwa kuwa hatuwezi kwenda kwenye maeneo yanayotuhusu,” anasema mmoja wa maofisa wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, akilalamikia ufinyu wa bajeti ya wizara, seuse kuanzishwa mfuko.

Waziri wa wizara hiyo, January Makamba alipoulizwa na FikraPevu juu ya hili alisema apewe muda kidogo ili atoe majibu. Tunasubiri.

Taarifa zinaeleza kuwa ongezeko kubwa la matumizi ya vifaa vya kielectroniki katika nchi ya Tanzania, ambavyo baada ya muda wake kuisha au kuharibika, hutupwa hovyo.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa vifaa vingi vya Kielectroniki huwahi kuharibika kutokana na kuwa na ubora hafifu.

Akizungumza na FikraPevu Alex Katanda, fundi kompyuta na mfanyabiashara katika Kariakoo, Dar es Salaam, anasema kuwa mabaki ya kielectroniki yameongezeka katika eneo hilo analofanyia biashara.

Alex anasema sababu kubwa ya ongezeko hilo ni kuuzwa kwa bidhaa zilizotumika kutoka nje ya nchi ambazo huwalazimisha wauzaji wake kuziacha baada ya kukaa muda mrefu bila wateja na kuharibika.

“Vifaa hivyo hata vikinunuliwa, hurudishwa kwa mafundi wa eneo la Kariakoo kwa ajili ya kutengenezwa, lakini napo hushindwa kutengenezwa na kufanya kazi, hivyo vikikaa sana wahusika huvitupa tu,” anaongeza.

FikraPevu imebaini mrundikano mkubwa wa vifaa vibovu katika maduka ya kompyuta na  simu yaliyopo Mtaa wa Aggrey, Dar es Salaam.

Katika mtaa huo kuna wale wanaojiita mafundi wa vifaa vya kielektroniki; hasa simu za mkononi.

Baadhi ya mafundi simu katika eneo hilo walipohojiwa walikiri kuwa lipo ongezeko kubwa la mrundikano wa simu zilizoharibika, ambazo huamua kuzitupa pindi zinapokosa wateja au kupitwa na wakati.

“Tunapokea simu nyingi sana hapa, baadhi ya simu hizo huletwa eneo letu kwa ajili ya kutengenezwa, hata hivyo zipo zinazoshindikana, hivyo kubakia eneo hilo na kurundikana, mwsiho wa siku tunazitupa tu,” anasema Juma Ismail, fundi wa simu ambaye anasema kazi hiyo hajawahi kuisomea bali alifundisha na rafiki yake.

Daktari Dominic Mabula wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo anakiri kwamba takataka za kielektroniki kuleta madhara katika afya ya mwanadamu.

“Takataka hizo zisipotupwa kwa uangalifu au kuharibiwa kabisa, zinaweza kupenya katika vyanzo vya maji au katika sehemu za kilimo kama mashamba na bustani, hivyo kuleta madhara ya kiafya kwa watumiaji wa mazao yanayolimwa au maji yanayopitiwa na mabaki ya vifaa hivyo,” anaeleza mtaalamu huyo wa afya.

Anataja kemikali hizo ambazo zinaweza kupatikana kwenye mabaki hayo kuwa ni risasi, berylium, arsenic, zebaki, antimony na cadimium.

Kemikali hizo hupatikana katika vifaa vilivyotumika kwenye simu za mkononi, kompyuta; vikiwamo – saketi, mazabodi,  monita pamoja na betri.

Madhara yanayoweza kumpata mtu endapo atatumia kemikali zinazozalishwa na vifaa hivyo baada ya kutupwa hovyo ni pamoja na kuvurugwa kwa mfumo wa fahamu, shinikizo la damu, figo kushindwa kufanya kazi na maini.

Madhara mengine yanayoweza kujitokeza ni pamoja mfumo wa mmeng`enyo wa chakula, mfumo wa homoni na magonjwa ya saratani.

Dk. Mabula ameshauri kuwa njia bora ya kuepuka madhara hayo ni kwa kutafuta njia mbadala za kurejeleza takataka hizo, kuzichoma moto kwa usimamizi wa watu weye ujuzi, kwani vifaa vingine huweza kuripuka.

“Pia mafundi badala ya kutupa hovyo vifaa hivyo, baadhi wanaweza kutumia kama spea, kuepuka kabisa kutupa katika vyanzo vya maji au sehemu za kilimo kwani kwa kufanya hivyo huhatarisha afya za watumiaji wa vyakula na maji katika eneo husika,” anaongeza.

Akizungumza na FikraPevu msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala anakiri kuwepo kwa tabia ya kutupwa hovyo kwa biadhaa za kielektroniki zikiwamo simu na kompyuta.

Miongoni mwa simu ambazo zinaonekana kuzagaa kwenye majalala ni zile za zamani, hasa zisizokuwa za kidigitali ambazo zilipigwa marufuku na TCRA.

Anasema kazi ya ofisi yake ni mawasiliano, lakini kuangalia namna bidhaa za kielektroniki zinavyoweza kuharibiwa ili zisiwe na madhara kwa wananchi siyo majukumu yao.

“Ndugu mwandishi mimi ninachojua ni kuwa zipo simu feki tulizozizima, na huenda nyingi zimetupwa, lakini kwenye suala la kuzikusanya na kuziharibu, inawahusu watu wa mazingira Zaidi,” anasema.

Aliongeza kuwa vipo baadhi ya vituo ambapo ukusanyaji wa simu feki ulifanyika mfano Mlimani City, Dar es Salaam, lakini hana uhakika simu hizo zilipelekwa wapi, maana ofisi yake haikuhusika kuzikusanya, bali wenye kampuni za simu.

Kampuni ya simu za mkononi ya TiGo inasema kuwa wao wakati wa zoezi la kuachana na analogia walikusanya simu kadhaa na kuwapa wateja simu mpya na zile walizokusanya waliziharibu.

Akizungumza na FikraPevu, mmoja wa maofisa waandamizi wa TiGo anasema kampuni yao ilizikusanya simu hizo na kuzichoma moto kwa kufuata njia za kisayansi kuharibu vifaa vyenye madhara kwa mazingira.

Hata hivyo, mabaki ya vifaa vya kielektroniki yanaweza kugeuka kuwa na faida kubwa kama yalivyomtoa kwenye umasikini kijana Alex Mativo wa Kenya.

Alex kwa kutumia mabaki ya vifaa vya kielektroniki anatengeneza mapambo, samani za ndani na viatu.

Serikali kupitia mamlaka zinazohusika inao wajibu wa kuhakikisha kuwa inapunguza takataka za kielectroniki kwani madhara yake kwa mazingira na binadamu ni makubwa.

Kupunguza idadi ya takataka ni pamoja ni kuzuia uagizaji wa vifaa vya mitumba kutoka nje ya nchi mfano televisheni, redio, simu pamoja na kompyuta ambazo kwa namna moja au nyingine huwa na maisha mafupi.

Wananchi nao wanawajibu wa kuhakikisha wanaepuka kununua vifaa vilivyotumika au vyenye kiwango kidogo cha ubora, kwani madhara yake kiafya ni makubwa endapo vitaharibika na kutupwa hovyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *