Tatizo la maji kwa Watanzania ni ufinyu wa fikra za watanzania

Jamii Africa
Residents fetch water at a water point in Amari Yewebesh Kebele in Amhara Region of Ethiopia 3 July, 2013. Photo by Jiro Ose Dr. Peter Salama, UNICEF Ethiopia Representative, left, and Denis Thieulin, Head of EU Delegation, visit WASH project in Amahara region.

Moja kati ya vituko vya Tanzania, ni Tanzania hubaki na shida ya maji baada ya shida ya mafuriko.
Tanzania ina miji yenye maji mengi kiasi cha kuweza kuua watu kwa mafuriko kila mwaka. Kuwa na mvua za kutosha zenye kuleta mafuriko pia.

Zaidi ya kuwahamisha watu au kuwatahadharisha watu kukaa katika maeneo hatarishi, hakuna mwenye mpango wa kufanya hatari ya mafuriko kuwa fursa. Kwa upande wangu nimeona, tunaweza kuyaelekeza maji katika maeneo tunayoyataka ili kuzuia mafuriko, na katika kiangazi tukatumia maji tulioyahifadhi ili kuwapatia raia maji safi na salama kwa mwaka mzima bila shida.

Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuleta kauli ya kutunza vyanzo vya maji, kiasi cha kuwahamisha watu maeneo ya milimani, na kuwaleta maeneo yasiyo na maji bila kuandaa miundo mbinu ya kuwapelekea maji maeneo wanayowahamishia.

Na hata ikiwa kuna miundo mbinu maji huwa ni shida kwa kuwa miundo mbinu hiyo hupitisha hewa badala ya maji. Shida imekuwa mara mbili, wakati wa mvua watu hulalamika maji (Mafuriko), wakati wa kiangazi watu hulalamika kukosekana kwa maji. Kituko.

Dhana yetu dhidi ya mafuriko ipo kwa upande mmoja, na ndio huzaa tatizo lingine. Mafuriko yakichukuliwa kama chanzo kikuu cha maji, shida ya maji haitakuwepo, badala ya kuliona hili watendaji huona mafuriko ni janga lisilo na faida ndani yake.

Baada ya kuona mafuriko kuwa janga, tumekuwa tukilikwepa. Ni akili finyu pekee ndiyo inapaswa kutegemea vyazo vya asili vya maji, kwa kuwa vyanzo hivyo hupunguza uwezo wa kutoa maji wakati wa kiangazi hivyo maji huwa shida, hapo ndipo mtu ilibidi afikiri namna ambayo angeyahifadhi maji ya mafuriko ambayo kwa akili za woga aliyakimbia na kukosa namna ya kuyafanya.

Sisemi kwamba tusiepushe vifo vinavyotokana na mafuriko, ila baada ya kukwepa mafuriko tuangalie namna ya kuyafanya maji hayo yatakavyotusaidia wakati wa kiangazi. Ni kawaida kwa mamlaka za maji kusema kuwa uhaba wa maji unaotokea kipindi cha kiangazi ni matokeo ya kupungua kwa maji katika vyanzo husika. Ni jibu sahihi, ila linatokea kila mwaka, je nini hufanyika ili kufanya hata maji yakipungua katika vyanzo vyake, hakutakuwa na mwananchi atakayepata shida ya maji?

Hapa ndipo kituko kilipo, katika hili huwa napenda kuchukua mfano wa mkoa wa Morogoro. Katika wilaya ya Kilosa, ni kila mwaka maji huleta tabu hasa maeneo ya Dumila ambapo kuna eneo wameamua kuliita ferry kwa kuwa hufurika sana wakati wa mvua. Yapo maeneo mengi ya milimani ambayo pia huwatesa raia kwa mafuriko, ni katika mkoa huo huo wa Morogoro ambao kuna maeneo hayana maji kabisa na wala sidhani kama kuna mpango wa kupeleka maji.

Serikali inayojisifu kuleta maisha bora hujisifu kwa miradi ya waarabu ambao huwachimbia visima wananchi wa kijijini. Hii ni sawa na mtu kukodi gari kuanza kujinadi kuwa gari ni lake. Kujisifu kwa misaada.

Katika fikra sahihi, tunaweza kuyafanya maji ya mafuriko yasiwe na tabu kwetu ila yakatusaidia wakati wa kiangazi. Ubaya ni fikra. Nchi kama Tanzania yenye mito mingi inayofurika kila mwaka, sio nchi ya kukosa maji hata kwa mikoa iliyo katika maeneo ya nusu jangwa kama Dodoma, ni namna ya kusambaza maji kutoka katika maeneo mbalimbali.

Labda ni uvivu au kutokuwa tayari. Nasema tatizo ni fikra. Huwezi kutegemea SDG’s kutatua tatizo lako ambalo liko ndani ya uwezo. Ndio hao na sera zao za kuleta maisha bora tangu wakati MDGs wameleta matatizo ambayo bado wengi hatujayajua kuwa ni matatizo.

Uhuru wa kweli ni fikra. Sisi wengi hatuna kazi na fikra. Tumekuwa na tabia za zamani, kuwa mkarimu kwa mgeni kuliko kwa sisi wenyewe. Hoteli za kitalii zina maji hadi wanayamwaga kwa urembo kwenye ‘fountains’ wakati kuna mwananchi ambaye japo ana bomba la maji nyumbani kwake mwezi mzima maji ananunua. Maji yamewezaje kutoka yalikotoka yakafika kwenye hoteli hizo? Nataka kusema kuwa, uwezo wa kuyasafirisha maji na kufika tunapotaka yafike tunao.

Tuyape sura mpya mafuriko. Tuyafanye kuwa fursa na sio kuona kama ni tatizo la kutolihitaji. Fikra ya ukombozi ni ile inayoangalia matatizo kama fursa na kaweza kuitumia. Hapa ni fikra ndogo sana inayohitajika, kama kuku tu katika uchafu hakosi cha kumshibisha. Tanzania katika mafuriko haipati maji ya kunywa hata kuku ametushinda katika hili.
 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *