Tanzania: Utajiri wa gesi waanza kunufaisha vigogo!

Jamii Africa

UTAJIRI wa gesi asilia Tanzania, unatishiwa na ufisadi ndani ya mfumo wa utawala na kuna taarifa za uhamishaji wa fedha zinazohofiwa kutokana na uwekezaji katika sekta hiyo.

Uchunguzi umeonyesha kwamba, kwa miaka kadhaa, baadhi ya watu ndani ya mfumo wamekua wakitumia mbinu chafu kujinufaisha na rasilimali ya gesi nchini.

Tanzania inatarajiwa kuongeza makisio ya kiwango cha utajiri wake wa gesi asilia hadi kufikia takriban futi za ujazo trilioni 30.

Pamoja na marekebisho hayo, kuna mashaka kama mapato mengi yatakayotokana na gesi hiyo yatatumika vema bila kuathiriwa na ufisadi.

Tayari baadhi ya kashfa zimekwishakuibuliwa ndani ya Bunge na katika baadhi ya vyombo vya habari na kuzidi kuibuliwa hivi karibuni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Juni mwaka huu, Zitto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Upinzani na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alidai kwamba maafisa na wanasiasa walikula rushwa ili kutoa leseni za kutafuta gesi katika duru ya 2004/06 na kwamba walikuwa tayari kufanya vivyo hivyo katika duru inayofuatia.

Wizara ya Nishati na Madini imo mbioni kupanga duru ya nne ya zabuni kwa vitalu tisa vipya, na hivyo kufanya masuala ya utawala bora  kuwa nyeti. Matarajio ya wabunge wengi ni kwamba bahati hiyo ya gesi hatimaye itamaliza kabisa tatizo sugu la upungufu wa nishati ya umeme ili watu wengi zaidi wafaidike nayo.

Hadi sasa ni Watanzania wachache waliounganishwa kwenye gridi ya taifa, ambayo nayo huathiriwa na kukatika kwa umeme kwa hadi saa 12 kwa siku.

Tanzania haijabuni sera ya taifa ya kukuza sekta ya gesi  ukaa na mfumo maridhawa wa sheria ya kodi, jambo linalowatatiza wachambuzi wa masuala ya uchumi.

Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, aliwatuhumu kwa mgongano wa kimaslahi ama ufisadi wabunge sita walio katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

Waziri mpya wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, Julai 29, 2012 alikuwa amedokeza juu ya madudu katika shirika la umeme, Tanesco.

Wabunge hao walituhumiwa makosa madogo katika manunuzi pale Muhongo alipomsimamisha kazi Mkurugenzi Mwendeshaji wa Tanesco William Mhando, pamoja na mameneja wengine waandamizi watatu – Robert Shemhilu, Lusekelo Kasanga na Harun Mattambo – akiwatuhumu kwa ubadhirifu.

Lissu aliyatupilia mbali madai ya kufanya makosa kwawanakamati wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kutoka Chadema. Hata hivyo Spika Anna Makinda aliivunja kamati hiyo akisubiri kukamilika kwa uchunguzi.

Kamati ndogo ya Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili naMamlaka ya Bunge inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake bunge litakapoanza kikao chake tarehe 30 Oktoba. Hata hivyo wachunguzi wanasema kwamba ripoti hiyo itasahauliwa haraka.

Tuhuma hizi zinahusu mikataba ya kuipatia Wizara ya Nishati  matairi, petroli na vitu kadha wa kadha vilivyozingirwa na udanganyifu na ufisadi mdogo mdogo. Hazilinganishwi kamwena pesa lukuki zinazotolewa kulipia mikataba inayokosolewa sana ya wafuaji umeme wa binafsi.

Muhongo alilitaarifu bunge hivi karibuni kwamba Tanesco ilikuwa inawalipa hawa wafuaji umeme wa binafsi 42billion/- (USD 26 million) kwa mwezi, kiasi ambacho ni nusu ya mapato yake yote kwa mwezi.

Muhongo aliahidi wakati anaingia madarakani kwamba angeishughulia mikataba hiyo mibovu, lakini mpaka sasa hajafanya hivyo.

Hata hivyo ni uwezekano mkubwa wa ufisadi wa kutisha katika kutoa leseni mpya za utafutaji gesi baharini kunakowaogofya wachambuzi wa mambo katika tasnia hiyo.

Hata hivyo Kabwe amekuwa akijumuisha pamoja ufisadi mdogona mkubwa ili kulitohoa suala la ufisadi na kuishinikiza serikali.

Agosti 15, 2012  Zitto alitangaza kwamba taarifa ya mwezi Juni ya benki kuu ya Uswisi, Swiss National Bank (SNB), ilionyesha kwamba viongozi serikalini pamoja na wafanyabiashara wakubwa walikuwa wameficha fedha katika akaunti zao nchini humo zinazofikia 315.5bilioni/- (USD 200million).

Kila mwaka Benki Kuu ya Uswisi huchapisha jumla ya fedha na mikopo zinazomilikiwa na wageni, ingawaje taarifa hiyo haichambui kiasi ambacho kila mwenye akaunti anamiliki.

Kabwe aliliambia bunge, “Kambi rasmi ya upinzani imepata taarifa kwamba kiongozi mmoja mwandamizi na mawaziri kadhaa katika utawala uliopita wamo katika orodha ya watu wenye mapesa hayo.

Sehemu kubwa ya pesa hizo zililipwa namakampuni yanayotafuta mafuta na gesi katika pwani ya Mtwara yaliyopewa leseni kati ya mwaka 2004 na 2006.

“Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kutoa tamko rasmi kuhusu hatua ilizochukua tangu tangu ripoti hiyo ya Benki Kuu ya Uswisi ilipotoka. Tunaitaka serikali iliambie taifa hatua itakazochukua ili kuzirejesha fedha hizi pamoja na nyingine ambazo zimefichwa katika nchi nyingine za nje. Kambi rasmi ya upinzani itayatangaza majina ya wanaomiliki fedha hizi katika mabenki nchini Uswisi kama serikali haitotoa taarifa rasmi juu ya suala hili.”

Kampuni ya Kiingereza ya Ophir Energy, ambayo inamilikiwa kwa ubia na kigogo mmoja katika chama tawala nchini Afrika ya Kusini cha African National Council, Waziri wa Makazi Tokyo Sexwale, kilipewa Kitalu 1 katika pwani ya Mtwara katika duru ya tatu ya utoaji leseni mwaka 2005.


Ophir ilipewa vitalu viwili zaidi, Kitalu 3 na 4, bila kushindanishwa mwaka uliofuata. Hii si kutoa hisia kwamba rushwa ilihusika. BG, zamani ikiitwa British Gas, baadaye ilinunua hisa katika vitalu hivyo na ndiyo inayoviendesha wakati Ophir ni mbia mwenye hisa chache.

Mtu wa kati ambaye ni mfanyabiashara raia wa Afrika ya Kusini na mwenye mahusiano ya karibu na ANC, Moto Mabanga, alisaidia Ophir kupata vitalu hivyo. Alifungua kesi jijini London mwezi Juni 2012 dhidi ya Ophir kuhusiana na mgao wake wa asilimia tano (5%) ya faida kwa mujibu wa mkataba wa kuchangia uzalishaji uliofikiwa.

Mabanga pia aliliingia katika mgogoro na kampuni ya nchini Afrika ya Kusini ya Vodacom juu ya ada kwa huduma zake baada ya kufanisha matatizo yaliyokuwa yanaitatiza kampuni hiyo nchi Kongo-Kinshasa.

Wakielezea aina ya ufisadi ambao unaweza kujitokeza katika duru inayotarajiwa ya utoaji leseni, wachunguzi wanaufananishana kesi inayowakabili sasa waziri wa zamani wa Fedha katika utawala wa Rais Benjamini Mkapa, Basil Mramba na Daniel Yona, aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini katika serikali hiyo hiyo kutoka mwaka 2002 hadi 2005.

Mramba na Yona, pamoja na katibu mkuu wa zamani wa wizara ya  Fedha Gray Mgonja, wanashtakiwa kwa kuzembea kazi zao na hivyo kuisababishia serikali upotevu wa 11,752,350,148/- (USD 7.5million).

Hii inatokana na misamaha ya kodi kwa kampuni ya Alex Steward Assayers, iliyokuwa imepewa tenda nono ya kuhakiki dhahabu iliyopatika kati ya mwaka 2003 na 2007. Daniel Yona pia alikuwa mkurugenzi asiye mtendaji katika kampuni ya Dominion Petroleum, kwa mujibu wa mashirika ya habari.

Kampuni ya Dominion ilinunuliwa na Ophir mapema mwaka huu. Wote watatu wamekana mashitaka yanayowakabili katika kesi hiyo, ambayo imeahirishwa hadi tarehe 12 Oktoba.

Ndani ya bunge, Kabwe ameitaka serikali kutoka taarifa rasmi kuhusu hatua ilizokwishachukua kuhakiki uhalali wa wenye fedha zilizotajwa katika ripoti ya Benki Kuu ya Uswisi (SNB).

Anataka pesa hizo zirejeshwe nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na fedha nyinginezo zilizofichwa nchi za nje. La sivyo anatishia kuwaanika wenye fedha hizo kama serikali itachelea kutimiza madai yake.

Mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu kulikuwa na shinikizo kwamba wizara isitishe duru ya nne ya zabuni za leseni za  kutafuta gesi hadi hapo Bunge litakapokuwa limeyashughulikia masuala ya sera na mikakati ya ukuzaji uchumi mintarafu tasnia ya nishati.

Inaelekea kwamba Wizara ya Nishati imeitikia wito huo na sasa inataka duru hiyo isitishwe hadi Sera ya Gesi Asilia itakapokuwa imewasilishwa bungeni hapo bunge litakapokutana tena tarehe 30 Oktoba. Rasimu ya Sera ya Gesi tayari imeshawasilishwa wizarani, kwa mujibu wa Prof Samuel Wangwe.

Taasisi ya utafiti na uelekezi katika masuala ya umasikini ya mjini Dar es Salaam, Research on Poverty Alleviation (REPOA) imeombwa na wizara kubuni mapendekezo. Wizara ingependa sera hiyo iridhiwe kwanza kabla serikali haijaanza juhudi za kutangaza fursa katika sekta ya gesi. Maonyesho juu ya fursa hizo yaliyoandaliwa na shirika la ukuzaji wa sekta ya petroli nchini, Tanzania Petroleum Development Corporation, yatafanyika katika miji ya Houston, London, Singapore na Arusha.

Mbali ya sera ya gesi, upungufu mkubwa zaidi ambao wachunguzi wanauona ni mfumo mwafaka wa kisheria kuhusiana na rasilimani ndani ya bahari. Ukiachilia mbali uchelewesho, hakuna uwezekano wa kupitishwa kwa rasimu ya sheria ya gesi (Gas Bill) kabla ya mwezi April 2013. Hivyo huenda isiwe na athari yoyote kwenye duru mpya za zabuni. Muswada utaweka mfumo wa mikataba ya uzalishaji kwa ubia na mfumo wa kifedha. Katika hotuba yake ya bajeti, Muhongo alidokeza kwamba huenda ada kwa kusaini mikataba ikaanzishwa.

Pendekezo kali kabisa lililotolewa na Bunge ni kwamba mikataba ya sasa ya uzalishaji kwa ubia ipitiwe upya, jambo ambalo wawekezaji watajitahidi kuhakikisha kuwa linapingwa. Uhakika wa kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo utakuwa muhimu katika kuhakikisha kuwa gesi nyingi zaidi inaelekezwa katika sekta ya nishati, ambayo kihistoria imekumbwa na matatizo makubwa.

Sheria ya Gesi inaweza kusaidia kurejesha imani ya wawekezaji kwa kuweka bayana mfumo wa kodi, mrahaba na taratibu nyinginezo ambazo makampuni ya mafuta yanatakiwa kufuata. Mpango Mkuu wa Gesi yasemekana pia unaandaliwa, lakini, mbali ya kuwa haujawekwa bayana, utekelezaji wake uko mbali kama ule wa Sheria ya Gesi.

Habari hii imeandaliwa na timu ya Uchunguzi ya FikraPevu

4 Comments
  • Kwa mtanzania anayefuatilia maendeleo ya nchi yake habari hii inatia moyo juhudi zinazofanywa na serikali katika utafutaji wa gesi asilia nchini Tanzania

    Kama tunavyofahamu gesi hii ikitumiwa vizuri itakuwa mkombozi wa watanzania na kuwatoa wengi katika hali ya umaskini hususani kutumiwa katika nishati, gesi ya kuendeshea mitambo viwandani , hata kupikia majumbani

    Lakini habari hizi za kuhusisha juhudi hizi na ufisadi zinazorotesha juhudi hizi na kuifanya serikali yetu ionekane kama haitilii maanani umaskini uliotandaa na gesi hii ingekuwa mkombozi.

    Kama tulivyowahi kuzungumza huko nyuma kuwa serikali ya hayati Mwalimu Julius Nyerere siyo kwamba ilishindwa kufanya haya ila mwalimu aliona wakati wa sisi kujiendesha , kuchimba madini haya ulikuwa haujafika.

    Aidha baada ya kuondoka pamoja na kuwaalika wageni kukamilisha utafutaji wa madini na uchimbaji wa gesi lakini tumeshughudia malalamiko mengi toka kwenye machimbo ,kama ndege kutua na kusafirisha madini bila wakala wa TRA kuwepo na hata walipokwenda ujazo ulioandikwa na uliokuwepo physically kwenye madini hayo ya dhahabu ulitofautiana kwa kiwango kikubwa.Aidha tumeshughudia mauaji katika maeneo ya machimbo hayo

    Wenyewe tunashughudia taarifa ya ufisadi na uwekaji wa fedha /mabilioni ya fedha zilizotokana na kuuza vitalu vya gesi asilia kwenye akaunti za bank nchini Uswis.

    Jambo hili linaendelea kuiwekea serikali yetu doa kama haitafuatilia haraka na kujua ni akina nani hao waliochota/waliohongwa fedha hizo kabla kambi ya upinzani haijawaanika hadharani

    Kwa busara alizonazo mheshimiwa Rais Kikwete ambaye kwa kiwango kikubwa anatekeleza kwa asilimia kubwa sera alizojiwekea kama tulivyoshughudia kujengwa daraja la Kigambobi, kuhakikisha barabara za Dart kwa magari yaendayo kwa kasi zinajengwa na kupunguza msongamano , kuanza kwa fly over huko Ubungo ni juhudi tosha zinazotia imani kuwa mheshimiwa Kikwete anajali yale aliyoahidi

    Aidha siyo muda mrefu tulishughudia aliwaacha mawaziri na manaibu waziri waliotajwa kwenye taarifa ya mkaguzi Utoh tuna imani kuwa hili nalo atalifanyia kazi kwa haraka na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinarudishwa nchini kwa maendeleo ya watanzania

    Aidha sheria ya gesi iharakishwe ili kuondoa mwanya wa hawa watu wachache wanaotaka kujilimbikizia utajiri haramu kinyume na taratibu za nchi

    Ni matarajio yangu kuwa kila kiongozi aliyepewa dhamana ya kuongoza nchi hii awe na uchungu na nchi hii na naamini maendeleo ya haraka yatapatikana kwani Tanzania ni nchi tajiri mno na nchi nyingine za Afrika zitakuja kuiga maendeleo yetu kama tulivyotumia amani yetu kuzikomboa nchi nyingi za Afrika na kulinda amani duniani

    Kwa maana hiyo tusitake amani yetu hiyo ichezewe kwa watu wachache wanaotaka kujilimbikizia utajiri na kuanza kuleta kutokuelewana na chokochoko kwenye mfumo huu wa vyama vya upinzani.

    Tuangalia majirani zetu ambao wamekuwa na mali asili na kushindwa kuisimamia na matokeo yake ni mauaji kila siku na mapiduzi ya serikali kila kukicha

    Mungu ibariki Tanzania

  • Tatizo langu kubwa ni pale ambapo viongozi wa taifa hili hawajaamua kwa dhati kuwekeza kwenye hii sekta kwa kujenga chuo kikuu kitakachozalisha watalaam wa kutosha nchi nzima kwa kipindi kifupi kwenye hii sector ,wataalam wa level tofauti certificate ,diploma na bachelor au wapanue chuo cha madini kiwe Higher learning institution

  • utajiri wa nchi yetu hauendani kabisa na umasikini wa watanzania hii yote ni matokea ya uongozi mbovu saana tulionao chini ya chama cha mapinduzi ambacho kwa sasa hakionio aibu kamwe kwa haya yanayoendelea chini, ninahakika kabisa kwamba utajiri wa nchi hii utawanufaisha zaidi viongozi wa serikali kuliko watanzania wenyewe kwakuwa wao wako nmadarakani kwa manufaa yao ebu jiulize kuhusu wanyama poli walivyotoroshwa nchini, tena kwa ndege ya kijeshi.

    Jiulize jinsi kagoda walivyo iba pesa katika akaunti ya madeni ya nje epa. naamini kwamba chini ya utawala mbovu wa ccm maisha ya watanzania yataendelea kuwa mabaya sana kwakuwa ni chama kilichodhihilisha kwamba chenyewe na mafisadi ni ndugu hivyo kushindwa kuwajibisha wale woote wanaoonekana kwenda kinyume na misingi ya chama.

    Hebu tujiulize kama kweli mwenyekiti wa chama cha mapinduzi jakaya kikwete hana uhusiano na Kagoda, ni kwanini alivuja sheria ya nchi kwa kukaa na wezi na kuwaomba warudishe pesa? Hii yote nikwasababu mlango wa nyuma ccm ndio kagoda kitu kilicho fanya wakwame hata kuigusa kagoda tunahitaji mapinduzi makubwa ya kuiondoa serikali ya kifisadi madarakani.

    Haya yoote yanawezekana tukiamua kwa dhatyi kuichukia ccm kwa dhati.

  • Nchi hii ni nzuri sana, kila lililo bora na lenye heri lipo hapa na ndiyo maana majambazi wa uchumi wanaikimbilia sana na wale wanaoshindwa kuifikia wanakuwa na uchu wa fisi.

    Lakini ninachoweza kusema ni kwamba,haya yote ya ufisadi wa makusudi na wazi yanaotokea kwa sababu ya mfumo mzima wa uongozi tulionao sasa. Viongozi wengi walioko madarakani wanajua wanachokifanya, tena bila hata aibu wameamua kugawana raslimali tulizonazo kiaina.

    Mimi nasema hivi ili mambo yaende sawa tunahitaji kuwa na kiongozi mwenye utawala wa kidikteta, kwamba akitamka jambo basi ijulikane na kuheshimika.

    Jamani tunahitaji kiongozi kama wa Rwanda,hakuna kuangalia nyuma katika masuala ya maendeleo anayekwamisha apate mkong’oto.

    Mafisadi mtanisamehe lakini ukweli ndio huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *