TAASISI ya Twaweza imetoa utafiti wake leo Alhamisi Juni 15, 2017 na kueleza kwamba kiwango cha rushwa kwa watendaji wa umma kimeshuka ndani ya siku 500 tangu Rais Dkt. John Magufuli aingie madarakani ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Imeelezwa kwamba, vitendo vya rushwa katika kipindi hicho vimeshuka hadi kufikia asilimia 10, tofauti na miaka iliyopita huku utendaji kazi kwa watumishi wa umma nao ukiongezeka.
“Idadi ya wananchi wanaotaja rushwa au uongozi kama moja ya matatizo makubwa imepungua kwa kiwango kikubwa: kutoka asilimia 24 hadi 30 mwaka 2012-2015 mpaka asilimia 10 mwaka huu,” umeeleza utafiti huo.
Katika utafiti huo wa Sauti za Wananchi, imebainika hata hivyo kwamba, hali ya maisha kwa wananchi imezidi kuwa ngumu ambapo umaskini na uchumi duni umefikia asilimia 60 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo hali ilikuwa nusu ya kiwango hicho.
Utafiti huo uliotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, ulilenga kuangalia sekta mbalimbali tangu Rais Magufuli aingie madarakani na kuteua watendaji wakuu wa sekta hizo.
“Kipindi hiki kinatosha kuwapa wananchi mwenendo wa vitendo vya serikali na kuona jinsi ambavyo aina ya uongozi huu unavyoyagusa maisha yao ya kila siku,” ulieleza muhtasari wa utafiti huo ambao ulifanyika kati ya tarehe 31 Machi na tarehe 17 Aprili mwaka 2017 ukiwahusisha wananchi 1,805 wa Tanzania Bara.
Kwa upande mmoja, utafiti huo umesema, tatizo la rushwa limeshuka katika orodha ya kero kubwa za wananchi huku chanzo kikitajwa kuwa huenda ni msimamo mkali wa serikali ya awamu ya tano dhidi ya rushwa.
“Wananchi wanataja afya, elimu na maji kama matatizo ambayo si makubwa sana ikilinganishwa na miaka iliyopita. Inawezekana kwamba wananchi wanapokea juhudi zinazofanywa na serikali katika sekta hizi,” umeeleza utafiti huo.
Hata hivyo, wananchi wametaja tatizo la upungufu wa chakula kuwa ni kubwa sana, kuliko ilivyokuwa miaka iliyopita.
Matokeo hayo mapya yanaunga mkono matokeo yaliyopatikana na utafiti wa Sauti za Wananchi wa mwezi Februari 2017, ambapo wananchi nane kati ya kumi walisema kuna upungufu wa chakula kwenye maeneo yao.
“Umasikini (asilimia 60), upungufu wa chakula (asilimia 57) na afya (asilimia 40) ndio changamoto kuu zinazowakabili wananchi kwa sasa. Idadi ya wananchi waliotaja huduma za umma (afya, elimu na maji) kama matatizo makubwa matatu yanayoikabili nchi imepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita,” umebainisha utafiti huo.
Kwa mujibu wa utafiti huo, idadi ya wananchi wanaotaja upungufu wa chakula kama
tatizo kubwa imeongezeka ambapo asilimia 57 ya wananchi hao wamesema tatizo hilo ni suala la kipaumbele katika masuala matatu makubwa yanayoikabili Tanzania kwa sasa.
“Idadi hii imeongezeka ikilinganishwa na asilimia 7 hadi 20 ya miaka iliyopita,” umesema utafiti huo.