Tanzania kujitathmini mapambano dhidi ya dawa za kulevya

Jamii Africa

 Kila ifikapo Juni 25 kila mwaka dunia inaadhimisha siku ya kupiga vita dawa za kulevya na kutathimini jitihada zilizofikiwa katika kupunguza tatizo la matumizi ya dawa hizi. 

Biashara ya dawa za kulevya ni tishio katika nchi mbalimbali duniani huku ikiathiri uchumi wa dunia kutokana na jitihada za kutokomeza kukabiliwa na changamoto nyingi. 

Pamoja na harakati za wadau katika nchi yetu kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya tumeshuhudia ongezeko kubwa la biashara hii haramu kutokana na kiasi kikubwa cha dawa  kinachokamatwa  na idadi ya watumiaji kuongezeka. 

Tume ya Kuratibu Uthibiti wa dawa za kulevya iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ndio iliyopewa jukumu la kuratibu masuala yote yanayohusu dawa haramu za kulevya hapa nchini, imefanya kazi nzuri ikishirikiana na vyombo vya dola hususani  kikosi kazi cha kupambana na dawa za kulevya. 

 Jitihada hizo bado hazijafanikiwa kwasababu biashara hiyo haramu inaongezeka na hili limedhihirika kwa  kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kinachokamatwa kila mwaka.

[

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2011 kilo 264.3 za dawa za kulevya aina ya heroin zilikamatwa ikilinganishwa  na kilo 185.8 zilizokamatwa mwaka 2010 ikiwa ni ongezeko la asilimia 42 la kiasi cha heroin kilichokamatwa  katika kipindi cha mwaka mmoja tu.

Kama hiyo haitoshi, mwaka huo huo kilo 126 za dawa za kulevya aina ya cocaine zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 63 zilizokamatwa mwaka 2010, ambapo ni ongezeko la asilimia 100. Ongezeko hili ni kubwa na linaashiria kukuwa kwa biashara ya dawa za kulevya na kuwa upatikanaji wake ni rahisi huku  watumiaji wake wakiongezeka.

Ingawa hakuna takwimu sahihi za watumiaji wa dawa za kulevya katika nchi yetu lakini inakadiriwa takribani watu laki moja na nusu hadi laki tano wanatumia dawa hizo. Kati ya watumiaji hao wengi ni vijana ambao wameacha shule na kujiunga na makundi rika ambayo yana mitandao na wauzaji wa dawa hizo. Lakini hali ngumu ya kimaisha ambayo watanzania wengi wanapitia nayo ni kichocheo kingine cha kukua kwa biashara hii.

Athari zaidi za matumizi ya dawa za kulevya inaonekana katika afya za watu ambapo wakati huu watu wengi wanakumbwa na maradhi ya moyo, ini, mapafu, meno, figo, umbo, ngozi, maradhi ya akili, kansa, ugumba, kuzaa watoto wafu. Pia huwafanya watumiaji kuwa tegemezi kwa ndugu, uteja, kusababisha au kupata ajali na wakati mwingine hata vifo.

Taarifa za tume ya kuratibu uthibiti wa dawa za kulevya zinaonyesha katika kipindi cha mwaka 2011 jumla ya watumiaji 4,684 wa dawa za kulevya walihudumiwa katika vituo vya afya vya manispaa na majiji nchini. Pia takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwezi Desemba 2011 wajidunga  heroin wapatao 250 walikuwa wakipatiwa tiba katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 

Idadi hii ni kubwa na inaathiri nguvu kazi ya taifa kwa sababu matatizo ya kiafya yanayotokana na dawa za kulevya huwafanya watumiaji kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo hivyo kurudisha nyuma jitihada za serikali kuboresha maisha ya wananchi.

Kutokana athari za kiafya za matumizi ya dawa za kulevya idadi ya wagonjwa wa akili inaongezeka na kuleta mtafaruku katika familia nyingi kwa sababu watumiaji wakipatwa na maradhi yatokanayo na dawa za kulevya huwa tegemezi na kuzidisha umaskini.

Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nayo yanachochewa na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kushirikiana sindano kwa wale wanaojidunga  na kufanya ngono zisizo salama. Hata wale waliokwisha ambukizwa VVU wanapoendelea kutumia dawa za kulevya kinga yao hushuka haraka zaidi na kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa nyemelezi kama vile homa ya ini, kifua kikuu, kaswende na kisosono.   

Katika utafiti uliofanyika mkoani Dar es salaam mwaka 2006 ulionyesha kuwa asilimia 42 ya wajidungao walikuwa wamepata maambukizi ya VVU. Utafiti mwingine kwa wajidunga wilaya ya Temeke mwaka 2010 uliofannywa na Asasi ya Medicine Du Monde uligundua asilimia 34.8 ya wanaojidunga heroin waligundulika na VVU, wengine asilimia 27.7 waligundulika  na virusi vya homa ya ini.

Biashara  na matumizi ya dawa ya kulevya  huvuruga mfumo wa maisha ya jamii ikiwa ni pamoja na mmomonyoka wa maadili. Kutokana na kuiga kwa tamaduni za kigeni kupitia vyombo vya habari watu wamebadili mfumo wa kuishi na kuacha tamaduni za jamii.

 Tabia hizi zimesababisha vijana wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya ambapo huambatana na unyang’anyi, ngono zembe hivyo kujenga jamii isiyo na mwelekeo mzuri wa maendeleo.
Matukio ya kigaidi utekaji nyara  na vita vya wenyewe kwa wenyewe au vita kati ya serikali na magenge ya  wafanyabiashara wa dawa za kulevya inachochewa zaidi na matumizi ya liyokithiri ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana, hivyo kuhatarisha usalama wa nchi na kujenga jamii isiyo na amani na utulivu.

Ni rai yangu kwa wadau wanaohusika ikiwemo tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya kuongeza juhudi na kutumia tekinolojia mbadara za kutokomeza biashara hii haramu ambayo inakuwa na  kuathiri sehemu kubwa ya jamii yetu hivyo kudhorotesha harakati za kujenga jamii iliyostaarabika.

 Mapambano haya yanahitaji dhamira ya dhati kutokomeza kwa kuwa wanaohusika wanavumbua mbinu mpya za kuendeleza biashara hii ili kutekeleza maslai yao binafsi.

Kazi hii siyo ya tume pekee bali ni ya jamii nzima, tushirikiane kwa pamoja kutokomeza biashara ya dawa za kulevya kwa sababu watumiaji na wafanyabiashara wa dawa hizi wapo katika jamii yetu. Tujenge jamii yenye afya bila dawa za kulevya

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *