Hivi karibuni tunashuhudia duniani nchi mbalimbali zikihaha kuhakikisha suala la kodi linakuwa la kipaumbele. Kuhakikisha nchi zinapata kodi stahiki toka kwa vyanzo vyote hususan vile vya ndani. Suala hili kwa uzito wake limekuwa miongoni mwa ajenda kuu katika mikutano mbalimbali ya kimataifa mathalani ule wa G20 wa hivi karibuni. Kwanini sasa?
Suala hili, kwa nchi zinazoendelea zenye kuendesha serikali zao kwa kutegemea kiasi kikubwa misaada toka nje ya nchi zao ni la muhimu sana. Kwani, kiasi kikubwa sana kimekuwa kikipotea katika mianya mbalimbali ya ukwepaji kodi huku nchi hizo zikiendelea kutumia muda mwingi na rasilimali katika kusaka misaada.
Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mnamo Machi 13, 1995 katika hotuba yake maarufu ambayo aligusia “nyufa” zenye kuangamiza taifa endapo zisiposhughulikiwa ilikuwa pia suala la kutokukusanya kodi.
Mwalimu, alienda hatua kadhaa mbele kuweza kuonyesha na kudhihirisha uhusiano wa karibu sana kati kutokukusanya kodi na rushwa.
“Serikali corrupt haikusanyi kodi. Itabaki kufukuzana fukuzana na vijitu vidogo vidogo mabarabarani hivi basi” – Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa kiasi kikubwa yale ambayo Mwalimu alikuwa akitahadharisha juu ya kuacha kukusanya kodi na hasa kukusanya kodi kwa wote yaani wananchi na taasisi zote na sio kuweka msukumo upande mmoja, kwa wananchi wadogo wadogo bado mpaka sasa hali inaendelea. “Sikio la kufa halisikii dawa” wahenga walipata kunena.
Tunaona juhudi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kuhakikisha kodi inakusanywa. Kubuni njia mbalimbali mathalani matumizi ya vifaa vya kieletroniki vya EFD, na malipo mengine kama ya kulipia ushuru wa magari kwa kupitia mitandao. Juhudi ambazo si za kubezwa. Lakini bado haiondoi fursa ya kuhoji kwa mapana; hasa juu ya ukusanywaji wa kodi stahiki toka kwa vyanzo vya mapato vikubwa kama makampuni makubwa ya kimataifa na wafanyabiashara wakubwa.
Kwa haraka haraka; bado TRA inajihusisha sana na kutumia nguvu nyingi kwa vile “vijitu vidogo vidogo” ambavyo Mwalimu Nyerere alikuwa akivigusia huku makampuni makubwa na wafanyabiashara wakineemeka kutokana na mazingira duni ambayo tumejiwekea wenyewe kupitia sheria na sera mbalimbali zenye kutoa misamaha mikubwa ya kodi achilia mbali uwezo wa makampuni hayo kutumia wataalamu katika kukwepa kulipa kodi.
Mazingira ya kisera ambayo tunapaswa kuzingatia ni pamoja na kuhakikisha ulipwaji wa kodi unakuwa wa haki kwa kila raia. Tajiri maarufu duniani, Warren Buffet alipata kukiri kupitia vyombo vya habari kuwa sekretari wake, Debbie Bosanek alikuwa analipa kodi kiwango kikubwa sana kuzidi hata ambacho yeye analipa. Bosanek alikuwa akilipa kodi ya kiwango cha asilimia 35.8 cha kipato chake huku bilionea Buffet alikuwa akilipa asilimia 17.4 tu!
Hali hiyo iliweza kutokea tu kutokana na mfumo wa kisera wa kodi uliopo nchini Marekani. Jambo ambalo liliushtua ulimwengu na hasa wanaharakati wanaopigania haki katika masuala ya kodi.
Tukumbuke hayo yaliweza kutokea katika nchi kama Marekani yenye mifumo imara ya kuhakiki, kufatilia kodi na kukusanya kodi; je hali ipoje kwa nchi kama yetu Tanzania ambapo tunamifumo dhaifu mingi katika kufatilia na kuhakiki ulipwaji kodi? Ni matajiri wangapi kwa utashi na makusudi wanakwepa kodi huku walalahoi wakizidi kubanwa kwa kodi kadha wa kadha.
Baya moja alihalalishi baya jingine, hivyo si lengo la uchambuzi huu wa makala kuwahamasisha wananchi wa kipato cha chini kutolipa kodi; bali hasa kuzisukuma mamlaka husika na watendaji kusimamia vyema haki katika kutoza kodi stahiki kwa kila raia, taasisi, makampuni na wazalishaji.
Uwepo wa sheria zenye kutoa mianya kutumiwa vibaya na wawekezaji hususan wa nje na makampuni makubwa ni pamoja na; sheria ya ukanda wa uzalishaji kwa ajili ya kusafirisha (Export Processing Zone Act, 2002), Sheria ya mwaka 1997 ya Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Act, 1997) na Ukanda maalumu wa uzalishaji ya mwaka 2005 (Special Economic Zone, 2005).
Katika sheria hizo tunaweza kuna misamaha ya ulipaji wa kodi kwa miaka kumi. Lakini pia misamaha katika bidhaa (capital goods and raw materials) ambapo huko nako kuna kunaweza kutumika kuepa kodi inayopaswa kulipwa.
Tukiangalia sheria nyingine ya kodi ya mapato kwa makampuni; “corporate income tax” ambapo kwa Tanzania makampuni yananeemeka nafuu ya punguzo la kodi kwa asilimia 25. Hii ni tofauti hata kwa nchi nyingine za kiafrika katika sheria hiyo hiyo. Tukichukua mfano: Nigeria ambapo kwa sheria hiyo hiyo wao wanatoza nafuu ya kodi kwa asilimia 30, Ghana kwa asilimia35 au Afrika Kusini kwa asilimia 28!
Kisingizio kikubwa kikiwa ni kuvutia uwekezaji na kutoa fursa ya ajira na uzalishaji; jambo ambalo linapingwa na wataalamu wa kiuchumi kuwa kiwango cha misamaha hakiendani na namna ambavyo taifa linaneemeka kwa kodi.
Eneo hili la misamaha ya kodi ni eneo ambalo kwa miaka mingi sasa limekuwa likiandikwa na kulalamikiwa na Mkaguzi mkuu na mdhibiti wa hesabu za serikali (CAG); hii ikiwa ni pia kutoa ushauri wa kuwekwa ukomo kisera na kisheria katika kiwango cha kutoa misamaha hiyo. Kwa mwaka 2011 CAG alishauri serikali iweke aidha ukomo wa utoaji wa misamaha ya kodi isiyozidi asilimia 5 ya jumla ya mapato yaliyokusanywa au kuacha kabisa kutoa misamaha hiyo ya kodi kwa makampuni na watu ambao kiuhalisia wanaouwezo kabisa wa kulipa kodi.
Na ifahamike, wanaoneemeka sana na misamaha hii ni makampuni makubwa na si mashirika ya kidini kama ambavyo miaka michache iliyoaminishwa kama njia ya propaganda kuendelea kutetea uwepo wa misamaha.
Uchambuzi wa shirika la Uwazi uliotolewa mwaka 2010 na kupewa jina; “Misamaha ya Kodi Tanzania: Ipo juu sana na kutufanya kwa kiasi kikubwa kutegemea misaada ya nje” ulibainisha misamaha ya kodi iliyotolewa katika mwaka wa kibajeti wa 2008/09-2009/10 makampuni ya madini yalipata misamaha takribani asilimia 7.51 huku makampuni binafsi na watu binafsi wakipewa misahama ya asimilia 6.00. Na vinara wa kuneemeka na misamaha ya kodi wakiwa ni wale wenye vyeti vya uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Ukuzaji wa Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambapo inafikia asilimia 45. Asilimia kubwa ya makampuni yenye vyeti/hati hizo ni makampuni ya kimataifa.
Taasisi za kidini kwa uchambuzi wa bajeti kwa mwaka huo zilikuwa zinapata kwa asilimia 0.05 tu huku mashirika yasiyo ya kiserikali yakiwa yanapata asilimia 4.06! Huo ndiyo ukweli. Huo ndio uhalisia.
Uhalisia wa mianya iliyopo na mbinu zinazotumika na makampuni hasa ya kimataifa ni nyingi sana ambazo zinapaswa kuendelea kuanikwa kwa makala zijazo kwa manufaa hasa ya wananchi kufahamu uhalisia wapi mianya ya upotevu wa fedha inakuwapo ambapo serikali inashindwa kutumia fursa hizo ili kuhakikisha inapata fedha za kuzitumia katika kutoa huduma bora za kijamii kama elimu, afya, maji safi na salama.
Ni wakati sasa wa kusema inatosha na kuamua kuziboresha sera na sheria zetu za Tanzania na kuhakikisha zinatoa fursa madhubuti za kukusanya kodi na kuondosha mianya yote ya ukwepaji kodi. Tunao uwezo kabisa wa kuboresha makusanyo ya kodi na kumudu kutekeleza mikakati mbalimbali ya kimaendeleo kwa fedha zetu wenyewe stahiki endapo tutatumia vyema wataalamu wetu na kuhakikisha sera, sheria na mifumo inakuwa imara kudhibiti ukwepaji wowote unaoweza kutokea.