Tetemeko: Nini kinamkwamisha Rais Magufuli kwenda Bukoba?

Jamii Africa

RAIS John Pombe Magufuli “hajakanyaga” Bukoba hadi leo, zikiwa zimepita Zaidi ya siku 60 tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi katika maeneo kadhaa ya Mkoa wa Kagera.

Kiongozi huyu wa Tanzania, hajaenda kuwapa mkono wa heri. Hajaonekana kuwafikia na kuwapa pole wananchi wa Kagera, kufuatia msiba wa Watanzania 16 waliopoteza maisha yao kufuatia tetemeko hilo.

Tetemeko hilo linaloelezwa kitaalamu kuwa na nguvu ya kushambulia ardhi kwa 5.7 kwa vipimo vya richa (Richter), lilitokea Septemba 10, mwaka huu.

Hakuna maelezo yanayotolewa na Rais Magufuli mwenyewe, wasaidizi wake wala Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu; kwamba lini atakwenda kuwafariji wananchi wa Kagera, au atatuma mwakilishi maalum na kuutangazia umma hivyo, au labda ataamua kuhutubia taifa kuelezea namna alivyoguswa na tukio hilo kubwa kuwahi kutokea Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

Watanzania waliaminishwa kwamba, Rais Magufuli alikuwa katika maandalizi ya kwenda kuwapa pole Wana-Kagera.

Siku moja baada ya janga hilo la tetemeko, Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Jaffar Haniu, alitoa taarifa kwa umma kwamba Dk. Magufuli alikuwa katika maandalizi ya kwenda Bukoba.

Katika taarifa yake hiyo aliyoitoa Septemba 11, Haniu alisema Rais Magufuli aliahirisha safari ikiwa ziara ya kikazi ya siku tatu kwenda Lusaka, Zambia, kuhudhuria kuapishwa kwa Rais Mteule wa nchi hiyo, Edgar Lungu. Hata hivyo hadi leo Magufuli hajaenda Zambia wala Kagera.

Wakati Rais Magufuli “akiendelea kujitafakari” kwenda Bukoba, mwenzake wa Uganda, Rais Yoweri Museveni, alienda kuwa pole na kutoa misaada kwa waatirika wa tetemeko hilo lililoathiri pia maeneo kadhaa ya Uganda, hasa wilaya ya Rakai.

Rais Museveni akiwa katika vijiji vilivyoathirika kwa tetemeko nchini mwake, alitekeleza ahadi ya serikali ya kutoa msaada wa mabati 30 kwa kila nyumba iliyoanguka, huku dawa, vyakula na misaada mingine ikitolewa na kiongozi huyo.

Kenya, kupitia kwa Rais Uhuru Kenyatta, siku mbili baada ya tetemeko, ilitoa msaada wa magodoro, mabati na mablanketi kwa wahanga wa kadhia hiyo.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Uhuru alitoa pole kwa familia zilizokumbwa na maafa na kuwatakia uponaji wa haraka wale waliopata majeraha na kuvunjika viungo.

Msaidizi wa Rais Magufuli alipoulizwa na FikraPevu juu ya “ukimya” wa kiongozi wa nchi kwenda Bukoba, harakaharaka, alijibu; “Rais ana ratiba yake na kama amepanga kwenda ataenda.”

Huku akikataa kutajwa jina kwa umma, msaidizi huyo wa Rais Magufuli alisema, Rais anaweza pia kutuma wasaidizi wake kwenda kutoa pole.

“Waziri Mkuu Majaliwa (Kassim) alikwenda kuhani na kuaga miili ya watu waliopoteza maisha mjini Bukoba, sasa huoni kuwa huo ni uwakilishi mkubwa sana wa Rais?” alihoji.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania(GST), Profesa Abdulkarim Mruma anasema tetemeko hilo ni kubwa kwa nusu ya kipimo cha juu cha Richa 10 na limezidi kipimo cha chini cha ukubwa wa Richa tatu. Anasema limezidi lililotokea Dodoma hivi karibuni.

Profesa Mruma alisema tetemeko hilo limesababishwa na mpasuko wa ardhi katika Bonde la Ufa la magharibi karibu kabisa na Ziwa Victoria .

Ieleweke kuwa, mbali ya kupoteza Watanzania wenzetu 16, pia tetemeko hilo lilisababisha uharibifu mkubwa wa majengo, miundombinu na kuongeza umasikini kwa wananchi.

 

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu) Salum Kijuu, anabainisha kuwa mbali na kusababisha vifo, mchanganuo wa athari za tetemeko la Bukoba, unaonesha kuwa kuna jumla ya nyumba 840 ambazo zimebomoka, 1,264 zimepata nyufa kubwa. Watu 253 walipata majeraha na kuvunjia viungo pia.

Kalimbe Kagasheki, mmoja wa waathirika wa tetemeko hilo, ambaye nyumba yake ilianguka, pamoja na kuendelea kushangaa ukimya wa Rais Magufuli, pia aliishangaa serikali kwa kuruhusu baadhi ya watu aliowaita “wahuni” kutoa misaada “inayochekesha.”

“Lazima tuseme ukweli, yaani watu wanakufa, wanapoteza viungo, wanageuka kuwa masikini kwa kuanguka nyumba zao, leo taasisi au viongozi wa serikali wanakuja na misaada ya biskuti?” alihoji, akisikika kutoa sauti ya ukali.

Katika hali ya kushangaza, Serikali imetoa kauli kuwa wahanga wa tetemeko hilo wajijengee nyumba zao wenyewe kwakuwa michango iliyokusanywa imeelekezwa katika Taasisi za Serikali.

Kauli hii imeibua mjadala mkali kwani wengi wanakumbuka kuwa wafanyabiashara na wadau kadhaa waliitoa michango yao Septemba 13 wakilenga kuwasaidia wahanga tena mbele za Waziri Mkuu.

 

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alinukuliwa kupitia Televisheni ya Taifa(TBC) akiahidi Serikali kugharimia athari za tetemeko hilo kitu ambacho leo hii kinaelezwa kwa lugha tofauti.

Hadi sasa, inavyoonekana, ipo misaada mingi imekusanywa na serikali, lakini haijawafikia walengwa au imewafikia wasiopaswa. Kwani wengi bado wanalalamika na kuona serikali yao haijawasaidia sana.

Zaidi pia waathirika na waathiriwa wanahoji uwepo na misaada inayotakiwa kutolewa na Mfuko wa Maafa wa Taifa – ukiwa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ambao kazi yake kubwa ni kukabiliana na matokeo ya majanga, ikiwamo matetemeko makubwa.

Wengi wanahoji, Je, mfuko huu wa maafa unahitaji nao kupewa msaada ili utoe misaada? Mbona hadi sasa haujaeleza umma umetoa kiasi gani kwa wahanga wa tetemeko la Kagera au nao wanasubiri ratiba ya Rais Magufuli atakapoamua kutembelea Kagera kuzungumza na waliopata majanga, ili nao watoe tathmini?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *