Tanzania yamtimua nchini raia wa Uingereza

Jamii Africa

SERIKALI kupitia Idara ya Uhamiaji, imewatimua nchini wahamiaji 26 akiwamo Raia mmoja wa Uingereza mwenye asili ya Afrika Magharibi, Fikra Pevu imethibitisha.

Uchunguzi wa Fikra Pevu, umebaini kuwa wahamiaji yao wametimuliwa nchini kwa kupewa hati ya wasiotakiwa nchini (PI) katika msako wa kushitukiza uliokuwa ukifanyika na Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam.

Habari zilizothibitishwa na maofisa uchunguzi wa Uhamiaji, zimeeleza kwamba msako huo ulifanyika kati ya Novemba 9, 2011 na Alhamisi ya Januari 5, 2012, ambako wahusika walichukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Muingereza aliyetimuliwa nchini kwa kupatikana na hatia ya kuishi nchini kinyume cha sheria ametajwa kwa jina la Sialuka Kuba-Kuba, ambaye alikamatwa na kupewa hati ya kutakiwa kuondoka nchini hivi karibuni.

Wengine ni pamoja na raia wa Malawi mmoja Sohail Masoud, na Mnigeria Prince Chukwudi Ukaegbwem pamoja na Raia watatu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Wamo pia raia wanne wa Kenya, Waganda wawili.Warundi wawili, Mnyarwanda mmoja aliyetajwa kwa jina la Ngendehimana Omar, Wapakistan watano, Wahindi wawili, raia wawili wa Nepal na Wachina wawili.

Wakati huo huo, msanii maarufu wa sauti za viongozi Steven Nyerere, Alhamisi jioni alionekana katika ofisi za Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam, akiwa pamoja na baadhi ya watuhumiwa, lakini haikufahamika hasa alikuwa na shughuli gani.

Hata hivyo, maofisa wa Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam, walikataa kuzungumzia kuhusiana na kuwapo kwake eneo hilo, na kusema kama kuna jambo linalomhusu watatoa taarifa, pamoja na kuelezwa kwamba alifika kuwawekea dhamana baadhi ya watuhumiwa.

Baadhi ya wahamiaji haramu wakiwa ofisi za Uhamiaji Dar es Salaam
1 Comment
  • Aisee! Unajua this time bongo ni kama chimbo la wageni haramu. Idadi inazidi siku hadi siku. Kkoo sa hivi ukilogwa tu kuingia katika duka la computer lazima ukutane na wasomali kama wanne hv wanakukaribisha, achilia wawili walio kaunta na wawili wanaojifanya technicians wanaokuunganishia vifaa. Haya ngoja tuendelee na siasa tuone…..!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *