Imeelezwa kuwa ili Tanzania iwe kitovu cha uzalishaji wa vito vya madini ya Tanzanite, serikali na wadau wa madini nchini washirikiane na kutumia sheria kutatua migogoro baina yao na wachimbaji wadogo.
Licha ya Tanzania kumiliki hazina kubwa ya madini mbalimbali ikiwemo almasi, dhahabu lakini inasifika kwa kuzalisha vito vya madini ya tanzanite ambayo hayapatikani sehemu nyingine duniani. Madini hayo yamekuwa yakichimbwa na wawekezaji na wachimbaji wadogo katika eneo la Merelani mkoa wa Manyara.
Changamoto inayojitokeza ni migongano na wawekezaji kugombania maeneo ya kuchimba madini hayo. Hali hiyo inachochewa na maeneo waliyokabidhiwa wawekezaji ikiwemo kampuni ya Richland Resources kutokuyaendeleza ambapo wachimbaji wazawa huingia na kuchimba Tanzanite katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wawekezaji kutoka nje.
Mwaka 2004 serikali ilibadilisha leseni na kuipatia kampuni nyingine ya African Gem Resources ili kuendeleza eneo hilo ambalo linazungukwa na wachimbaji wadogo.
Malalamiko ya wachimbaji wadogo ni kutothaminiwa na kupewa huduma muhimu za kijamii ikizingatiwa kuwa wanafanya shughuli zao kisheria kama wazawa ambao wana haki ya kutumia rasilimali zilizopo ili kuchangia katika maendeleo ya taifa.
Kulingana na Sera ya Madini (2009) ambayo ilijenga msingi wa kuanzishwa kwa Sheria ya Madini ya mwaka 2010, inaitaka serikali kuhamasisha, kusaidia na kuwawezesha watanzania kushiriki katika uchimbaji wa vito vya madini ili Tanzania iwe kitovu cha uzalishaji wa vito vya thamani Afrika. Pia kuhakikisha uchimbaji wa kati na mdogo wa vito vya madini unamilikiwa na kuendeshwa na watanzania na kuwashirikisha wawekezaji wa ndani katika uchimbaji huo.
Ripoti ya Taasisi ya Umiliki wa Rasilimali Asili (2009) inaeleza kuwa mamlaka za serikali zimeshindwa kutumia sheria na sera kikamilifu kumaliza migogoro katika eneo la Merelani na badala yake wachimbaji wadogo wanaondolewa katika maeneo hayo ili kupisha uwekezaji mkubwa ambao utaihakikishia serikali mapato.
Mitambo ya kuchakata madini ikiwa eneo la mgodi wa TanzaniteOne
Ili kutuliza migogoro ya madini, Serikali imeanza ujenzi wa ukuta kutoka kitalu A hadi D kuzunguka eneo lote la mgodi wa Tanzanite One ili kudhibiti uchimbaji na soko la madini hayo ambayo yanapatikana Tanzania pekee. Lakini wachambuzi wa masuala ya madini wanasema njia hiyo inaweza isiwe suluhisho kumaliza migogoro na wachimbaji wadogo waliopo katika eneo hilo.`
Imeelezwa kuwa njia sahihi ni kuweka mfumo wezeshi ambao utawakutanisha wachimbaji wadogo na wawekezaji wa kigeni kufanya kazi pamoja kwa kuzingatia matakwa sheria. Kampuni ya Williamson Diamond ambayo inachimba dhahabu katika eneo la Mwadui, mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kwa sehemu kupunguza migogoro na wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakivamia eneo la uchimbaji linalomilikiwa na wawekezaji hao.
Mwaka 2006, kampuni hiyo ilianzisha jopo la wadau kutoka sekta mbalimbali lililojulikana kama Community Diamond Partnership ikishirikiana na kampuni ya De Beers, serikali ya Tanzania na vijiji saba vilivyo karibu na mgodi huo.
Jopo hilo lilifanikiwa kutenga eneo la uchimbaji wa dhahabu kwa ushirikiano na wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kupata ujuzi, kuongeza thamani ya madini, huduma za fedha na afya. Njia hii ilifanikiwa kupunguza migogoro na wachimbaji wadogo.
Sheria kuwalinda Wachimbaji wadogo
Tangu kuanza shughuli za uchimbaji wa madini nchini, Tanzania imechukua hatua mbalimbali kuwawezesha wachimbaji wadogo kutambulika na kufanya shughuli zao kisheria. Mwaka 1997 serikali ilirahisisha upatikanaji wa leseni, ardhi na kuongeza eneo la uchimbaji kwa ajili ya wachimbaji wazawa.
Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ilianzisha leseni ya awali ya uchimbaji madini kwa wachimbaji wazawa ambayo ilikuwa inapatikana kwa Dola za Marekani 100,000 kwa ajili ya uwekezaji na mkataba wa miaka 5 hadi 7. Mchakato wa kupata leseni ya awali hauna mahitaji makubwa ikilinganishwa na leseni zingine japokuwa tathmini ya mazingira na uchunguzi wa kijamii katika eneo husika ni muhimu.
Leseni hizo zinatolewa na Afisa Madini wa Kanda na sio Kamishna wa Madini ambaye ofisi yake iko Dar es Salaam. Tangu mwaka 2004 serikali imetenga zaidi ya kilomita 2,000 ya ardhi kwa ajili ya wachimbaji wazawa ikiwemo vitalu mbalimbali vya uchimbaji wa vito vya thamani. Pia inatoa fedha kuwasaidia wachimbaji wadogo, japokuwa usimamizi wake sio wa uwazi.
Hata hivyo, serikali ina mipango mingi kuwawezesha wachimbaji wazawa lakini changamoto inajitokeza kwenye utekelezaji wa mipango hiyo na kuhakikisha sekta ya madini inakuwa na uwiano mzuri wa ushindani kati ya wawekezaji wakubwa na wachimbaji wadogo.