Wakati mjadala ukiendelea kuhusu serikali ya Zanzibar kuagiza walimu 300 kutoka Nigeria kwaajili ya kufundisha masomo ya sayansi, nchi hiyo imeendelea kutoa somo la uboreshaji elimu kwa Tanzania baada ya kuanzisha mpango wa kutoa chakula shuleni.

Nigeria, nchi iliyopo Magharibi mwa Afrika imeanzisha Programu ya Kitaifa ya chakula shuleni (NSFP) ambayo inalenga kuongeza ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi kwa kuhakikisha wanapata  chakula na kutulia darasani.

Nigeria imeajiri  wapishi 87,000 kwaajili ya kuandaa chakula kwa wanafunzi milioni 8.2 ambao wako kwenye program hiyo. Hapo awali wakati program hiyo ilipoanzishwa na rais Muhammadu Buhari mwaka uliopita ilikuwa inawahudumia wanafunzi milioni 5.5 wa shule za msingi.

Ili kuwafikia wanafunzi wote, programu hiyo inatekelezwa kwa awamu ambapo, wanafunzi wengine 8,260,984 waliopo katika shule 45,394 za msingi wameingizwa rasmi kwenye program hiyo. Na programu hiyo inatekelezwa katika majimbo 24 huku lengo ni kuyafikia majimbo yote 36 ya serikali ya Shirikisho ya Nigeria.

Programu hiyo, sio tu imetengeneza ajira nyingi lakini imechangia katika ukuaji wa uchumi wa ndani kwa kuwakutanisha wakulima na masoko ya shule zinazohitaji mazao.

Pia imeongeza uandikishaji na wanafunzi wengi kutulia shuleni, jambo linaloashiria mwanzo mzuri wa kuboresha elimu ya Nigeria ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

 

Kupunguza umaskini na utapiamlo

Kwa upande mwingine, program hiyo inatatua tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto na uwezekano wa wanafunzi kuendelea na masomo na kufanikiwa katika maisha utakuwa mkubwa.

Chakula huchangamsha ubongo wa mtoto na kumuwezesha kusoma kwa bidii

Kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mwaka 2016 pekee watoto milioni 59 wa Afrika walidumaa na milioni 14 walidhoofika na kupungua uzito. Ukiweka pamoja, idadi hiyo ni zaidi ya wakazi wote wa Ufaransa na Afrika Kusini; pia ni mara saba zaidi ya idadi ya wakazi wa Switzerland.

“Kuna kila sababu ya kujali: lishe duni ni kisababishi kikubwa cha vifo vya mamilioni ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano. Watoto milioni 3 wanafariki kila mwaka barani Afrika kwa utapiamlo. Ikiwa hali hii itaendelea hadi 2030, Afrika itapoteza watoto milioni 36 kwasababu walikuwa hawana chakula cha kutosha au hawakula vizuri”, amenukuliwa rais wa AfDB, Akinwumi Adesina.

Programu hiyo ni sehemu ya Dola za Marekani 1.6 bilioni za mfuko wa Uwekezaji wa Jamii wa serikali ya shirikisho ambao unalenga kupunguza umaskini na kuimarisha afya na elimu ya wanafunzi na makundi yaliyo pembezoni mwa nchi.

Makamu wa rais wa nchi hiyo, Yemi Osinbajo amesema program hiyo itaongeza uandikishaji na idadi ya wanafunzi wanaohitimu. Kila mwaka asilimia 30 ya wanafunzi wa shule za msingi Nigeria wanakatisha masomo.

 

Tanzania ina la kujifunza?

 Tanzania ina la kujifunza kutoka Nigeria ikizingatiwa kuwa haina mpango wa kitaifa wa kutoa chakula shuleni, licha ya kufanikiwa kutoa elimu bure iliyoongeza uandikishaji shuleni.

Huduma hiyo imekuwa ikitolewa na wazazi kwa kushirikiana na walimu katika baadhi ya mikoa ukiwemo Kilimanjaro ambao unafanya vizuri katika sekta ya elimu.

Utafiti ulioendeshwa na Shirika la chakula na kilimo, (FAO) mwaka 2013, unaonyesha kwamba mpango wa kuwalisha chakula wanafunzi mashuleni unaongeza ulinzi wa kijamii, chakula na lishe kwa wanafunzi.

Utafiti huo ulioangazia utaoaji wa chakula mashuleni na uwezekano wa kununua nafaka moja kwa moja kutoka kwa familia husika umehusisha nchi nane ambazo ni Bolivia, Colombia, El Salvador, Guatemala, Honduras, Nicaragua, Paraguay na Peru na unaonyesha kwamba mpango huo unaimarisha mahudhurio na kukuza mchakato wa kujifunza.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO  , José Graziano da Silva amesema mbinu hiyo ina faida tatu alizoziainisha kwamba ni usalama wa ubora wa chakula kwa wanafunzi katika shule za uma, kukuza matumizi ya chakula chenye afya na safi pamoja na kufungua uwezekano wa masoko na kipato kikubwa kwa wakulima huku ukikuza maendeleo ya maeneo husika.

By Jamii Africa

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism

Leave a Reply

Your email address will not be published.