SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), limesema lipo tayari kutangaza mgogoro mkubwa na Serikali, utakaoambatana na migomo nchi nzima, iwapo Rais Jakaya Kikwete ataridhia nyongeza kubwa ya posho za Wabunge.
TUCTA imesema, haipo tayari kuona Serikali ikiwapa maslahi makubwa wabunge, huku ikionekana kukataa kulipa madeni ya wafanyakazi, wakiwemo walimu, na kwamba Serikali itarajie migomo isiyo na kikomo endapo itabariki posho hizo.
Kauli hiyo imetolewa hii leo Jijini hapa na Katibu wa TUCTA mkoa wa Mwanza, Ramadhan Mwendwa, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na posho mpya za wabunge.
Mwendwa ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti nchini (RAAWU), Kanda ya Ziwa alikwenda mbali zaidi na kusema, wafanyakazi wapo tayari kuendesha migomo isiyo na kikomo kupinga hatua hiyo aliyoiita ya ubaguzi wa hali ya juu.
“Tunamwambia Rais Kikwete kwamba, tutatangaza migomo nchi nzima kupinga ubaguzi wa namna hii. Hatukubali hata kidogo!. Kama noma na iwe noma katika hili.
“Hatupo tayari kukubali kwamba watumishi wengine wanalipwa mishahara kidogo, lakini wabunge ndiyo Serikali inawajali zaidi. Nasema tutatangaza mgogoro na Serikali kama itabariki hizi posho”, alisema Mwendwa huku akionekana kukerwa na hatua hiyo.
Hivi karibuni kumeibuka marumbano kati ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wake, Dk. Thomas Kashilila, ambapo Katibu wa Bunge amesema wabunge hawajaongezewa posho kutoka 70,000 hadi 200,000.
Lakini juzi Spika alikaririwa akisema tayari wabunge walishaanza kulipwa posho mpya za sh. 200,000, kwa siku moja kuanzia Novemba 8 hadi 11 na kikao cha tano cha Bunge lililomalizika hivi karibuni.
Kauli hizo zinazopingana baina ya Spika na Katibu wa Bunge, zimeonekana kuibua malalamiko mengi kwa wananchi wa kada mbali mbali, jambo linaloweza kupandikiza chuki na hasira dhidi ya wananchi, wabunge na Serikali kwa ujumla.
Katika hilo, Mwenda alisema: “Kwa sasa taifa letu hili linaonekana linaongozwa kienyeji kabisa. Huyu anasema kivyake…sisi tunamtaka Rais aueleze umma wa Watanzania kama alishabariki posho hizi ama la”.
Aliwaomba wananchi kote nchini kuhakikisha wanawahoji wabunge wao punde wapokuwa majimboni kuhusu kukubali nyongeza hizo za posho, na kwamba ni vema wakachukizwa na kitendo hicho cha ubaguzi wa kimaslahi.
Hata hivyo, aliwataka wafanyakazi kote nchini kuanza kudai haki na maslahi yao, ili kila mmoja anufaike na rasilimali za nchi, badala ya rasilimali hizo kuwanufaisha wabunge peke yao.
Kwa mujibu wa Katibu huyo wa TUCTA mkoa wa Mwanza, Mwendwa, Serikali ya Tanzania inapaswa kuiga mfano wa nchi ya Botswana kwa kuwalipa vizuri wafanyakazi wake, ili kuondoa migogoro na migomo ya mara kwa mara.
*PICHANI: Katibu wa TUCTA mkoa wa Mwanza, Ramadhan Mwendwa, akiwaonesha waandishi wa habari vitabu vya sheria za utumishi wa Umma leo ofisini kwake
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza