MWANAFUNZI mmoja tu kati ya wanafunzi wote 17 waliofaulu darasa la saba mwaka 2012 katika shule ya msingi Njenga iliyopo kilometa 80 kutoka mjini Tunduru mkoani Ruvuma ndiye aliyejiunga na masomo ya sekondari ya Nalasi kidato cha kwanza mwaka huu .
Utafiti uliofanyika katika shule hiyo umebaini kuwa mwamko wa elimu katika kijiji hicho ni duni kwa kuwa wanafunzi wengi wanaofaulu shule hiyo ya msingi hawajiunga na masomo ya kidato cha kwanza hali ambayo inawakatisha tamaa walimu wanaofundisha katika shule hiyo.
Utafiti huo umebaini kuwa wanafunzi wengi wanaofaulu katika kijiji hicho cha Njenga wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na mila na desturi za msondo,unyago na jando hali ambayo inasababisha wanafunzi wengi wa kike kupata mimba, utoro wa kudumu na wengine kuolewa.
Mwaka 2010 wanafunzi waliofaulu darasa la saba katika shule ya msingi Njenga walikuwa ni 41 kati ya hao ni wanafunzi watatu tu ndiyo waliojiunga na kidato cha kwanza na kwamba mwaka 2011 wanafunzi waliofaulu darasa la saba katika shule hiyo walikuwa ni 46 na waliojiunga na kidato cha kwanza ni wanafunzi saba tu.
Katika shule ya msingi Ruanda iliyopo katika kata ya Nakapanya wilayani Tunduru inaonyesha kuwa wanafunzi wote 26 waliofaulu darasa la saba mwaka 2011 katika shule hiyo hawajajiunga na kidato cha kwanza.
Kitendo cha wanafunzi wote waliofaulu kutojiunga na kidato cha kwanza kunadaiwa kuwavunja moyo walimu ambao walikuwa wanafundisha katika shule hiyo ya Ruanda hali ambayo imesababisha shule hiyo mwaka 2012 kutofaulisha mwanafunzi hata mmoja kwenda seondari.
Katika shule ya sekondari Malumba wilayani Tunduru waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza msimu huu ni wanafunzi 149 lakini wanafunzi walioripoti hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu ni wanafunzi 48 sawa na asilimia 33.
Hata hivyo baadhi ya wadau wa elimu wamedai kuwa viongozi wa serikali za Vijiji wanastahili kubeba lawama huku wakiwataka viongozi kutochanganya elimu na Siasa kwa kuboresha mbinu za kufundishia na kuchukua hatua kwa Wanafunzi ambao wamekuwawakibainika kuchaguliwa huku wakiwa hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu.
Mkuu wa shule ya sekondari Mgomba Elis Banda alishauri kupunguzwa kwa idadi ya vitabu vya kufundishia huku akiitaka serikali kutoa maelekezo ya vitabu vya kununuliwa tofauti na sasa ambapo kumekuwa na maelekezo ya kuwataka wakuu wa shule kutumia vitabu kutoka katika kampuni ya EMACK pamoja na Muingiliano wa sekula pia ni kikwazo katika elimu.
“Sasa walimu wanalazimishwa kusajiri watoto wote kufanya mitihani bila kuangalia wakati huo huku mamlaka zikiwataka walimu kuwafukuza watotowasiofika shule katika kipindi cha miezi mitatu na serikali ikihamasisha na kuwapeleka shule wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochelewa kuripoti Shuleni ni kikwazo kingine ambacho kimekuwa kikiwafanya walimu kufundisha kwa kulipua na kuchangia kushusha kiwango cha elimu’’,alisema.
Mkuu wa Shule ya sekondari Lukumbule Mathias Katto anavitaja vikwazo vingine vinavyochangia kushusha taaluma wilayani Tunduru kuwa shule zao kutokuwa na walimu wa masomo ya Sayansi, maktaba na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Wazazi na walezi wengi katika wilaya ya Tunduru wanadai kuwa watoto wa kike hawastahili kusomeshwa elimu ya sekondari kwa kuwa hawana faida yeyote zaidi ya kuolewa kwa madai kuwa wao ni kitega uchumi na wanatakiwa kuwahudumia wanaume kulingana na mila na desturi za kabila la wayao.
Afisa elimu sekondari wilaya ya Tunduru Ally Mtamila mebainishwa kuwa Mahusiano mabaya kati ya Walimu,wazazi,walezi na wanafunzi ni miongoni mwa vikwazo vya maendeleo ya elimu Wilayani Tunduru hali iliyosababisha Wilaya hiyo kupata matokeo mabaya kwa wanafunzi waliofanya mitihani ya Kidato cha Pili Nne katika kipindi cha mwaka 2011/2012 .
Kaimu Afisa elimu wilayani Tunduru Flavian Nchimbi
Mtamila amewaasa wazazi,walezi na walimu kushiriki katika usimamiaji wa Watoto wao kwa kufuatilia masomo ili waweze kuyapenda masomo na kukemea watoto ambao wanaacha kuzingatia masomo na kujiingiza katika vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo ya elimu wilayani humo.
Kwa mujibu wa tarifa ya maendeleo ya elimu ya wilaya hiyo mwaka 2011 matokeo ya Kidato cha pili yanaonyesha wilaya hiyo ilifaulisha kwa wastani wa asilimia 35, huku takwimu hizo kwa upande wa matokeo ya Kidato cha Nne katika kipindi cha mwaka 2012 zikionesha kuwa Wilaya hiyo ilifaulisha kwa wastani wa asilimia 59.4 kiwango ambacho kiliifanya Wilaya hiyo kushika nafasi ya mwisho katika mkoa wa Ruvuma
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Chande Nalicho amekiri ya hali elimu inayotokana na mwamko duni katika wilaya hiyo ni mbaya hivyo kuchangia kushusha kiwango cha elimu ya msingi na sekondari.
Amesema wilaya hiyo kila mwaka inakuwa ya mwisho kitaaluma katika wilaya za mkoa wa Ruvuma ambapo kwa mwaka jana wilaya hiyo pia ilikuwa ya mwisho kwa kwa kupeleka wanafunzi wachache waliochaguliwa kidato cha kwanza ambao walichaguliwa walikuwa ni 2788 hata hivyo walioripoti hadi kufikiwa mwezi Aprili mwaka huu ni 1700 tu.
Utafiti uliofanywa katika baadhi ya shule za msingi wilayani Tunduru umebaini kuwa mwamko wa elimu katika maeneo mengi hauridhishi kwa kuwa wanafunzi wengi wanaacha shule kwa utoro,mimba na kuolewa kutokana na mila na desturi zinazoendelezwa na wakazi wa wilaya hiyo wengi wao wakiwa ni wa kabila la wayao.
Hiyo ni balaa la kutosimamia ipasavyo mpango wa MKUKUTA maana tatizo lwa watu wa Tunduru yaonekana ni umasikini ndo mana hawendi shule.