Mwanamke aliyetuzwa na serikali ya Marekani apokewa Jijini Mwanza kwa nderemo

Jamii Africa

Na Juma Ng’oko, FikraPevu – Mwanza

MAMIA  ya  wakazi wa Jiji la Mwanza pamoja na vitongoji  vyake, hasa wanawake wakiwemo  askari  wa Jeshi la Polisi, jana walifurika  kwenye viwanja ya ukumbi wa  Gandhi jijini,  kwa ajili ya kumpokea  mwanamke mwenzao, Maimuna Kanyamala,  aliyetuzwa  ngao pamoja na cheti  cha  ujasiri   katika  kutetea haki za wanawake na wasichana  mkoani hapa.

Kanyamala ambaye ndiye Mkurugenzi wa shirika  la Kivulini; shirika  lisilokuwa la Kiserikali Jijini hapa  amepata  tuzo  ya ujasiri  mwaka huu kutoka  serikali ya Marekani  kutokana na  mafaniko  katika  suala zima la  kutetea haki za wanawake na wasichana.

Maandamano hayo yalianzia katika uwanja wa ndege  majira ya saa 2 asubuhi hadi Gandhi Hall (majira ya saa 4 asubuhi)  kupitia barabara kuu la lami, Airport –Jijini kati na  yaliyepokea   Mkuu  wa Wilaya ya Nyamagana, Said  Amanzi ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Pamoja na mapokezi hayo ,  Kanyamala  alikabidhiwa  mavazi ya kishujaa pamoja na silaha za jadi  zinazotumiwa na kabila la  Wasukuma, ikiwemo mkuki na ngao ili aweze kukabiliana vyema na  wanaume wenye tabia za ukatili dhidi ya wanawake.

“  Wito wangu  kwa wanawake  ni kwamba ondokaneni na kasumba kwamba mkiwezeshwa mnaweza; kwa hakina ninyi mnaweza hata bila kuwezeshwa na ndiyo maana  mwamke mwenzenu Maimuna  ameleta heshima ndani na nje ya mkoa  wa Mwanza  mwaka huu “ alisema  Mkuu  wa Wilaya  wakati  akihutubia.

Alifafanua kuwa  tuzo hiyo imepatikana kutokana  na kazi  nzuri iliyofanywa  na mwanamke mwenzao; kazi ambayo  ilikubalika ndani na nje ya nchi.

Mkuu  huyo wa Wilaya aliwaasa wanawake wajitume katika kufanya kazi za uzalishaji mali pamoja na mambo mengine, waweze kuheshimika katika jamii.

Amanzi aliwataka  wanawake  wasifanye mapinduzi  ambayo  yanaweza kusababisha  migogoro isiyokuwa ya lazima baina yao na wanaume  kwa kisingizio cha kutetewa  kisheria.

“ Ninatoa wito tena kwa wazazi hasa Wasukuma kwamba  tafadhali wapeni nafasi za masomo  watoto wenu wa kike; na hapo ndipo tutakapopata wajasiri wengi  wanawake mkoani mwetu” alisisitiza  Mku huyo wa Wilaya.

Alisema  baadhi ya wazazi  katika kabila la Wasukuma  hawathamini  elimu kwa watoto wa kike, kitendo  ambacho kinawanyima fursa  wanawake katika masuala mbalimbali ya maendeleo mkoani hapa.

“ Kwa heshima ya kabila la Wasukuma, ninamkabidhi  kwa kumvalisha mkia wa nyumbu ikiwa ni ishara ya mnyama mpole, na pia ninamvalisha ngozi ya ng’ombe ambayo ni ishara ya mnyama ambaye anaishi na binadamu kama rafiki” alisema Mhangwa Mhangwa, wakati  akikabidhi zana za kimila  na kuongeza kwamba

“ Ninakukabidhi ‘shimbi’ na mkanda  wa ngozi kwa ishara kuwa utawaunganisha wanawake na wanaume katika masuala ya kuzuia ukatili; unyoya wa mbuni ni ishara ya ujasiri; ngao kwa ajili ya kujikinga na wenye tabia  za upinzani  wa harakati hizi pamoja na mkuki kwa ajili ya vita  dhidi  ya  wanaokaidi sheria zinazopingana na ukatili  dhidi ya wanwake” alisema Mhangwa  huku akishangiliwa na  umati wa wanawake.

Kwa upande  wake, Kanyamala  aliishukuru serikali ya Tanzania  ambayo ilishirikiana  bega kwa began a serikali ya Marekani  kwa ajili ya maandalizi ya  tuzo hiyo.

Alisema  tuzo hiyo imetolewa na ubalozi wa nchi ya Marekani, Balozi Altonso Lenhardt.

Kanyamala  alitumia fursa hiyo kuwataka wanawake wenzake washirikiane na shirika la Kivulini pamoja na serikali  kwa ajili ya kuwaelimisha wanaume ili wabadilike na kuchukia vitendo vya unyanyasaji  dhidi ya wanawake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *