TUCTA Mwanza wataka ‘Bunge la posho’ livunjwe

Jamii Africa

UONGOZI wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), mkoani Mwanza, umetoa kauli nziti ukitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano kuvunjwa kwa maelezo kwamba limeshindwa kusimamia na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Umma.

Katibu wa TUCTA Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Mwendwa

Katika kauli yake Jumatano Januari 18, 2012, Katibu wa TUCTA Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Mwendwa alipendekeza Rais Jakaya Kikwete kulivunja Bunge kwani sasa limegeuka kuwa kinara wa kuidhinisha matumizi makubwa ikiwa ni pamoja na posho kubwa kwao na kwa vigogo Serikalini.

Mwendwa amesema Wabunge wa Bunge la sasa wanaonekana kujali zaidi maslahi yao binafsi, badala ya Watanzania na maendeleo ya taifa kwa ujumla, hivyo chombo hicho kimepoteza sifa ya kuwa mhimili mkuu wa nchi.

Kiongozi huyo amesema Bunge limeonekana kushindwa kabisa kuisimamia Serikali kwa mujibu wa sheria za nchi, hivyo Rais hana budi kulivunja na kuitisha Uchaguzi mwingine.

Hata hivyo, utaratibu uvunjwaji wa Bunge ni mgumu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977, utaratibu ambao unaigharimu hata serikali na Rais mwenyewe.

Kwa mujibu wa Mwendwa, wabunge wengi waliopo bungeni wanaonekana kuwa na lengo la kuwatalawa wananchi wao, na si kuwahudumia na kuwasilisha mawazo yao katika chombo hicho, na kwamba wamekuwa vinara wakubwa wa kuidhinisha matumizi makubwa ya posho zao na vigogo wengine waliopo katika taasisi na Wizara mbali mbali.

“Tanzania ya leo ipo kwenye wakati mbaya sana. Bunge limeshindwa kabisa kuisimamia Serikali juu ya matumizi mabaya ya fedha za umma, badala yake limegeuka kuwa chombo cha kuidhinisha matumizi makubwa posho zao na vigogo wengine Serikalini.

“Wabunge wengi wanaonekana wapo kwa ajili ya maslahi yao bungeni. Hawawajali kabisa wananchi waliowachagua….hivyo tunamuomba sana Rais Kikwete ni bora alivunje hili Bunge maana Watanzania hawatapona kwa mtindo huu wa posho ya 200,000”, alisema Katibu huyo wa TUCTA Mkoa wa Mwanza.

Mwendwa ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti nchini (RAAWU), Kanda ya Ziwa alikwenda mbali zaidi na kusema: “Kwa sasa Bunge linaonekana kumtumikia kafiri ndiyo maana wameshindwa kuidhibiti Serikali kwa sababu nao wanajali zaidi maslahi yao binafsi”.

Alisema, wapo baadhi ya wabunge ni wajumbe wa bodi za taasisi au idara fulani zaidi ya tano, na kwamba kwa hali hiyo wamekuwa wakiwaza vikao tu ili walipane posho, na alitoa angalizo kwa wabunge kuacha mara moja kujipendelea wao wenyewe, bali waishinikize serikali iwalipe mishahara stahili watumishi wa Serikali na si kama ilivyo hivi sasa.

Mwendwa anasema nchi yoyote duniani ikizungukwa na wezi kamwe wananchi wala taifa halitapata maendeleo, na kwamba inavyoonekana hata serikali imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi, hivyo taifa la Tanzania linakabiliwa na ombwe la uongozi na inatakiwa Katiba mpya haraka iwezekanavyo.

Aliitaka pia Serikali kusikiliza kilio cha wafanyakazi wake, ikiwa ni pamoja na kuwaongezea mishahara na marupurupu, na kusema madaktati, walimu, askari polisi, watumishi wa kawaida na hata maofisa kilimo na mifufugo wanalipwa ujira kidogo sana ikilinganishwa na kazi kubwa wanazozifanya kila siku.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

1 Comment
  • Naunga mkono hoja 100%. Jamaa hawa wametumia hela za mikopo kununua kura halafu wanataka kutumia kodi zetu kulipa maden hayo! Haiwezekani. Watanzania wasipo andamana nitaandamana peke yangu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *