Tarime: Utoro waathiri shule za msingi. Walimu, wanafunzi ‘washindana’ kuokota mawe ya dhahabu mgodini

Jamii Africa

UTORO limekuwa tatizo sugu na linaloonekana kudumu katika shule za msingi zilizopo Nyamongo, wilayani Tarime mkoani Mara.

Kati ya wanafunzi 3,465 walioandikishwa darasa la kwanza 2016, ni 2,991 ndio wameweza kuripoti na kuendelea na masomo ya darasa la pili kwa mwaka wa 2017.

FikraPevu ina taarifa kuwa wanafunzi 474  hawajulikani waliko, hivyo kufifisha kufikiwa kwa malengo ya elimu bure nchini kwa shule za msingi na sekondari.

 

Katika uchunguzi wake, FikraPevu ilifika  kwenye shule za msingi 13 zilizopo Nyamongo. Miongoni  mwa shule hizo ni shule ya msingi Kenyangi iliyokuwa ya mwisho katika mtihani wa darasa la saba mwaka  2016 kati ya shule 116 za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

FikraPevu imebaini utoro katika shule hizo za msingi, unachangiwa na sababu mbalimbali. Miongoni mwa sababu hizo ni wanafunzi kwenda kuokota mawe yenye dhahabu  kwenye Mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo kwa lengo la kujipatia kipato.

Walimu wakuu waeleza

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamongo,  Musiba Zerubabeli anakiri kuwepo kwa utoro kwa wanafunzi wa darasa la pili. Darasa hilo limeakia na wanafunzi 294, kati ya 360 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2016.

“Kuna mwitikio mdogo wa elimu. Watu waliandikisha watoto kwa sababu walitishiwa kuwa wasipoandikisha watakamatwa. Baada ya kuwaandikisha wameona hakuna hatua zinazochukuliwa,’’anasema Zebubabeli.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kewanja, Mwanaisha Sabaya anasema darasa la pili shuleni hapo linaongoza kwa utoro. Wakati darasa la kwanza kulikuwa na wanafunzi 356, hivi sasa wanafunzi 80 hawajulikani waliko.

“Hili ni eneo la utafutaji. Wazazi wanahamahama. Tulishaandika barua kwenda serikali ya kijiji ili waweze kuwatafuta mtaani, tukawaandikia wazazi barua, lakini wanafunzi hao hawajafika shuleni.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kewanja, Kata ya Kemambo-Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara wakiwa darasani.

walimu Mkuu wa Shule ya Nyabigena ambaye pia ni Kaimu Mratibu Elimu Kata ya Kemambo, Mnanka Gweso anasema wanafunzi kati ya wanafunzi 420 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka jana, ni wanafunzi 321 tu ndiyo walioripoti darasa la pili mwaka huu.

“Mzungu asipomwaga mawe ya dhahabu, mzazi anahamia eneo lingine lenye dhahabu. Pia siku ya Jumatatu, idadi ya wanafunzi inapungua kutokana na kuwa siku ya mnada. Wanaenda mnadani Jumatatu na Ijumaa,” anasema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya  Kerende, Julius Wambura anathibitisha kuwepo kwa utoro kwa wanafunzi wa darasa la pili. Kati ya wanafunzi 335 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2016, ni wanafunzi 116 tu walioendelea darasa la pili.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Ng’eng’i Beatrice Msaki akisema kati ya wafunzi 169 walioandikishwa,  waliopo darasa la pili ni 160.

Anasema utoro unasababishwa na ugumu wa maisha na wazazi kushindwa kumudu mahitaji ya shule.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Nyabusara,  Sijali Ngangambe anasema  walioandikishwa darasa la kwanza  ni 349 walioko  darasa la pili ni 263 na 30 wa madarasa mengine walifutwa shule.

Tofauti na shule zingine, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Murito, Abdalla Ntire anasema darasa la pili ni 163, idadi ambayo pia iliandikishwa kwa darasa la kwanza.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Nyangoto, Ibrahimu Igambwa anasema wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2016 ni 364, lakini waliofika darasa la pili ni 296; na watoro wa rejareja kwa mwezi February, 2017 ni 125.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Matare, Edward Kikererwa akisema wanafunzi watoro  ni 109 kati  ya hao darasa la pili ni 41.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Nyabichune,  Paul Yuda anasema ya wanafunzi 224 waliandikishwa darasa la kwanza mwaka jana walipo darasa la pili mwaka huu ni 222. Jumla ya watoro wote wakiwa 131.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyabusara kijiji cha Murito Kata ya Kemambo-Nyamongo wlayani Tarime mkoani Mara wakikusanya kuni walizoleta shuleni kwa wajili ya matumizi ya walimu.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya msingi Kwihore Joseph Nicolous anaeleza kuwa waliojiunga darasa la kwanza walikuwa 448 na waliopo darasa la pili ni 224.

Wakati Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kenyangi, Joseph Mniko anasema walioandikishwa la kwanza ni 260 na walioko darasa la pili 227, huku watoro wa shule nzima wakiwa 61.

Sheria ya mtoto ya mwaka 2009, inampa haki mtoto kupatiwa mahitaji yake muhimu, ikiwa ni pamoja na kupata elimu.

Hata hivyo, vyombo vyenye dhamana ya kusimamia sheria, vimekuwa vikishishwa kutekeleza wajibu wake.

-Hano hutaseretele wao nuraterwe – ni sauti ya Bhoke Nyamuhanga (58) akieleza kwa lugha ya Kikurya, akimaanisha usipoezeka nyumba yako, utanyeshewa na mvua, ikiwa ni msisitizo kwamba  mtu wa kwanza kumdhibiti mtoto wake ni mzazi wake mwenyewe na si jukumu hilo kumwachia mtu mwingine.

Ester Paul, mkazi wa Kiongoji cha Kegonga kata ya Matongo anaiambia FikraPevu kuwa serikali ilihamasisha wananchi wakawaandikisha watoto, lakini imeshindwa kuchukua hatua dhidi ya watoto wasiokwenda shule.

‘’Serikali ilikuja kasi kuhakikisha watoto wanaandikishwa shule,  lengo watoto wapate elimu, lakini haijafuatilia kuona kama wanafunzi wanaendelea kusoma. Wazazi waliwapeleka kwa kuogopa kukamatwa,’’ anasema.

 

Wadau wa elimu wanena

Imebainika kuwa umasikini kwenye familia unachangia utoro kwa wanafunzi na kwenda kuokota mawe ya dhahabu au vibarua vya kuchunga mifugo na kupalilia mashamba ili kupata fedha za kununua mahitaji ya shule kwa kuwa hawako kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini (Tasaf).

Mwita Mwikwabe mkazi wa Kijiji cha Nyabichune anasema, “Kuna wanafunzi wanatoka kwenye maisha magumu ambao walitakiwa kunufaika na fedha za Tasaf.  Serikali itambue kuwa si watu wote wa Nyamongo wanajishughulisha na kazi za mgodi, kuna watu wana hali duni”.

Anaongeza kuwa, “kwakuwa ni Nyamongo wanajua wote wana uwezo kuna mtoto hana baba, wala mama analelewa na bibi na babu ambao wote ni wazee inabidi yeye atafute pesa ili awasaidie wazee sasa muda wa kwenda shule unakosa na Serikali zikiwamo za vijiji zinawafahamu lakini wamefumba macho hawawasaidii.”

Mniko Chacha mkazi wa Matongo (15) anasema, “mimi baba yangu aliachana na mama miaka mingi iliyopita wakati huo nilikuwa darasa la tatu, hatukuwa na wa kutuhudumia, baba yangu ni mlevi, ilibidi mimi na mdogo wangu tuache shule”

FikraPevu imebaini kuwa wanapouza mawe hayo huweza kupata Sh. 100,000 hadi 500,000, kutegemea ukubwa yenyewe na namna “wanavyoyapima” kama yana “mali.”

Huyu anaongeza kwamba ameshaoa mke kwa ng’ombe 8 ambazo alitafuta mwenyewe na amejenga nyumba ya vyumba vitatu. Anasema “kwahiyo mimi nitaendelea kutafuta mawe siku yakiisha mgodi ukisitisha nitafanya kazi ya kilimo.”

Mwita Nyanteto (17) mkazi wa Kitongoji cha Kegonga, anasema kuwa alikuwa anasoma shule ya Msingi Kenyangi iliyoko jirani na mgodi na kwamba aliacha shule akiwa darasa la tano.

“Mawe yakimwagwa, unawaona watu mgodini wakitafuta riziki. Uvumilivu wa kukaa darasani wengine wanaenda kupiga pesa ukanishinda, labda serikali isaidie watoto wa familia masikini, ’’ anasema Nyanteto.

Walimu wa shule za msingi zilizopo Nyamongo, akiwamo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Matare, Edward Kikererwa na mwenzake kutoka Shule ya Masingi Matongo, William Kibasso wanakiri kuwa hakuna wanafunzi wanaonufaika na mradi wa Tasaf, ingawa wapo wanafunzi wanatoka familia duni.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyabichune, Alfred Mollel anasema, “Kuna siku nikiwa namchapa mwanafunzi, wenzake wakawa wanamcheka, nikawauliza mnacheka nini wakasema wanacheka yuko uchi. Kumbe nguo zilikuwa zimechanika nikamwonea huruma ikabidi nimwache”.

 

Wasemavyo viongozi wa serikali

Kumekuwepo mtindo wa kutupiana majukumu katika udhibiti wa utoro ambapo walimu kila mwisho wa mwezi wanapeleka majina ya watoro kwenye serikali za kijiji, lakini hakuna mrejesho wa hatua zozote zilizochukuliwa.

Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mnadani, Samson Magasi anasema baadhi ya wazazi hukamatwa, lakini Polisi huwaachia kwa dhamana pasipo kufikishwa mahakamani.

“Ni kazi ngumu kwa wenyeviti kuzunguka maeneo yote. Kunahitajika wiki nzima, muda huo ni mkubwa na sisi tuna kazi zetu zingine za kutafuta kipato kutafuta kipato,” anasema.

Mtendaji wa Kijiji cha Nyangoto, Samwel Mwita anasema kuwa alipokea majina ya watoro wa mwezi Januari, mwaka huu na kukaa na viongozi wa serikali ya kijiji na kutolewa kwa maazimio kuwasaka watoro kwa kuwatumia askari mgambo, wazazi wa wanafunzi watoro, kisha wawafikishe mahakamani.

Mratibu wa Elimu Kata ya Matongo, Hermes Rugeyasira anasema kuwa wanaokwamisha jitihada za kupambana na utoro ni viongozi wa serikali ya vijiji, wakiwamo watendaji kwa kushindwa kuchukuwa hatua kwa majina ya watoro wanayopewa na walimu wakuu.

Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Emmanuel Johnson anawataka wazazi kushirikiana na walimu kudhibiti utoro kwa nakwamba wapo wazazi wanapenda watoto wasome, lakini watoto wao hawapendi.

Alipozungumza na FikraPevu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Apoo Tindwa kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya baadhi ya wasiokuwa na sifa kunufaika na fedha ya Tasaf, alisema Halmashauri tayari imeunda tume ya kuchunguza kaya masikini.

 

Polisi walonga

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime /Rorya, Sweetbart Njewike alisema kuwa hajapokea malalamiko juu ya wazazi ambao watoto wao hawahudhurii shule nakwamba atafuatilia kuhusu tuhuma hizo za wazazi kufikishwa polisi na kuachiwa .

Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya mtoto Na.9 ya mwaka 2009, inamtaka mtoto kupewa stahiki zote, lakini sheria hiyo haijasema wazi kumfunga mzazi iwapo mtoto wake ameacha shule.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa aliomba muda kufuatilia idadi hiyo ya wanafunzi watoro, baada ya kupata taarifa za idadi ya wanafunzi watoro kwa shule kutoka kwa mwandishi wa makala haya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *