Tume ya Haki za Binadamu yamshukia Kamanda Kamuhanda mauaji ya Mwangosi

Elias Mhegera
  • Apingana na Jaji Ihema wa Kamati ya Nchimbi
  • Aikingia CHADEMA kifua

    Jaji Amir Manento
  • Amshushua John Tendwa

Siku moja baada ya kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani kulisafisha jeshi la polisi na mauaji ya mwandishi wa kujitegemea Bw. Daud Mwangosi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imemshukia bila huruma Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Bw. Michael Kamuhanda. Baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na tume hiyo yenye jukumu la kikatiba kuangalia suala la haki za binadamu na utawala bure Kamanda Kamuhanda ambaye hadi hivi sasa bado ameachwa kuongoza Mkoa wa Iringa alivunja sheria kadha wa kadha na ni uamuzi wake wa kuingilia mkutano wa CHADEMA ndio ulisababisha mauaji ya mwandishi Mwangosi.

 

Akitoa muhtasari wa ripoti hiyo Jaji Ameir Manento amesema kuwa uchunguzi wa tume yake ambayo imepewa madaraka ya kusimamia utawala bora na haki za binadamu amesema kuwa tukio la mauaji ya Mwangosi “limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora”

 

Akielezea undani wa tukio hilo Jaji Manento amekitetecha Chama cha Demokrasia na Maendeleo kuwa kilikuwa na haki ya kufanya mikutano yake ya ndani na katazo lililokuwa limetolewa na viongozi mbalimbali akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa lilikuwa ni kinyume na sheria na kanuni za utawala bora. Jaji Manento amesema kuwa CDM kilikuwa kimepata baraka zote za kuendelea na mikutano yake na jukumu la vyomob vya usalama lilikuwa ni kuhakikisha kuwa chama hicho kinapatiwa ulinzi.

 

“CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina usajili wa kudumu. Chini ya sheria ya vyama vya siasa (Cap. 258 RE. 2002), vyama vya siasa vyenye usajili vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa “Afisa wa Polisi” wa eneo husika. Baada ya taarifa kutolewa chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi na “security agencies” (mawakala wa usalama)” umesema muhtasari wa ripoti hiyo.

 

Taarifa hiyo imefafanua kuwa “ kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji wa majukumu yake alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11(a) na (b) na sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika. Kwa maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora”.

 

Kimsingi Tume hii ya kudumu inamtaja Bw. Kamuhanda kama mhusika mkuu wa usababishaji wa mauaji ya Mwangosi na kuwa kutokana na uvunjaji wa wazi wa sheria vyombo vilivyojuu yake vinatakiwa kumchukulia hatua ikiwemo kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka. Ni yeye aliyetoa amri ya kulipua mabomu ya machozi eneo lile, ambalo mojawapo ndilo linalodaiwa kumlipua Bw. Mwangosi. “RPC aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA” amesema Jaji Manento.

 

Pamoja na hilo Tume ya Haki za Binadamu imekaripia vikali uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa Bw. John Tendwa kutoa maagizo ya kuingilia shughuli za kisiasa wakati hana mamlaka hayo. “hatua ya Msajili wa vyama vya siasa, Mhe. John Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo yaliyotolewa ndani ya barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Na. 1 ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa pia ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) Kifungu cha 11(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila ya kuingiliwa.” Imesema taarifa hiyo fupi.

 

Bila kuuma maneno tume hiyo ambayo inaongozwa na miongoni mwa majaji wenye kuheshimiwa sana nchini na ambaye wapigania haki za kiraia wanamtambua kama kinara wa haki za kiraia katika mahakama amesema kuwa haki za msingi za raia kupata habari na kufanya mikutano yao iliingiliwa na vyombo vya dola na hivyo kuvunja misingi ya utawala bora. Jaji Manento amesema kuwa “Haki hii imekiukwa kwa kiasi kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Nyololo Mufindi kwa kuwa waandishi wa habari na wafuasi wa CHADEMA walizuiwa na Polisi kufanya shughuli zao za kupata habari na za kisiasa. Huu ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa kuwa hali hiyo inazorotesha au inafifisha uhuru wa habari.”

 

Tume katika baadhi ya mapendekeo yake imekitaka CDM kutii maagizo ya serikali na kuwa “Pale wanapogundua kuwa pana uonevu au upendeleo ni vyema busara ikatumika ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea”. Vile vile aliliasa Jeshi la Polisi pamoja na Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua maamuzi bila kuonekana inapendelea baadhi ya vyama na kutolea mfano kuwa wakati CDM walitakiwa kutii uamuzi wa kuzuia mikutano jeshi la polisi liliacha mkutano wa CCM huko Bububu uendelee. “Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria” amesema Jaji Manento.

 

Ripoti ya Jaji Manento imekuja siku moja tu baada ya Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Emmanuel Nchimbi kulisafisha jeshi la polisi na kurushia lawama Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Kamati hiyo ambayo ilipingwa na CDM mapema iliongozwa na Jaji Ihema huku ikihusisha jeshi la polisi, vyombo vya habari na JWTZ. Ripoti ya Jaji Ihema imepokelewa kwa kebehi na wananchi wengi hasa baada ya kukwepa kujibu maswali ya msingi huku Waziri Nchimbi akieleza kuwa ripoti hiyo inayo mambo ambayo yanaweza kumsaidia mtuhumiwa wa mauaji ya Mwangosi kuwa huru.

 

Vyanzo vya ndani vya kuaminika toka Tume ya Haki za Binadamu vinadokeza kuwa Jaji Manento alikasirishwa sana na ripoti ya Kamati ya Nchimbi ambayo aliona imetumiwa kisiasa kulisafisha jeshi la polisi. “Ripoti ya Jaji Manento ilikuwa itolewe kama wiki mbili kuanzia sasa kwani ilikuwa bado inaandikwa kitaalamu kama ilivyo kawaida yake” amedokeza mmoja wa watu wa karibu na tume hiyo. “Baada ya kusoma ripoti ya Ihema uamuzi ulichukuliwa na Jaji Manento kuharakisha kutoa muhtasari wa ripoti yake ili kuhakikisha kuwa taarifa za kamati ya Nchimbi hazitumiwi vibaya kuwasafisha watu” amesema mpashaji habari wetu.

Na. M. M. Mwanakijiji na Waandishi wa Fikra Pevu

2 Comments
  • kwanza niipoe pole familia ya barlow kwa yaliyotokea, Mungu ailaze roho ya marehemu Barlow pema peponi amin, hapa ndipo tulipofika kama taifa uhai wa binadamu hauna Thamani kabisa kwa muuaji, lakini cha kusikitisha muuaji anasahau kwamba na yeye ni wa kufa tu hata angekuwa na hali bora kiasi gani.

    Jeshi la Polisi kwa sasa lisiwaruhusu viongozi wa juu wa jeshi hilo kuwa peke yao bila walinzi wao kwa wakati woote wanapokuwa nje amaa ya ofisi au hata kwenye mambo yao binasfi ili kuwepo ulinzi kwa muda wote hii itasaidia kuwafanya wawe salama kwa muda woote.

  • HIVI HII TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALABOBA ILIKUWEPO AU IMEPEWA MENO BAADA YA KUUNDWA VYAMA VINGI VYA SIASA HAKI ZA BINADAMU ZIMEVUNJWA SANA TANZANIA JE VIKONGWE WENYE MACHO MEKUNDU WAMEUAWA KUANZIA LINI KAMA SI TOKA AWAMU YA KWANZA YA UONGOZI KWELI TUME MUNAWEZA KUTHUBUTU KUSEMA MULIKUWA MUMEZALIWA AU MIMBA ILIKUWA HAIJATUNGWA.WATANZANIA WENGI WAMECHUNWA NGOZI WAKAUAWA HIVI NI LINI ANGALAU MULIKEMEA TU HIVI KATI YENU KUNA AMBAYE ANA DINI ANAMWABUDU NANI? AWMU YA TATU YA UONGOZI UJAMBAZI ULIKITHIRI WATU WALIDHALILISHWA WALIVULIWA NGUO NA MAJAMBAZI WENGINE WALIUAWA JE KUNASIKU MULIISAIDIA SERIKALI HATA KUWAKEMEA MAJAMBAZI AU MULISHIRIKI KUMSINGIZIA MUNGU KATOA NA KATWAA JINA NAMUNGU LIHIMIDIWE ,AWAMU YA NNE MAUAJI YA ALIBINO YALIKITHIRI NI KAMA VILE NA NYINYI MULIHALALISHA UKIPATA KIUNGO CHA ALIBINO NI UTAJIRI NINAWAOMBA LABDA IUNNDWE TUME NYINGINE NYINYI MUSITHUBUTU KUWAZUNGUMZIA ALIBINO MPAKA ALIKUJA ALIBINO ANI KUSUTA WATANZANIA SASA MAUAJI YA KIDINI YANANUKIA HIVI MUNAYO CV YA KUYAKEMEA YAANI MUMEFULIA HEBU JIUZULUNI TENA HARAKA WANAFIKI WAKUBWA KUZIMU KUMEJAZANA WATANANIA WENGI WALIODHULUMIWA UHAI WAO KUTOKANA NA UZEMBE WENU

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *